Lissu ameumizwa, lisitokee tena Tanzania

Na Deodatus Balile

Leo nimeona niandike mada inayohusiana
na hali ya usalama, amani, utulivu na
upendo kwa taifa letu. Nimesoma maandishi
ya Mbunge wa Singida Mashariki
(CHADEMA), Tundu Lissu, wakati anatimiza
mwaka mmoja wa maumivu tangu
alipopigwa risasi Septemba 7, 2017 jijini
Dodoma.
Si nia yangu kurejea aliyoyasema Lissu, ila
kwa picha ya video niliyoiona, inayoonyesha
kuwa mfupa wake wa nyuma ya goti
umechanwa na risasi alizopigwa na
kuachana kwa inchi 7, sawa na sentimita
70, hivyo anapaswa kuuguza kwa siku 70
akitumia spana kufunga vyuma vya
kuurejesha kila baada ya saa 8. Hakika
Lissu amepitia mateso makali.
Sitanii, yapo mambo ameyazungumza Lissu
ndiyo yamenisukuma kuandika makala hii.
La kwanza, ni mfumo wa vyama vingi.
Napata tabu kuelewa kama Watanzania

tunafahamu maana ya mfumo wa vyama
vingi. Nguvu ninayoona inatumiwa na
vyama vya siasa kuanzisha vikundi vya
ulinzi vya Green Guard, Red Brigade na
Blue Guard inanithibitishia hilo.
Mara kadhaa nawasikiliza viongozi wa
chama tawala na wa vyama vya upinzani,
naona kuna upungufu wa uelewa. Mfumo
wa vyama vingi uliletwa si kwa nia ya kuleta
uadui. Mfumo huu uliletwa kwa nia ya
kuwapa wananchi fursa ya kutoa mawazo
mbadala kwa chama kinachoongoza, lakini
kwa bahati mbaya naona vyama vingi
vinaanza kufumua mkeka wa umoja wetu.
Sitanii, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga
umoja, upendo na mshikamano kwa taifa
hili. Ilifika mahala kila mtu akawa anamwita
mwenzake NDUGU. Mataifa jirani yakawa
yanatushangaa kuona hata wabunge
tunawaita ndugu. Ila ni bahati mbaya miaka
ya karibuni, viongozi wetu wamevua undugu
na kuwa waheshimiwa.
Nikiangalia ndani ya vyama naona kuna
tabu. Vyama vya upinzani wanafukuzana
kama digidigi. Chama tawala wanaminyana
kama mbu kwenye chandarua. Ukifika
uchaguzi kanuni ya wateule inakuwa

mikononi mwa mwenyekiti. Wengine
wanabadili gia angani. Hali hii imegeuza
lengo la msingi alilolifikiria Mwalimu Nyerere
wakati anajenga hoja ya kurejesha mfumo
wa vyama vingi.
Nyerere alisema wengi wape na wachache
wasikilizwe. Nasoma mijadala kwenye
mitandao ya kijamii kama Jamii Forums.
Nikiona michango ya watu wenye kuwaza
milengo tofauti ya kisiasa, napata hofu
kubwa. Kuna watu wanashangilia Lissu
kupigwa risasi hizo 16, na ukipima hoja zao
wala si za kuisaidia serikali iliyoko
madarakani, bali ni za kujipendekeza ili
wapate vyeo. Wengi ni wachumia tumbo!
Sitanii, la pili, Lissu amezungumzia suala la
uchunguzi dhidi ya waliomuumiza. Mimi ni
mwanasheria kitaaluma pia. Naangalia
sheria mbalimbali ikiwamo ya Jeshi la Polisi,
Kanuni ya Adhabu na Mwenendo wa
Mashtaka, sheria hizi zote zinataka
linapokuwapo tukio kama la Lissu kupigwa
risasi uchunguzi ufanyike.
Kitendo cha uchunguzi wa tukio la Lissu
kuendelea bila ukomo, huku yeye mara
kadhaa akisema hajahojiwa na wala dereva
wake hajahojiwa, huku ikiwa hakuna
aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo au

Jeshi la Polisi kusema bayana kuwa
limeshindwa likaomba msaada wa kimataifa
suala kama hili lichunguzwe, inaweka
kiwingu.
Mbele ya macho ya jamii inayolalamika
kwenye mitandao na washuhudiaji
wasiosema lolote, wanaweza kufika mahala
wakaamini kuwa polisi wanawafahamu
wahusika ndiyo maana hawatoi taarifa
yoyote. Kila mara sisi waandishi tukimuuliza
IGP Simon Sirro anasema atafurahi
kupatiwa taarifa za siri juu ya nani
aliyehusika na shambulio hilo.
Sitanii, suala la tatu ni hili la Bunge kukataa
kumlipia matibabu Lissu hata baada ya
familia kudai kuwa ilikuwa tayari kuandika
barua kama ilivyoelekezwa. Hoja kwamba
hakupitia Muhimbili kabla ya kwenda nje ya
nchi kwa matibabu, ni hoja dhaifu mno.
Tunapaswa kujiangalia na kuliweka mbele
taifa letu, badala ya siasa za vyama kama
nilivyotangulia kusema.
Mwisho, naamini sisi sote tuna moyo wa
nyama. Bila kujali itikadi za vyama,
tunakubaliana kuwa Lissu aliumizwa mno.
Naamini wakati umefika mambo mawili
yafanyike kama nchi. Moja, uchunguzi
ukamilishwe na waliohusika wafikishwe

mahakamani, maana tukiwaacha hawa, ipo
siku watapata hamu ya kututenda hata sisi
tunaowafunga.
Suala jingine katika kuhitimisha, nadhani
Bunge chini ya Spika Job Ndugai, ambaye
nikizungumza kuhusu suala la matibabu
naamini ananielewa vizuri kuliko mbunge
yeyote, anapaswa kupiga moyo konde,
aagize Lissu alipiwe matibabu, kwani sina
uhakika kama ubishi kwamba hakupitia
Hospitali ya Taifa Muhimbili iwapo
unaandika historia nzuri kwa taifa letu.
Tumgeukie Mungu. Ni bora tuamini kuwa
Mungu yupo, twende tusimkute, kuliko
kusema hayupo, tukafika tukakuta
anapokea wageni. Mungu Ibariki Tanzania.

Mwisho