NA ANGELA KIWIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. John Magufuli,
amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Anthony Mtaka, kwa kuchapa kazi
kimyakimya na kuleta maendeleo makubwa
katika mkoa wake.
Rais Magufuli amebainisha kwamba Mtaka
ndiye kinara katika wateule wake wa ngazi
ya mikoa nchini.
Amesema kuwa Mtaka ndiye mkuu wa
mkoa anayeongoza kwa kufanya kazi vizuri
kuliko wote, hii ni kutokana na ripoti
iliyomfikia.
Rais ameyasema hayo wakati akiendelea
na ziara anayoifanya katika mikoa ya Kanda
ya Ziwa.
Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake

mpeni. Mtaka ni miongoni mwa vijana
waliopata fursa ya kuteuliwa huku akiwa na
fikra chanya, asiye na majivuno kama
ambavyo tumeshuhudia kwa baadhi ya
vijana nchini.
Hivi karibuni alisikika akiwatahadharisha
viongozi wanaofanya kazi katika Mkoa wa
Simiyu kutimiza wajibu wao ipasavyo na
kutoonyesha ubabe.
Alitoa angalizo/onyo kwa wakuu wa wilaya
katika Mkoa wa Simiyu kutothubutu
kuwatisha watendaji wa mkoa huo, ikiwa ni
pamoja na kuwaweka ndani kama ambavyo
wakuu wengine wa wilaya nchini
wanavyofanya.
Huyu ndiye Anthony Mtaka, anayesifiwa na
rais.
Mtaka kwa kushirikiana na viongozi wa
mkoa ameunda mkakati wa kuboresha
elimu na kuinua kiwango cha ufaulu mkoani
Simiyu.
Amefanikiwa katika hili, na Simiyu ni moja
ya mikoa inayofanya vizuri katika matokeo
ya mitihani kitaifa.

Tanzania inahitaji kuwa na viongozi aina ya
Mtaka, viongozi wasiojikweza na kujitwika
ubabe na ukatili huku wakishindwa kutimiza
wajibu wao.
Wateule wa rais ni vema wakatambua kuwa
cheo ni dhamana, hivyo ni jukumu lao
kutimiza wajibu wao na kumsaidia rais
katika kutatua kero, kusimamia sheria na
kuwa wasimamizi wazuri wa rasilimali za
nchi.
Tumeshuhudia jinsi vijana wengi wateule
wa rais wanavyotumia madaraka yao vibaya
na kusababisha chuki kwa raia dhidi ya
serikali yao.
Ikumbukwe kuwa wateule wa rais wapo kwa
ajili ya kumsaidia rais kutimiza ahadi na
majukumu ya kila siku, si kutengeneza
chuki kwa raia wanaowaongoza.
Watanzania tunasifika kwa kuwa wapole na
wapenda amani, hivyo ni jukumu la wateule
hawa hasa wakuu wa wilaya na mikoa
kutambua wajibu wao na kukumbuka kuwa
amani na utulivu katika maeneo yao ni
jukumu lao.

Si sifa hata kidogo kwa kiongozi wa serikali
kuwa kinara wa vitisho na kejeli kwa baadhi
ya watumishi wa serikali na wasaidizi wake.
Tanzania ni nchi yetu inayotuhitaji kuijenga
kwa pamoja bila vitisho kama afanyavyo
Mtaka, kijana mwenye maono na mtizamo
chanya kiuongozi.
Rais anahitaji wasaidizi wenye weledi,
wabunifu na wasio tayari kumjengea chuki
na wananchi wake katika kusukuma
gurudumu la maendeleo.
Mtaka ni kiongozi wa mfano miongoni mwa
viongozi wanaohitajika katika nchi yetu kwa
maendeleo ya sasa na baadaye.
Tunahitaji wasaidizi wa rais watakaokuwa
wabunifu, wasio na majivuno na wenye
utayari wa kuonyesha vipawa vyao katika
kuongoza jamii inayowazunguka.
Nachukua fursa hii kumshukuru rais kwa
kutambua na kuthibitisha kipawa
alichonacho Mtaka.
Mungu Ibariki Tanzania.

Mwisho

1465 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons