Na Angalieni Mpendu

Amani ni neno fupi na jepesi kutamkwa na mtu yeyote – awe mstaarabu au mshenzi. Maana ya neno hili ni ndefu kiwango cha upeo wa macho ya mtu kuona na kutafakari. Na nzito mithili ya nanga au jiwe. Amani ina thamani kupita feruzi, yakuti au almasi.

Amani ukiimithilisha ni chakula ni mkate wa divai ukiutia kinywani huyeyuka haraka na kuleta baraka kwa mlaji. Amani kama tiba ni chungu mithili ya shubiri au kwinini tiba ya ugojwa. Kama ni pambo mwilini basi ni kito cha lulu ing’aayo kumpendeza mvaaji na mwangaliaji.

Mtu huru, mstaarabu na mwadilifu ndiye mtambuzi wa maana na thamani ya amani. Mtu mwenye sifa hizi kamwe haendi kinyume. Mtu ambaye hajastaarabika haoni na hajui thamani ya amani na huwa rahisi kuivunja kama avunjavyo yai la ndege.

Amani haiwekwi poni, haikodishwi na haiuzwi kama bidhaa sokoni. Haiendeshwi kwa upepo kama jahazi. Si rafiki wa ghasia au fujo au vita. Amani ni hali ya utulivu iliyojaa upendo wa asili ya nafsi sikivu na adilifu.

Tangu tupate Uhuru mwaka 1961 hadi mwaka jana, 2017 Watanzania tumeweza na kutia fora kutunza amani yetu mbele ya Afrika na duniani. Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuishika amani na nchi kuwa salama.

Bado nasisitiza kusema tuendelee kuilea na kuilinda tusipokonywe na hao wasiothamini amani tuliyonayo mikononi. Zipo dalili za kukinga kuona upeo wa amani unakuwa mfupi. Aidha, uzito wake kumomonyolewa kama ladu, kutokana na virusi vya gubu, kimondo, tafarani na kindumbwendumbwe.

Lisemwalo liko kama haliko li njiani laja. Ni methali kongwe inayotumika hata sasa kufumba na kufumbua jambo lililopo au lijalo. Tusiipuuze methali hii kwa sababu dalili za kuiyumbisha amani na kuitoa katika mhimili wake na kuiweka polepole kwenye fukuto la kisiasa, inaonekana.

Gubu linavuma masikioni na kukaririwa akilini, kutoka baadhi ya vyama vya siasa, taaluma ya sayansi ya siasa, viongozi wa taasisi za dini, watetezi wa demokrasia na wananchi wa makundi hayo. Kila kundi lina mtindo wake ijapokuwa mapigo yanazungumzia suala la haki za binadamu na demokrasia.

Maelezo yanayotolewa katika gubu hili ni mahitaji ya Katiba mpya na nchi, Serikali kuacha kuminya demokrasia yaani uhuru wa mawazo, hisia ya kuondoa mfumo wa vyama vingi vya siasa na dhana ya kupikwa kwa takwimu za Serikali na kusambazwa kwa wananchi. Vyote hivi ni virusi vinahitaji kinga na tiba.

Haya ni malumbano kati ya kundi la siasa na Serikali. Hadhari inahitajika sana. Mwaka 2018 umerithi malumbano haya pamoja na vikorombwezo vyake. Ni matarajio yangu tena kuomba mwaka huu unatupatia wananchi tiba na matibabu ya virusi na kuondoa gubu.

Tazama ramani, utaona nchi nzuri
Yenye mito na mabonde mengi ya nafaka
Nasema kwa kinywa halafu kwa kusitiri
Nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania.

Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote
Nchi yangu Tanzania, jina lako ni tamu sana
Nilalapo nakuota wewe, niamkapo ni heri mama wee
Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote.

Mungu ibariki Tanzania, dumisha uhuru na umoja
Wake kwa waume na watoto, Mungu ibariki
Tanzania na watu wake
Ibariki Tanzania, ibariki Tanzania
Tubariki Watoto wa Tanzania.

By Jamhuri