Novemba 25, mwaka 2015, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alifungua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulihutubia.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Magufuli alibainisha mambo kadhaa aliyokuwa ameyabaini wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 moja kwa moja kutoka kwa wananchi.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na suala la rushwa. Akasema suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayogusa wananchi.

Pili, ni Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Hapa akasema kumekuwa na upotevu wa mapato, hali ya kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi na uzembe.

Tatu, ni kuhusu ardhi. Alisema migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, mipango miji na kujenga maeneo ya wazi ni kero sugu.

Nne, alizungumzia Bandari, akisema kuna rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu.

Tano, ni sekta ya maji. Kwamba kulikuwa na changamoto kuhusu kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama. Pia huduma ya maji kupatikana mbali na makazi.

Sita, ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akibainisha kuwapo kwa ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa kukusanya kodi, hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabiashara wakubwa. Ni kweli kwamba tangu kuingia kwake madarakani kuna hatua kubwa zimepigwa katika utatuzi wa kero hizo na nyingine nyingi.

Hata hivyo, ni dhahiri kuwa bado utekelezaji dhidi ya kero hizo  kwa upande wa baadhi ya watendaji serikalini si wa kuridhisha. Kimsingi, Rais Magufuli binafsi anasikitishwa na hali hiyo, na kwa bahati, amekuwa muwazi mbele ya wananchi kuhusu hao wanaomuangusha.

Ni matarajio yetu kwamba wahusika hao wanaweza kurejea hotuba hiyo ya Rais Magufuli bungeni ili kujikumbusha dhamira na mwelekeo wa rais katika kipindi cha awamu ya kwanza ya uongozi wake.

Tumemsikia rais akilalamika dhidi ya baadhi ya viongozi kwenye ziara yake katika mikoa ya kusini. Hali hii si nzuri kwa wote waliopewa dhamana. Lakini pia JAMHURI tunawapongeza viongozi wote wanaofanya kazi kwa bidii bila kumwangusha rais.

Please follow and like us:
Pin Share