Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetoa tishio la kukifuta Chama cha ACT-Wazalendo.

Sababu kadhaa zimetolewa, zikiwamo za madai kwamba chama hicho kinatumia udini na kinaharibu kadi na mali za chama kingine – CUF.

Tunaandika haya kwa unyenyekevu mkubwa tukitambua kuwa dola na vyombo vyake vina dhima ya kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa tulivu na salama.

Kwa kulitambua hilo, tunapinga aina zozote za ubaguzi au uvunjifu wa amani katika taifa letu. Huu umekuwa ndio msimamo wetu kwa miaka yote.

Pamoja na hiyo ‘nia nzuri’ ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hatuna budi kutoa hadhari mapema kabla mambo hayajaenda mrama.

Bahati mbaya, tunachokiona sasa ni kile tunachoweza kusema ni “double standard” katika baadhi ya mambo na hatua zinazochukuliwa na vyombo vya mamlaka katika nchi yetu.

Kama kweli Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imedhamiria kuzuia hayo inayoyatumia kutishia kuifuta ACT-Wazalendo, basi isisite kutoa onyo kwa vyama vyote vinavyoshiriki hayo mambo.

Kwa mfano, si jambo la kificho kuwa kadi na bendera za vyama vyote vya siasa zimekuwa zikichomwa na upande wa chama au vyama vinavyosigana kimtazamo. Haya mambo si ya kificho. Upo ushahidi wa picha na wa maandishi unaoonyesha haya mambo yakifanywa na pande zote. Kama hivyo ndivyo, basi litakuwa jambo la msingi sana kumsikia Msajili wa Vyama vya Siasa akikemea kote kote, badala ya kuwaandama ACT –Wazalendo pekee. Sheria inakuwa nzuri pale inapong’ata kote kote bila kujali umaarufu, ukubwa au udogo wa chama.

Bila kufanya hivyo wananchi wataona Msajili wa Vyama vya Siasa ana nia mbaya na baadhi ya vyama.

Pia itambulike kuwa dhima mojawapo ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni malezi ya hivi vyama ili viweze kukua na kuimarika kidemokrasia. Kamwe, kazi ya ofisi hii isiwe kufuta vyama.

Ni vizuri tukakubaliana kuwa vyama ni majina tu, bali uanachama wa kweli umo ndani ya mioyo ya watu. Msajili anaweza kufuta vyama kila uchao, akavimaliza vyote, lakini kamwe hawezi kufuta kiu ya watu wanaoona kuwa na mawazo au misimamo mbadala kwa mujibu wa Katiba ya nchi ni haki na wajibu wao.

Tunaomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iwe mlezi wa kweli wa vyama vya siasa, badala ya kuwa mchinjaji wa hivyo vyama. Tunaunga mkono juhudi zote za kukabiliana na mambo yanayohatarisha amani ya nchi, lakini kwa hili la kufuta vyama vya siasa hatuoni kama lina manufaa kwa nchi na wananchi wa Tanzania.

7636 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!