Uchaguzi wa madiwani uliofanyika mjini Arusha katikati ya mwezi huu, una haki ya kuwa fundisho kwa chama tawala CCM.

Fundisho la kwanza kabisa kwa CCM ni kwamba  kisijiamini mno. Sielewi kama CCM iko tayari kujifunza hilo. Na asiyejifunza hana alijualo na huishia  kwenye kuharibikiwa. Na CCM  ikiendelea na moyo huo wa kutotaka kujifunza basi ijiandae kuharibikiwa zaidi mwaka 2015.

 

Tukizungumzia uchaguzi wa madiwani uliofanyika Arusha ambao Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeshinda kwa kishindo, si vibaya tukikumbushana kuwa uchaguzi wa kwanza wa madiwani nchini Tanganyika (Tanzania Bara) ulifanyika Arusha Januari 1958. Katika uchaguzi huo, TANU ilishinda kwa kishindo wakati iliposhindana na chama cha Wazungu cha United Tanganyika Party (UTP).

 

Sasa kwa upande wa uchaguzi wa madiwani uliofanyika Arusha mwezi huu, ni mambo yapi mengine yalichangia kuanguka kwa CCM mbali na ukweli kwamba Arusha ni ngome ya Chadema na kwamba CCM haitaki kujifunza kitu?

 

Nitayataja mambo manne yaliyosababisha CCM kuanguka Arusha  na  yanayoweza kusababisha kuanguka kwa CCM mwaka 2015 kama haitataka kujitazama upya.

 

La kwanza ni makundi ndani ya CCM. Ni makundi yale yenye nia ya kuwania urais mwaka 2015. Ni makundi yaliyosababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya CCM. Kwa hivyo, unakuta CCM inakwenda vitani (kwenye uchaguzi) tayari watu wake wakiwa vitani wenyewe kwa wenyewe.  Katika mazingira hayo ni rahisi watu wa kundi moja kumsaidia adui wakihisi kwamba mtu wa kundi jingine atashinda uchaguzi huo.

 

Si sahihi kila mtu aliyemo ndani ya CCM  kujiaminisha kwamba akigombea  urais atashinda. Kinachotakiwa ni unyenyekevu utakaomfanya mtu atambue kwamba yeye si bora zaidi kuliko mtu mwingine. Utendaji wa sasa wa mtu katika nafasi yake ndiyo utakaosaidia wananchi kuamua kumpa au kumnyima kura.

 

Tatizo jingine la CCM ni kwamba wabunge na madiwani wake wako mbali sana na wananchi, ambapo wabunge na madiwani wa Chadema wapo karibu zaidi na wananchi.

 

Inasemekana kwamba ni rahisi sana kumwona mbunge au diwani wa Chadema kuliko kumwona mbunge au diwani wa CCM. Imeendelea kudaiwa kuwa wabunge na madiwani wa CCM wametawaliwa mno na ubinafsi. Hawana tabia ya kusaidia watu. Matokeo yake wananchi wanaambatana au wanashikamana na Chadema.

 

Ni katika mazingira hayo ile Nguvu ya Umma (People’s Power) inayohubiriwa na Chadema inafanya kazi. Ndiyo iliyofanya kazi Arusha.

 

Jambo la Tatu lililosababisha Chadema kushinda uchaguzi wa Arusha, hapana shaka ni uhasama mkubwa ulioota mizizi Arusha kati ya Chadema na Polisi.

 

Kama tujuavyo, watu wengi hawapendi Serikali polisi ikiwa sehemu yake. Kwa hiyo, polisi wanapopambana na vyama vya upinzani wananchi wa kawaida huwa upande wa wapinzani.

 

Kwa hivyo, ni muhimu sana polisi na Serikali vichukue tahadhari katika kupambana na vyama vya upinzani na wananchi kwa jumla. Na tahadhari hiyo isichukuliwe Arusha tu, ichukuliwe pia Mtwara ambako kila mtu anajua kuwa ukifanyika leo uchaguzi wa ubunge viti vyote vitachukuliwa na wapinzani.

 

Hofu ya kutokea vurugu katika uchaguzi wa Arusha ilichangia pia kushindwa kwa CCM.  Tumesikia kuwa ni wananchi wachache sana waliojitokeza kupiga kura Arusha. Na hapana shaka wengi miongoni mwao walikuwa wanawake.  Si siri wanaosababisha Chadema kushinda ni vijana kwa upande mwingine wanaosababisha CCM kushinda uchaguzi ni wanawake.

 

Vijana walikwenda kwa wingi vituo vya kupigia kura kuchagua Chadema. Wanawake wengi walibaki majumbani, hawakwenda kuchagua CCM. Matokeo yake Chadema imeshinda.

 

Katika mazingira hayo, Serikali ya CCM isipochukua hatua sasa ya kuhakikisha amani inatawala wakati wote wa kampeni za uchaguzi, CCM inaweza kujikuta mwaka 2015 ikishindwa uchaguzi kwa kishindo. Tusubiri tuone.

1350 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!