Na Helena Magabe,
Tarime

Wanawake wanaofanya kazi katika
mgodi wa dhahabu wa Kebaga uliopo Kata
ya Kenyamanyori, Tarime, Mkoa wa Mara,
wamemlalamikia diwani wa kata hiyo kwa
kuwanyanyasa vijana pamoja na
wachimbaji wadogo.
Diwani huyo aitwaye, Ganga Ganga,
anatuhumiwa kuwakamata watu hao kwa
kutumia ushawishi wa Jeshi la Polisi,
kuwatesa, pamoja na kuwazuia kuchimba
dhahabu kwa sababu zisizo za msingi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,

waathiriwa wa udhalimu huo wameliambia
Gazeti la JAMHURI kwamba wamechoka
kunyanyaswa na diwani huyo.
Mmoja wa kina mama, Pili Ngusa (60),
ambaye anafanya kazi ya kuosha mabaki
ya dhahabu katika mgodi huo, anasema
diwani huyo amekuwa akichonganisha
wawekezaji na wachimbaji na
kuuza ‘mida’ ya ulipuaji katika mashimo,
jambo linalosababisha vijana kukamatwa na
kupigwa na askari.
Anasema kutokana na manyanyaso
wanayoyapata hadi kufikia hatua ya
kuwafungia mashimo vijana zaidi ya mwaka
mmoja, kunasababisha kina mama na
vijana kukosa kazi.
Diwani Ganga amekuwa akiingia
makubaliano na wafanyabiashara kadhaa
kwa kuwauzia mashimo pale anapoingia
makubaliano ya uchimbaji na wahusika
(maarufu kwa jina la mida).
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la
JAMHURI umebaini kwamba hivi karibuni
kimeanzishwa kikundi kiitwacho

‘Mshikamano wa wawekezaji na wachimbaji
wadogo’

, kutokana na matukio ya

unyanyasaji uliokithiri yanayofanywa na
diwani huyo kwa wananchi wake.
Diwani huyo anatajwa kuwa katibu kwenye
kampuni yenye wakurugenzi zaidi ya saba,
huku akihusishwa pia na kuwasimamisha
wawekezaji kuchimba, na hata kuwafungia
kuchimba madini, mamlaka ambayo hana
kwa mujibu wa sheria mpya ya madini.
“Tunatambua wazi kwamba ardhi imo katika
dhamana ya rais, huyo pekee ndiye
anaweza kuzuia shughuli za uchimbaji
madini pamoja na Kamishina wa Madini…
cha kushangaza diwani amejivika mamlaka
ya Rais na Kamishna wa Madini.
“Diwani huyu amekuwa akilitumia vibaya
Jeshi la Polisi Kanda Maalamu ya
Tarime/Rorya na amekuwa ikiwavuruga
sana wachimbaji wadogo na wawekezaji,

anasema Ngusa.
Naye katibu wa kikundi cha wachimbaji
wadogo na wawekezaji, Mwalimu Sophia
Range, anasema yuko tayari kukutana na

Rais John Magufuli kumweleza
kinachofanywa katika mgodi huo.
Range anasema mbali na kuhitaji kumwona
Rais Magufuli, anajipanga kwenda Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) kutoa taarifa juu ya matumizi
mabaya ya madaraka ya diwani huyo, huku
akiingia makubaliano na wachimbaji na
kuyavunja bila makubaliano, hali inayoweza
kusababisha machafuko.
Pili Ngusa anasema diwani huyo akigundua
kuna shimo la mtu lina dhahabu
anachokifanya ni kufika na leseni yake,
anamtaka mwenye eneo husika apishe, kwa
kuwa yeye ndiye mwenye leseni.
Anasema amekuwa akitumia mabavu na
endapo mhusika akiwa mbabe zaidi yake,
anakimbilia Kanda Maalumu, huko anapewa
askari ili kutimiza azima yake.
Mfano mzuri ni tukio lililofanywa Agosti 20,
baada ya vijana kuungana na kwenda
kulala kwenye shimo la Marwa Marijani na
familia zao baada ya diwani huyo kunusa
kuwa kuna dhahabu imelipuka, alituma

vijana wake wakaingie.
Lakini wananchi wakagoma asubuhi,
waliitwa kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya
ya Tarime (OCD), Wilson Mlowola, ambaye
alisikiliza malumbano hayo na kuamua
kuwaruhusu wachimbaji wadogo waendelee
na kazi.
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini
kwamba baada ya wiki moja diwani huyo
aliamua kutafuta askari katika namna
ambayo anaijua mwenyewe, ambao walitii
maelekezo yake na kuja eneo la tukio
wakiwa na magari mawili.
Uchunguzi wetu umebaini kwamba
aliyeongoza operesheni hiyo ni Mrakibu
Msaidizi wa Polisi, Msekela, ambaye alisaini
katika kitabu cha wageni. JAMHURI
limebaini kwamba diwani huyo aliwambia
askari hao kwamba kuna maelekezo kutoka
kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), ya
katazo la kuchimba dhahabu ila vijana
wamekaidi.
ASP Msekela, ambaye alifika eneo la tukio
akiwa na askari kadhaa, alitumia busara ya

kuwauliza vijana kwa nini wamekaidi amri,
lakini kabla hawajamjibu, mzee Lugumba
Mwita, alisema hawajapata barua yoyote na
ndiyo maana wanachimba dhahabu.
Baada ya kujionea hali halisi, ASP Msekela,
aliwambia alikuwa amejipanga na askari
wake kuhakikisha wanasimamisha shughuli
za uchimbaji mpaka kikao kifanyike.
Marwa Marijani alianzisha shimo hilo
mwaka 2000 kwa gharama nyingi, kwa
kuuza mifugo ili kuwalipa wafanyakazi, kwa
muda mrefu hadi mwaka juzi ndipo akaanza
kupata dhahabu, ila alipopata hakuifaidi
mwanzoni mwa mwaka jana eneo hilo
likafungiwa.
Marwa Marijani pamoja na mdogo wake,
Mwita Marijani, wenye eneo la uchimbaji
namba 582, wamesimamisha shughuli za
uchimbaji na wenye mashimo ndani ya
eneo hilo, wakimsubiri Kamishna wa Madini
ambaye aliitwa na Ganga, hata hivyo
hakufika kama ilivyokuwa imepangwa.
Gazeti la JAMHURI limemtafuta diwani
huyo ili kujibu tuhuma zinazomkabili,

ambaye alitoa majibu ya ‘nyodo’ huku
akijinasibu kwamba, hao wanaomlalamikia
kwa nini wasimpeleke mahakamani.
Licha ya kwamba utaratibu wa kuchimba
uliwekwa na wakurugenzi hao kwa
kushirikiana na wawekezaji na wachimbaji
wadogo, lakini umekuwa unavunjwa
kutokana na masilahi binafsi.
Utaratibu wa kuchimba uko kama ifuatavyo;
mwekezaji ambaye ndiye mchimbaji wa
shimo la dhahabu anatakiwa kuwa na zamu
nne za kulipua dhahabu, anafuatia mwenye
leseni, ambao ni hao wakurugenzi zamu
tatu, wanafuatia wenye vifaa vya kazi zamu
mbili na mwisho mwenye ardhi naye zamu
mbili.
Diwani Ganga amekuwa akikiuka utaratibu
huo kwa kutumia madaraka yake, wengi
wananyanyaswa, Jeshi la Polisi limekuwa
likifanya kazi kwa amri yake.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kebaga, Kwame
Nsenga, aliamua kuitisha mkutano wa
hadhara kutokana na matukio mengine ya
nyuma ya kuhatarisha amani na usalama

lakini diwani huyo aliuharibu.
Lakini baadaye diwani huyo aliwaomba
radhi wananchi kwa kile anachowatendea
na kuahidi kutorudia, lakini baada ya
dhahabu kuanza kupatikana kwa wingi
kwenye shimo la Marwa Marijani, aliweka
kando ahadi yake na sasa ni vilio kwa
vijana, wazee na kina mama.
Wakili aliyefika kwenye kikao cha kikundi
cha mshikamano wa wachimbaji na
wawekezaji, Mary Samson, aliwambia
wanachama hao kwamba sheria inatambua
mikataba aina mbili; ya maandishi pamoja
na ya maneno, ambapo wakurugenzi na
wawekezaji na wachimbaji walikuwa
wakikubaliana kwa maneo na si maandishi.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Mkuu
wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga,
amesema hana mgogoro wowote
unaohusiana na Kibaga Mining ofisini
kwake, huku akisisitiza kwamba kulikuwa na
mgogoro mmoja ambao alikwisha
kuumaliza.
Luoga anasema hana mgogoro baina ya

wawekezaji na wenye ardhi katika mgodi
mdogo wa dhahabu uliopo Mtaa wa Kibaga,
Kata ya Kenyamanyori.
“Niko kwenye maandalizi ya Mwenge…
sema shida yako, mimi sina mgogoro
wowote ofisini kwangu unaohusu Kibaga
Mining… nilikuwa na mgogoro wa shimo
moja nilishaumaliza. Naomba uelewe kuwa
sina mgogoro huo,

” anasema Luoga.

Hata hivyo wananchi hao wanaonyanyaswa
wamefanya jitihada za kufikisha kilio chao
kwa Rais John Magufuli baada ya kufanya
jaribio la kuingia na mabango yao katika
Chuo cha Ualimu Tarime, ambako Rais
Magufuli alifanyia mkutano wake.
Mabango hayo yalizuiliwa na walinzi
waliokuwa kwenye lango maalumu
lililoandaliwa kuingia chuoni hapo, badala
yake wakaingia na kuacha ujumbe wao
mahususi nje.
Hata hivyo Gazeti la JAMHURI limemtafuta
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Yaredi
Kiboye, ili kufahamu kama amekwisha
kupokea malalamiko yoyote yanayomhusu
diwani huyo wa CCM, amesema amekuwa
anasikia ila hajapata malalamiko rasmi.

“Ila kwa kuwa sasa jambo hili limefika
kwenu, lazima nilifanyie kazi ili kulinda
taswira ya CCM, naomba uniulize baada ya
siku kadhaa nitasema tumefikia wapi,

amesema Kiboye.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share