Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani, kimepinga taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamishna wa Madini Tanzania, kikisema itavuruga amani na utulivu katika machimbo ya tanzanite ya Mirerani mkoani humo.

MAREMA wamesema: “Chama kimepokea kwa masikitiko makubwa majibu ya Kaimu Kamishna wa Madini Tanzania aliyotoa Novemba 13, 2015. Kutokana na majibu hayo tunatoa tamko kulaani kwa nguvu zetu zote kauli ya Kaimu Kamishna wa Madini kwa kuwa amechafua hali ya hewa Mirerani.

“Majibu ya Kaimu Kamishna siyo tu yanashindwa kutatua mgogoro kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo, bali yataondoa hali ya kuwapo kwa amani katika eneo la machimbo la Mirerani.

“Majibu hayo ya Kaimu Kamishna hayakutarajiwa na wachimbaji wadogo pamoja na wadau wa tanzanite, hasa ikizingatiwa kuwa katika kikao cha kamati ya kutafuta ufumbuzi wa suala la uchimbaji wa madini ya tanzanite lengo lilikuwa ni kuondoa uhasama kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo kwa kuwa chanzo cha mgogoro kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo wa Tanzanite ni mpaka kati ya kitalu ‘B’ na ‘C’,” imesema taarifa ya MAREMA.

Taarifa hiyo imetiwa saini na Katibu wa MARENA, Tawi la Mirereni, Abubakari Madiwa; na Mwenyekiti wa MAREMA wa Tawi hilo, Jafari Faraji.

Kaimu Kamishna wa Madini ni Mhandisi Ally Samaje. Alishika nafasi hiyo baada ya Mhandisi Paulo Masanja, kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.

Kamishna wa Madini aliunda Kamati ili kutoa mapendekezo ya utaratibu wa uchimbaji tanzanite Mirerani.

Pamoja na mambo mengine, ilitoa mapendekezo na ushauri wa namna ya kutatua mgogoro kati ya mchimbaji mkubwa na wachimbaji wadogo kwa kupitia nyaraka na mapendekezo ya tume mbalimbali zilizowahi kuundwa na Serikali kushughulikia mgogoro huo unaohusu mpaka.

“Kwa kuwa, pia kamati ilitoa mapendekezo ya rasimu ya Kanuni maalumu za uchimbaji wa madini ya vito vya tanzanite itakayotumika kutatua migogoro ya wachimbaji wakubwa na wadogo; hivyo basi, tunalaani kwa nguvu zote tamko la Kaimu Kamishna wa Madini Tanzania ambalo limesigana kwa kisigino taarifa ya Kamati na mapendekezo yake ambayo ndiyo yaliyokuwa mwarobaini wa kumaliza mgogoro kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo wa tanzanite, Mirerani.

“Badala yake ametoa tamko ambalo limeongeza chuki na kuibua hasira kwa wachimbaji wadogo; jambo ambalo linaweza kusababisha machafuko na vurugu ambazo zitaleta hasara na madhara makubwa kwa wachimbaji wa tanzanite na kuvuruga biashara ya madini hayo duniani,” imesema taarifa hiyo.

Kaimu Kamishna aliahidi kwamba mgogoro wa mpaka ataupeleka ngazi za juu zaidi kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

Imebainika kuwa Kaimu Kamishna ametoa haki kwa kampuni ya TanzaniteOne Mining Company Ltd/ STAMICO kuchimba katika eneo lenye mgogoro ambao haujapatiwa ufumbuzi huku akiwataka wachimbaji wadogo kuingia mikataba ya kuendeleza uchimbaji migodi yao ndani ya eneo lenye mgogoro kwa kufuatia masharti yatakayotolewa na kampuni ya TanzaniteOne Mining Company Ltd/ STAMICO.

“Jambo hili tunaona ni la kikatili, udhalilishaji, halikubaliki na linapaswa kulaaniwa na wachimbaji wote wadogo wa tanzanite.

“Kwa kuwa Kaimu Kamishna ameamua kwa makusudi kusigina taarifa na mapendekezo ya Kamati tunadiriki kusema kuwa uamuzi huo wa Kaimu Kamishna haujazingatia maslahi mapana ya Taifa, wakazi wa mji wa Mirerani na mikoa ya jirani pamoja na wachimbaji wanaohusika katika mgogoro huu.

“Uamuzi huu unaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwamo kuvurugika amani na umwagaji damu isiyo na hatia jambo ambalo linaweza kusababisha tanzanite ihusishwe na vitendo vya umwagaji damu, hatimaye itangazwe kuwa ni tanzanite ya damu.

“Kitendo hicho kinakwenda sanjari na yaliyoandikwa kwenye Jarida la Wall Street (Novemba 2001) lililohusisha biashara ya tanzanite na mtandao wa kigaidi uliokuwa unaongozwa na Osama Bin Laden (Al- Qaeda), ambayo iliharibu biashara ya tanzanite duniani.

 

“Hali hiyo ilisababisha ujumbe mzito kutoka Tanzania kwenda Marekani kusafisha tuhuma za madini ya tanzanite kuhusishwa na mtandao wa kigaidi.

Kutokana na hayo tunatoa tahadhari kwamba litakalotokea sasa kutokana na kitendo cha Kaimu Kamishna litakuwa gumu kusafishika na matokeo yake uchimbaji na biashara ya tanzanite vitakuwa imetoweka kitaifa na kimataifa.

“Kaimu Kamishna wa Madini itabidi awajibike kwa lolote litakalotokea.

Kutokana na haya sisi kama  wadau wa tanzanite tunaiomba Serikali na kuzishauri mamlaka zinazohusika zirejee katika mapendekezo halisi yaliyotolewa na Kamati iliyoteuliwa na aliyekuwa Kamishna wa Madini Juni 30, 2015 kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa suala la uchimbaji wa madini ya tanzanite katika eneo la Mirerani mkoani Manyara.

“Kwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kulinda kwa nguvu zote rasilimali za nchi hii; na kwa kuwa tunaamini kuna udanganyifu mkubwa katika uvunaji wa madini ya tanzanite kupitia wawekezaji wakubwa, tunaomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aingilie kati suala hili ili kulinda uchimbaji tanzanite ili uwe wa manufaa kwa Taifa -sasa na kwa vizazi vijavyo,” imesema taarifa ya MAREMA.

1357 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!