KIGOMA

Na Mwandishi Wetu

Kigoma kuna nini? Hii ni kaulimbiu yenye swali iliyotumika miaka ya 1980 wakati sherehe za Sabasaba zilipofanyika kitaifa mkoani Kigoma.

Safari hii imejirudia lakini kwa aina tofauti na sasa ni mashabiki wa Yanga ndio wanaojiuliza Kigoma kuna nini baada ya timu yao kukubali kipigo cha bao 1-0 mbele ya watani wao wa jadi, Simba, katika fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) iliyopigwa kwenye dimba la Lake Tanganyika.

Ilikuwa ni wiki ya aina yake kwa mji wa Kigoma ambapo wenyeji wanadai tangu kufanyika kwa sherehe za Sabasaba, mji huo haujawahi kuchangamka kama ilivyokuwa wiki iliyopita.

Mamia kwa maelfu ya wageni kutoka mikoa mbalimbali walimiminika Kigoma; huku kukiwa na picha za wageni kutoka Burundi wakiwa safarini kwenda kushuhudia mpambano huo.

Bao la dakika ya 80 lililowekwa kimiani kwa kichwa na kiungo wa kimataifa kutoka Uganda, Mhandisi Thadeo Lwanga, ndilo lililozima shamrashamra za mashabiki wa Yanga waliotamba kuifunga Simba kwa mara ya tatu ndani ya mwaka huu wa 2021.

Awali, Yanga waliifunga Simba katika fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyochezwa Januari mwaka huu mjini Zanzibar, kisha wakashinda tena kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara wiki tatu zilizopita.

Michezo hiyo ya awali ilichezwa mashariki kabisa mwa Tanzania na huu wa juzi ukapigwa magharibi mwa Tanzania, ikiwa ni mara ya kwanza watani wa jadi kukipiga mkoani humo.

Na kwa ushindi huo, Simba wamefanikiwa kutetea ubingwa wao walioutwaa mwaka jana kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga walikocheza na Namungo.

Ni Lwanga aliyepachika bao hilo pekee na la ushindi lililopeleka kilio Jangwani na furaha ya aina yake Msimbazi.

Lilikuwa ni pigo la kichwa, akitumia mpira wa kona iliyochongwa kiufundi na Luis Miquissone, ambaye Jumamosi ya Julai 25 ilikuwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake.

Katika mchezo huo uliodhaniwa kwenda muda wa nyongeza, Yanga walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa pungufu baada ya mchezaji wao, Mukoko Tonombe, kuonyeshwa kadi nyekundu.

Tonombe, raia wa Congo, alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumpiga kiwiko cha mkono kwa makusudi nahodha wa Simba, John Bocco, katika dakika ya 43.

Kutolewa kwa Tonombe kulitumiwa vema na Simba kwa kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha pili cha mchezo huo.

Simba wanatangazwa kuwa mabingwa wa Kombe la Shirikisho mbele ya watani wao wa jadi katika mji maarufu kama ‘mwisho wa reli’.

Ushindi wa Simba umepokewa kwa shangwe kubwa katika kila kona ya nchi, lakini hasa mjini Kigoma, ambako rangi nyekundu na nyeupe zimetawala.

Taji hili la ASFC ni la pili mfululizo kwa Simba, lakini ni la tatu kwa msimu huu baada ya kubeba Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimnu, na majuzi ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Kabla ya mechi hiyo, tambo za mashabiki zilikuwa nyingi huku Yanga wakijiamini zaidi, hasa kutokana na msuguano ulioibuka kwenye Klabu ya Simba kati ya Mtendaji Mkuu, Badra Gonzalez na Msemaji wa Simba, Haji Manara.

Hata hivyo, mshikamano wa hali ya juu miongoni mwa viongozi wengine na wachezaji wao umeifanya Simba kwenda Kigoma wakiwa na morali kubwa, na kisha kushinda mechi hiyo.

Wakati timu zinakwenda mapumzikoni kujiandaa kwa msimu ujao wa Ligi Kuu, miamba hiyo ya soka Afrika Mashariki itapambana tena katika mechi ya ufunguzi wa ligi; Ngao ya Jamii, kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

By Jamhuri