Lala Salama ya Ubunge kwa Chadema, CCM

Maulid Mtulia, Mgombea wa CCM, Jimbo la Kinondoni.
Salum Mwalimu, Mgombea wa Ubunge Kupitia Chadema Jimbo la Kinondoni
Rajabu Salum Juma, Mgombea Ubunge Jimbo Kinondoni kupitia CUF

Na Waandishi Wetu

Vyama vyenye ushindani mkubwa wa kisiasa nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vinaingia wiki ya mwisho kwa kampeni za uchaguzi mdogo katika majimbo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam  na Siha mkoani Kilimanjaro.

CCM imewasimamisha Dk Godwin Mollel (Siha) na Maulid Mtulia (Kinondoni) wakati wagombea wa Chadema wakiwa ni Elvis Mosi (Siha) na Salum Mwalimu (Kinondoni).

Pamoja na CCM na Chadema, vyama vingine vikiwamo Tanzania Labour Paty (TLP) na Chama cha Wananchi (CUF), upande wa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, vimesimamisha wagombea ambao hata hivyo hawapewi nafasi kubwa ya ushindi, kwa mujibu wa maoni ya wananchi.

JAMHURI imefanya mahojiano na wagombea ubunge kupitia vyama hivyo ambao licha ya kutegemea ushindi katika uchaguzi mdogo wa Februari 17, mwaka huu, wamezungumzia hoja tofauti, endelea…

Chadema yahofia wapiga kura wachache

NA WAANDISHI WETU

Takribani siku nne kabla ya kufanyika uchaguzi mdogo katika majimbo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro, hofu ya kujitokeza wapiga kura wachache imeibuka kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mgombea ubunge katika jimbo la Kinondoni (Chadema), Salum Mwalimu amesema hofu hiyo inatokana na matukio yaliyoibua dhana ya kuwapo wizi wa kura, hivyo baadhi ya watu kutokuwa tayari kujitokeza.

Mwalimu amesema hofu ya wananchi kutojitokeza kwa wingi kupiga kura ni jambo lenye umuhimu lililojadiliwa pia na Kamati Kuu ya chama hicho ili kupata namna bora ya kukabiliana nalo hususani wakati wa kampeni.

Amesema miongoni mwa uamuzi uliofikiwa kukabiliana na hofu hiyo ni kuuhamasiaha umma hususani wakazi wa Kinondoni na Siha ili wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi na kuhakikisha wanalinda kura zao.

Amesema Chadema kwa kushirikiana na vyama washirika wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), imejiandaa kushiriki uchaguzi huo kwa lengo la kupata ushindi.

“Tumejiandaa kuanzia majukwaani na kampeni za nyumba kwa nyumba ili kuwashawishi wapiga kura watupatie ushindi,” amesema.

Vipaumbele vyake

Mwalimu amesema akichaguliwa kuwa Mbunge wa Kinondoni, atawekeza katika kipaumbele cha kuboresha mazingira ya uchumi mdogo kwa wananchi wa jimbo hilo.

Amesema vijana wengi wa Kinondoni jimboni humo wanajihusisha na biashara ndogo-ndogo ili kupata fedha za kujikimu kimaisha.

Mwalimu amesema kwa kushirikiana na wachumi waliopo ndani na nje ya Chadema,  atahakikisha vijana na wanawake wanajiunga ama kuimarisha vikundi vya ujasiriamali ili kupata mikopo itakayokuza mitaji yao.

Kwa mujibu wa Mwalimu, hatua hiyo itajumuisha urasimishaji wa biashara ili kuviwesha vikundi hivyo kukopesheka.

Eneo jingine la kipaumbele kwa Mwalimu ni uboreshaji wa makazi ya watu wakiwamo wanaoishi kuzunguka mto wa Ng’ombe.

Mwalimu amesema uboreshaji wa huduma za afya na kuchagiza kasi ya kuwezesha kila kata ya jimbo hilo kuwa na kituo cha afya kwa mujibu wa sera ya taifa ya afya, ni miongoni mwa mambo ya msingi kuyashughulikiwa ikiwa atashinda ubunge.

Haki ya kugombea

Amesema hoja inayoenezwa na washindani wake kwamba hafai kuchaguliwa kwa vcile si mkazi wa jimboni humo haina mashiko.

Amesema ni mkazi wa Kinondoni aliyezaliwa katika eneo la  Morocco alipokuwa akiishi na wazazi wake.

Mwalimu anasema wanaoeneza propaganda kwamba ni Mzanzibari asiyekuwa na haki ya kuchaguliwa wanapaswa kupuuzwa kwa vile licha ya kuwa ni mzaliwa wa jimboni humo, lakini ana haki zinazopingana na ubaguzi unaojidhihirisha kwa washidani wake wa kisiasa.

Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 67 (1), mtu atastahili kuchaguliwa kuwa Mbunge iwapo ana sifa za kuwa raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 21 au zaidi.

Mwalimu amesema sifa nyingine ni awe anajua  kusoma na kuandika kwa Kiswahili na Kiingereza, mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa chenye usajili kamili.

Pia anasema sifa nyingine ni hajawahi kutiwa hatiani na  mahakama kwa kosa la kukwepa kulipa kodi katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.

“Sifa zote hizo ninazo, ninachowaomba wapiga kura wa Kinondoni ni kuniamini ili niwe mtumishi na mwakilishi wao,” amesema Mwalimu.

Uzoefu katika siasa

Amesema uzoefu alioupata ndani ya Chadema hadi kufikia kuwa Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) mwaka 2014 hadi sasa, unatosha kutekeleza majukumu ya kibunge.

CUF yaonya wizi wa kura

Mgombea ubunge wa Kinondoni kupitia Chama Cha Wananchi  (CUF), Rajab Juma amesema mikakati inayopangwa kufanikisha wizi wa kura, haitafanikiwa kwa vile wamejipanga kuidhibiti kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa huo.

Akizungumza kupitia kwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF (anayeumuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba), Abdul Kambaya amesema, wamejidhatiti kudhibiti wizi wa kura na kwamba chama kinachotarajiwa kutangazwa ‘ushindi wa bao na mkono’ hakitafanikiwa.

Amesema mgombea wa CUF anafaa kuchaguliwa kwa vile anafuata imani na  itikadi ya chama hicho inayojikita katika kusimamia rasilimali za umma.

“Hii ni  tofauti na Mbunge aliyetangulia ambaye hakutaka hata kutumia ofisi yake na kuamua kupanga chumba sehemu nyingine,” amesema.

Bomoa bomoa

Amesema Juma akishinda nafasi hiyo atasimamia sheria na haki za watu ikiwamo ubomoaji holela wa nyumba za watu jimboni humo.

Amesema Mbunge aliyetangulia, kujiuzulu kisha kuteuliwa na CCM kuwania kiti hicho, Mtulia aliwatetea wananchi wanaobomolewa makazi yao hususani katika kata ya Kinondoni inayoongoza kwa makazi hatarishi, lakini hawezi kufanya hivyo akiwa ndani ya CCM.

Elimu na afya

Amesema elimu ni kipaumbele cha  mgombea wa CUF ili kujenga mazingira mazuri kwa watoto na wananchi wengine kupata elimu bora.

Amesema watahakikisha kuwa kila mwanafunzi katika shule za jimboni humo, anapata walau mlo mmoja kwa siku.

Kambaya amesema kama Mwalimu Julius Nyerere aliweza kufanya hilo huku wanafunzi wakipewa vitabu na madaftari bure, mgombea wao hawezi kushindwa kufanikisha azma ya kupatikana kwa mlo mmoja kwa siku kwa wanafunzi jimboni humo.

Amesema fedha zitakazotumika kuboresha elimu ni zile za mfuko wa jimbo. Pia ametaja kipaumbele kingine kuwa ni uboreshaji wa sekta ya afya.

Mwisho