Kiongozi wa upinzani nchini Bahrain, Sheikh Ali Salman, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya mahakama ya rufaa kumkuta na hatia ya kuipeleleza nchi hiyo kwa niaba ya nchi ya Qatar.

Hukumu hiyo inakuja miezi michache baada ya mahakama ya juu nchini Bahrain kumuondolea mashtaka Salman kwa kushirikiana na taifa hasimu.

Nchi ya Bahrain ilisitisha uhusiano wake na nchi ya Qatar mwaka 2017.

Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty limesema kwamba uamuzi huo wa mahakama ni moja ya ukiukaji wa haki za binadamu katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo inaendelea kupambana na wakosoaji.

Serikali ya Bahrain inaendelea kuzuia kwa nguvu ukosoaji unaofanywa na wapinzani wa nchi hiyo.

Ali Salman aliongoza vuguvugu ambalo sasa limepigwa marufuku la Al-Wefaq. Anashutumiwa kwa kushirikiana na nchi ya Qatar kuendesha vurugu dhidi ya serikali mwaka 2011 pamoja na viongozi wenzake wa upinzani ambao ni Hassan Sultan na Ali al-Aswad.

Hassan Sultan na Ali al – Aswad bado hawajahukumiwa, ingawa wamo katika mikono ya sheria ya nchi hiyo.

Mwendesha mashtaka nchini Bahrain amesema kuwa washirika hao watatu waliwekwa kizuizini kwa kile kilichodaiwa kuwa na mawasiliano na maofisa wa Qatar ili kuipindua serikali.

Njama hizo ambazo zinaelezwa kufanywa miaka saba iliyopita (2011), zimeibuliwa mwaka jana (2017) baada ya nchi za Bahrain, Saudi Arabia, UAE na Misri kukata uhusiano na nchi ya Qatar.

Washirika hao waliilaumu Qatar kwa kuunga mkono makundi ya kigaidi na kuwa karibu sana na Iran, madai ambayo Qatar inayakana.

Kilichotokea mwaka 2011

Waandamanaji wakiongozwa na jamii kubwa ya Shia waliingia barabarani Februari 2011 wakidai kuwepo kwa demokrasia nchini humo.

Familia ya kifalme ya Al Khlifa inayoshikilia nafasi nyingi za kisiasa na kijeshi ilizima maandamano hayo kwa msaada wa nchi jirani, hasa Saudi Arabia.

Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 30, wakiwamo askari watano.

Tangu mwaka 2011, Bahrain imekumbwa na misukosuko ya kisiasa, hivyo kusababisha serikali kupiga marufuku vikundi vya upinzani huku mamia ya wakosoaji wa serikali wakiishia gerezani.

Makala hii imeandikwa kwa msaada wa mitandao.

By Jamhuri