ChristopherMtikilaOktoba 4, mwaka huu, saa mbili asubuhi nikiwa nyumbani nilipigiwa simu. Nilipopokea simu ile iliyonifahamisha kuhusu kifo cha Mchungaji Mtikila, nilidhani kuwa ni utani kutoka na mtoa taarifa na jinsi alivyowasilisha msiba huo. 

Kutokana na jinsi tulivyozeana na uwasilishwaji wake wa kifo hicho, sikukubaliana naye. Lakini kutokana na msisitizo wake ilinilazimu kuhakiki taarifa hizo kutoka mkoani Pwani, ambako nilithibitishiwa kuwa ni kweli.

Mchungaji Mtikila, mtetezi wa haki za binadamu, mpambanaji aliyekufa huku akiidai Tanganyika aliyoiamini, hayupo tena nasi. Kamanda huyo wa vita mwenye jeshi la mtu mmoja, aliamini kuwa ushindi ni lazima bila kukubali kukatishwa tamaa.

Mtikila amekufa bila kutimiza lengo lake la harakati za ukombozi wa Tanganyika na lengo la kuwapo kwa mgombea binafsi katika chaguzi mbalimbali nchini. Hakika, tumempoteza mwanaharakati wa kweli aliyepigania uhuru wa kutoa mawazo ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo katika maandamano nchini.

Alitoa mchango mkubwa katika harakati za kisiasa zilizozaa matunda ya kuondoa woga kwa baadhi ya wanasiasa wetu, na kusimamia kile wanachokiamini hatimaye ufumbuzi kupatikana.

Namlilia Mchungaji Mtikila, rafiki asiye na unafiki kama walivyo marafiki wengi, rafiki aliye tayari kuusema ukweli hata kama unauma. Mchungaji Mtikila alikuwa miongoni mwa watu wachache waliovuka mipaka ya nchi ili kuweza kuhakikisha haki inapatikana hasa kwa kutumia Mahakama.

Katika moja ya kauli zake alisisitiza kuwa Mahakama ni rafiki yake, hivyo hawezi kuogopa kwenda mahakamani hata kama atatengwa na kupuuzwa na kila mmoja wetu. Mtikila hakuwa muoga, alikuwa ni jasiri sana na binafsi sitarajii Taifa kupata Mtanzania, mwanasiasa aina ya Mtikila kwa kizazi hiki labda pengine baada ya miaka 50 ijayo.

Kwa sababu wanasiasa wengi nchini wamekuwa waoga, wasio na uthubutu wa kufanya jambo, na wakati mwingine kuishi maisha ya kuvikimbia vyombo vya dola. Mtikila alikuwa tofauti.

Hakuogopa Polisi, Mahakama na dola kwa ujumla, mtu yeyote awe rais, yeye alikuwa akiamua kuanzisha jambo alikuwa akilipigania hadi mwisho na hata kama kulikuwa na watu waliokuwa wakimuunga mkono mwanzo wakati analianzisha jambo hilo, iwapo wakimsaliti alikuwa akisonga mbele bila kujali usaliti huo.

Tutamkumbuka Mtikila, mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambako alionesha msimamo wake katika kumtetea Mtanzania na kudai Katiba ya wananchi.

Pamoja na kuwa mmoja wa wanaharakati, mpambanaji na aliyepigania kufutwa kwa Sheria namba 12 iliyokuwa akizuia maandamano, na iliyowataka waandamanaji kupata kwanza kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya, ingawa kwa siku za hivi karibuni hakuwa muumini wa maandamano.

Aliamini kuwa haki inapatikana mahakamani siyo barabarani kama wengi wetu tulivyozoea kuona na kusikia. Msimamo huu ulimfanya kuonekana kuwa ni mtu mkorofi, jambo ambalo lilikuwa halimtishi kutodai haki hiyo.

Pamoja na kwamba Mchungaji Mtikila ameshatangulia mbele ya haki, lakini hakuwa akiamini katika kifo. Aliamini kuwa ameumbwa kuishi na siyo kufa. Daima ataendelea kuishi katika mioyo na akili za wale waliomwamini na kumuelewa.

Pamoja na kujiandikia historia ya kuwa na kesi nyingi, katika kesi zake nyingine alikuwa akijitetea mwenyewe bila kuweka wakili wa kumtetea na aliweza kushinda kesi hizo. Mtikila ulikuwa akifanya mawasiliano na wale anaoamini kuwa wanamuelewa amelala, amelala usingizi wa kifo.

Inauma kuwapoteza wapendwa wetu, inauma zaidi kumpoteza mpambanaji aliyekuwa tayari kusimama kwa ajili ya nchi yake na watu wake bila uoga. Yapo mambo mengi na makubwa niliyoweza kujifunza kutokana na mapambano yake, alinifundisha kujiamini na kutetea ninachokiamini bila kujali kuwa naweza kupachikwa jina la mkorofi.

Nitasimama kidete kuhakikisha kuwa sionewi kama ambavyo aliniasa, kupambana kuhakikisha natetea pale ninapoona pana uonevu. Taifa limepoteza Mtanganyika halisi, Mtanganyika aliyekuwa tayari kusimama na kuitetea Tanganyika bila haya.

Nenda kamanda, nenda rafiki yangu, nenda mtetezi wa wanyonge na mpiganaji wa kweli. Mungu aiweke roho ya Mtikila mahali palipo stahiki kwake kamanda wa jeshi la mtu mmoja.

By Jamhuri