Katika siku za karibuni uwanja wa siasa nchini umeshuhudia matukio makubwa. Ni matukio yenye kuzua mjadala na kimsingi, unaweza kusema ni matukio ambayo kwa sehemu kubwa yamevuruga mikakati ya vyama vya siasa kwa ujumla wake, mikakati kati ya chama kimoja dhidi ya kingine na hata mikakati kati ya mwanasiasa mmoja hadi mwingine.

Matukio haya yanahusu baadhi ya wanasiasa wenye majina makubwa kuhama vyama walivyokuwa wakivitumikia kwa njia ya uanachama na uongozi na kwenda kwenye vyama vingine. Tumeshuhudia aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, akifanya uamuzi mgumu wa kukihama chama hicho na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambako kwa tafsiri yake mwenyewe, uamuzi wake huo ni wa “kurejea nyumbani.”

Lakini mbali na Lowassa ambaye ni kama vile alifungua dirisha la hamahama ya viongozi wakuu, uwanja wa siasa tena hapa nchini ukashuhudia Katibu Mkuu wa muda mrefu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, naye akikihama chama hicho alichokitumikia tangu kuanzishwa kwake, akiwa mmoja wa waasisi, akijiengua na kujiunga na Chama cha ACT – Wazalendo.

Wanasiasa hawa wawili wakubwa wameibua mjadala ambao si haba katika duru za kisiasa nchini, kila mmoja ameondoka na baadhi ya wafuasi wake huko alikokuwa. Hii ni hali ambayo imefuatiwa na ile iliyoshuhudiwa mwaka jana pale baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani walipokuwa wakitangaza kujivua ubunge na uanachama wa vyama vyao kisha kujiunga na chama tawala, CCM, kwa tafsiri kuwa hatua hiyo ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli katika kuliongoza taifa.

Kwa upande wetu, JAMHURI, tunaamini matukio yote haya ni changamoto katika duru za kisiasa nchini. Ni changamoto zinazohitaji maarifa ya wanasiasa mmoja mmoja, sambamba na vyama vyao ili kila mmoja anufaike kwa upande wake. Hata hivyo, wakati kila mwanasiasa au chama cha siasa kikilenga kujinufaisha na mabadiliko hayo, tunashauri wakati wote kutangulizwa kwa masilahi ya taifa.

Please follow and like us:
Pin Share