Kuna usemi usemao unapopima maendeleo ya mtu usiangalie alipo, angalia mahali alipotokea. Usemi huo ndiyo unayagusa maisha ya Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), hususani katika muktadha wa elimu.

Lusinde amekuwa Mbunge wa Jimbo la Mtera, Mkoani Dodoma katika vipindi viwili, akianza utumishi huo kwa wanamtera tangu uchaguzi wa 2010. Katika uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi alimshinda aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi kadhaa na Waziri Mkuu mstaafu, Samweli Malecela.

Katika mahojiano maalum na Gazeti la JAMHURI, amesema kwamba hakuwahi kuhitimu wala kutunukiwa cheti cha darasa la saba, lakini kwa jitihada binafsi, ameweza kujua kusoma na kuandika.

Lusinde, ambaye mara nyingi bungeni amekuwa akikabiliana na wapinzani ndani ya Bunge hasa pale panapojitokeza hoja nzito, Amesema ingawa hakupata cheti hicho, amewekeza kwa kiwango kikubwa kwa watoto wake kupata elimu bora; ili, pamoja na mambo mengine, waepukane na kadhia alizokutana nazo.

Lusinde ni baba wa watoto wanne, kati yao kuna mapacha Penina na Isaya, wengine ni Neema na Lydia. Neema, amehitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Green Acres, na sasa anaendelea na masomo ya juu katika Chuo cha Bandari, jijini Dar es Salaam.

Lydia amehitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mtakatifu Peter Clever, wakati Penina amehitimu darasa la saba mwaka jana katika Shule ya Msingi Martin Luther King, shule iliyoko mjini Dodoma.

Lusinde amesema amekuwa akitumia wastani wa shilingi milioni 12 kila mwaka kwa ajili ya kuwalipia ada watoto wake, lengo likiwa ni kuwawezesha wapate elimu bora ili wakabiliane na mazingira ya sasa.

“Huwa natumia sehemu kubwa ya mshahara wangu kugharamia elimu ya watoto wangu, nisingependa na ninamuomba Mwenyezi Mungu awasaidie, wasipitie maisha yenye hali ngumu kama niliyopitia mimi,” amesema.

Anaongeza, “Nimefanikiwa kimaisha kwa uwezo wa Mungu tu, neema ambayo si rahisi kila mtu kuipata.”

MWANAYE AONGOZA DODOMA

Lusinde amesema, pamoja na kuomba dua hiyo, ishara njema kwa mafanikio ya kielimu kwa watoto zimeanza kuonekana baada ya mwanae, Penina, aliyehitimu darasa la saba mwaka jana, akiwa wa tano miongoni mwa wanafunzi 10 bora waliofaulu vizuri mkoani Dodoma.

Hata hivyo, watoto wa Lusinde wanatambua ‘kiu’ ya baba yao kuwajengea msingi mzuri wa elimu.

Penina anazungumzia mafanikio yake akisema bidii ya wazazi, utayari wa kuhudumia mahitaji yao na hamasa, vimechangia kuwa miongoni mwa wanafunzi bora.

Pia anasema bidii ya walimu katika kufundisha na kutia moyo, pamoja na jitihada binafsi katika kuzingatia masomo na ushauri ni nyenzo zinazoongoza kupata matokeo mazuri.

Ishara za Penina kufanya vizuri kitaaluma zilianza kudhihirika akiwa darasa la nne alipowekwa kwenye kundi la wanafunzi wenye uelewa mkubwa.

Akiwa darasa la saba, Penina alishika nafasi ya tano kwa wasichana waliofanya mtihani uliohusisha shule binafsi mkoani Dodoma.

Kwenye matokeo ya mtihani wa taifa, Penina alishika nafasi ya tano kwa wanafunzi bora mkoani humo akiwa na wastani wa alama 225.

NDOTO YA UDAKTARI

Penina amesema tangu akiwa mdogo, alihisi kuwasaidia watu wenye shida za kiafya na alipoingia darasa la nne, alibaini kwamba wito huo ni kuwa mtaalamu wa masuala ya afya ya binadamu.

Mama yake Penina, Edna Lusinde amemwelezea binti yake, kama binti mwenye huruma kwa wengine hususani wenye matatizo kiafya na kwamba hashangazwi na ndoto yake ya kuwa daktari wa binadamu.

Mwaka huu, Penina anatarajiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza katika shule moja ya jijini Dar es Salaam.

Lusinde amesema ufaulu mzuri wa Penina umempa hamasa ya kuwekeza zaidi kwenye elimu ya watoto wakati akijiendeleza kwa namna isiyoathiri uwajibikaji kwa watoto hao.

KWA NINI LUSINDE HAKUSOMA

Lusinde amesema miaka miwili baada ya kuzaliwa kwake, baba yake mzazi alifariki na kwamba tukio hilo lilimfanya akose huduma za elimu, hivyo kuishia darasa la pili. Wakati huo, Lusinde aliyezaliwa Machi 4, 1972 hakujua kusoma na kuandika.

Anasema mama yake mzazi hakuwa na uwezo wa kumgharamia. “Ninafahamu umuhimu wa elimu na nina uhakika ningepata fursa nzuri ya kusomeshwa, ningekuwa miongoni mwa wasomi wazuri nchini na duniani kwa sababu uwezo wa kiakili ninao,” amesema Lusinde.

KUANDIKA KITABU

Lusinde amesema hivi sasa anaandika kitabu chenye historia ya maisha yake, akikipa jina la ‘Safari Yangu’ anachoamini kwamba kitawawezesha waliovunjika moyo kutokana na ugumu wa maisha, wajue kwamba kuna mafanikio.

Amesema miongoni mwa mambo yaliyomfikisha katika hatua kubwa ya mafanikio ni pamoja na kuwa na msimamo, uwezo wa kufanya uamuzi sahihi na uaminifu.

UBUNGE                                                      

Lusinde alishinda ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010, alipoweka historia dhidi ya aliyekuwa Mbunge na mwanasiasa mkongwe katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Malecela. Malecela aliwahi pia kuwa Waziri Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara).

2605 Total Views 15 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!