magufuli1Kasi ya utendaji kazi ya Rais John Magufuli, imefanikisha kuanza kufungwa kwa mita 12 za kupimia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.

Rais Magufuli, baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), mashine za MRI zilianza kufanya kazi saa chache baadaye; na sasa ni zamu ya mashine za kupimia mafuta yanayoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam kuanza kufanya kazi.

Awali zilizokuwapo kulizuiwa na Wakala wa Vipimo (WMA) zisitumike miaka minne iliyopita kwa madai kuwa zinapunja wateja.

Biashara ya mafuta ni eneo ambalo Serikali imekuwa ikipoteza mabilioni ya shilingi kutokana na ukwepaji kodi.

Kwa miaka mingi, wafanyabiashara wamekuwa na mtandao wenye nguvu kubwa unaotajwa kuwa wa hatari.

Kufungwa kwa mita hizo kumekuja huku Rais Magufuli, akiwa ameishaandaa mpango mahsusi wa kuongeza mapato na kukabiliana na wakwepa kodi wakubwa waliokubuhu.

“Eneo la mafuta ni la kifo, kuna watu wenye nguvu kubwa ya fedha. Unadhani kifo cha yule ofisa wa EWURA kilikuwa cha kawaida? Udanganyifu unaanzia kwenye uingizaji mafuta nchini hadi usafirishaji.

“Kuna kampuni zinadai kupeleka mafuta nje, lakini mwishowe yanauzwa Dar es Salaam, Kibaha na mikoa mingine nchini bila kulipiwa kodi. Kuna kodi inakwepwa kwenye mafuta yanayotumika migodini na kwingine, hali ni mbaya, lakini chanzo kikubwa kabisa ni kwenye mita. Walihakikisha mita hazifanyi kazi,” kimesema chanzo chetu.

Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Awadhi Massawe, zinasema mita hizo 12 zimeanza kufungwa katika eneo la Kigamboni.

Massawe alithibitishwa na Rais Jakaya Kikwete (kabla ya kustaafu) hivi karibuni kushika wadhifa huo uliokuwa ukishikwa na Madeni Kipande, aliyeondolewa kwa tuhuma za utendaji mbovu.

Kufungwa kwa mita hizo zenye thamani ya Sh bilioni 11 ni pigo kubwa kwa wafanyabiashara ya mafuta ambao walilitumia aneo hilo la mafuta kama pepo yao kuu ya ukwepaji kodi.

Sakata la kusitishwa kwa matumizi ya mita hizo lilianza mwaka 2011 wakati ambao katika mazingira yasiyo wazi, WMA walisitisha utumiaji wa mita zilizokuwapo kwa madai kwamba hazifai kwa matumizi ya kupima mafuta yatokayo melini.

Kamishina wa WMA, Magdalena Chuwa, alichukua uamuzi wa kusitisha matumizi ya mita hizo kupitia barua yake ya Februari 02, 2011 kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA.

WMA walitoa sababu kadhaa za uamuzi huo, zikiwamo kwamba mita hizo zilikuwa zikifanya kazi katika kiwango cha nyuzijoto sentigredi 15 badala ya 20; na kwamba mita hizo zimetengenezwa kwa ajili ya kujaza na si kupakua mafuta.

Dosari hiyo, kwa mujibu wa WMA, ilisababisha usumbufu mkubwa wa foleni kwa wateja na hivyo kuongeza gharama za bei ya mafuta kwa watumiaji.

Uamuzi huo wa WMA uliibua msuguano mkali kati yake na TPA ambao waliamini kuwa usitishwaji wa mita hizo ulikuwa na athari kubwa mno kutokana na kulikosesha Taifa mapato.

“Nina furaha kusema kuwa mita 12 zimeanza kufungwa Kigamboni, zitasaidia kuongeza mapato ya Serikali kwa upande wa mafuta ambayo tumekuwa tukiamini yanapotea,” amesema Massawe.

Mita za awali zilifungwa katika gati maalumu la Kurasini, lakini hizi mpya zinafungwa eneo la Kigamboni.

Matumizi ya mita yaliafikiwa na Serikali baada ya kubaini upotevu mkubwa wa kodi kwenye mafuta yanayoingizwa nchini.

Hatua hiyo iliilazimu Serikali kuagiza matumizi ya vipimo vya uhakika zaidi badala ya ukadiliaji au kupokea taarifa za waagizaji pekee.

Pia hatua hiyo ililenga kuongeza mapato ya ushuru kwa Bandari na kodi kwa Serikali. Hoja nyingine kubwa ilikuwa ni kwa Serikali kuwa na kumbukumbu sahihi za mafuta yanayoingizwa nchini.

Ufungaji wa mita hizo ulikamilika mwishoni mwa mwaka 2004 na kuanza kutumika mapema mwaka 2005.

TPA iliandaa mafunzo kwa wadau muhimu kwenye sekta ya biashara ya mafuta ambao ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za NIshati na Maji (EWURA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), WMA na Shirika la Tanzania Italy Petroleum (TIPER).

Mei, 2010 TRA iliiandikia TPA barua ikidai kuwa mita hizo zilikuwa na matatizo, hasa kwenye mita za mafuta ya dizeli; wakati ambao TPA ilikuwa imebadilisha matumizi ya bomba la mafuta ghafi yaendayo TAZAMA ili kusafirishia mafuta ya dizeli.

Uchunguzi unaonyesha kuwa matumizi ya mita yalisaidia mno kuongeza ukusanyaji mapato kwa kiwango cha juu hadi ilipofika Februari 2011 ambako WMA walipoamua kusitisha matumizi ya mita hizo wakidai kwamba hazifai.

WMA wakataka mfumo wa upimaji mafuta unaoitwa “Accuload III” uondolewe kwa madai kuwa haufa kwa matumizi ya vipimo, badala yake TPA waweke mfumo mpya unaoitwa “Sybertrol”. Mifumo yote imetengenezwa na kampuni moja.

Kamati ya wataalamu iliyoaundwa kuchunguza suala hilo hawakukubaliana na kubadilisha mfumo ambao TPA walikuwa wameona unafaa.

TPA iliamua kuchukua hatua za kujirisha kama kweli mfumo huo haufai; na ikaamua kuwasiliana na wataalamu kutaka ufafanuzi kuhusu ubora kati ya mifumo hiyo miwili.

Uchunguzi wa JAMHURI kupitia nyaraka za mawasiliano unaonyesha kuwa wataalamu walijibu kuwa mfumo wa “Accuload III” ni wa kisasa na unafaa zaidi kwa matumizi ya vipimo. Baada ya majibu hayo, TPA iliomba wataalamu wafike nchini kuikagua na kutoa ushauri na kufanya marekebisho kama yangehitajika.

Wataalamu wa mifumo yote miwili walifika nchini Agosti, 2011 na kutoa ufafanuzi mbele ya wadau ambao ni wawakilishi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uchukuzi, WMA, TBS, EWURA na TPA.

“Wataalamu waliweza kutoa majibu juu ya masuala yote yanayowatatiza WMA kuhusu mifumo hiyo miwili na faida za Accuload III.

“Pamoja na juhudi zote hizo, WMA walisema kuwa kuleta wataalamu siyo sababu zitakazowafanya waruhusu mita kutumika,” kimesema chanzo chetu.

Mzunguko wote huo kwa wakati huo, yaani ukaguzi wa mita, ununuzi wa vipuri na matengenezo uligharimu dola 260,000 za Marekani. Kiwango cha dola moja ya Marekani kwa wakati huo kilikuwa sawa na Sh 1,600.

Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, alizungumza na waandishi wa habari na kueleza furaha yake kutokana na agizo la Rais Magufuli, la kutaka Mamlaka hiyo iwashughulikie wakwepa kodi bila woga.

Bade alisema “rungu” walilokabidhiwa na Rais litasaidia kuwadhibiti wale wote waliokuwa wakikwepa kodi kwa kukingiwa kifua na baadhi ya wakubwa serikalini.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Elimu ya Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, ameiambia JAMHURI: “Kufungwa kwa mita mpya za mafuta ni kitu kizuri, tuna hakika sasa ya kupata mapato sahihi.”

Huku hayo yakiendelea, JAMHURI limepata taarifa kuwa TPA imepangua wafanyakazi hasa wa idara ya uhasibu zaidi ya 30.

Sababu kuu ya kupangua wafanyakazi hao ni kutokana na wengi kufanya kazi kwa mazoea na kuwapo tuhuma kuwa baadhi walikuwa si waaminifu.

“Ingawa hatuna ushahidi wa wazi, lakini wakimtuhumu mfanyakazi mara kadhaa nasi inatupasa kuchukua hatua kwa kufuatilia utendaji wake na tusipopata ushahidi wa kimahakama ila kiutawala tukajiridhisha kuwa matendo yake hayaendani vizuri na sera ya utumishi wa umma, kwa kuokoa lisitokee janga tunamhamisha,” alisema mmoja watendaji wa TPA.

Massawe kwa upande wake alipoulizwa, alisema: “Kilichotokea ni uhamisho wa kawaida tu. Hata timu kocha huona leo mchezaji fulani acheze namba 6 au 8, siku nyingine anapangwa namba 10, yote haya tunayafanya kwa nia ya kuboresha utendaji. Kimsingi tunataka wafanyazi wachape kazi. Hapa hakuna kubebana,” anasema Massawe.

 

Ukwepaji kodi

Desemba 2013, iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma (PAC), ilifichua udanganyifu na mianya mikubwa ya ukwepaji kodi katika TRA.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini-CHADEMA) (sasa Mbunge wa Kigoma Mjini-ACT), Kabwe Zitto, alisema kuwa pamoja na TRA kufikia malengo kwenye makusanyo ya kodi katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, bado kulikuwapo udanganyifu na mianya ya ukwepaji kodi katika maeneo kadhaa.

Eneo kubwa alilolitaja ni la kusitishwa kwa matumizi ya mita za kupima ujazo wa mafuta yanayoingia nchini kupitia kituo cha kupakulia mafuta cha Kurasini, Dar es Salaam. 

Kamati iliitaka Serikali kulieleza Bunge sababu za msingi za kusitisha matumizi ya mita hizo na TRA kuainisha athari katika ukusanyaji wa mapato baada ya kusitishwa kwa matumizi ya mita hizo.

Alisema TPA baada ya kusitishwa kwa matumizi ya mita hizo ilitumia vijiti vya kupimia ambavyo vipimo huchukuliwa wakati mafuta yako kwenye meli na baada ya kuwekwa kwenye matangi ya wafanyabiashara walioyaingiza mafuta hayo.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika taarifa yake ya 2010/2011 alihoji sababu za kusitisha matumizi ya mita hizo katika bandari za Tanga na Dar es Salaam.

Kamati iliwahoji maofisa masuuli wa TPA walioeleza kuwa mita hizo zilinunuliwa mwaka 2004 na TPA na kufungwa katika kituo cha kupakulia mafuta cha Kurasini (KOJ) na kuanza kutumika mwaka 2005 kwa lengo la kupima kiwango cha mafuta yanayoingizwa nchini kupitia Bandari za Tanga na Dar es Salaam.

Februari 2011, WMA iliyoridhia awali matumizi ya mita hizo, iliwaandikia barua TPA kusitisha matumizi yake.

TPA kwa upande wao walisema mita hizo hazina matatizo yoyote na zinaweza kuendelea kutumika lakini WMA wakasisitiza kuwa mita hizo hazitoi vipimo sahihi.

Ripoti ya utafiti iliyotolewa na Shirika linalojihusisha na masuala ya uchumi la nchini Marekani la GFI mwaka jana inaonyesha kuwa Tanzania inapoteza Sh trilioni 3 kila mwaka kutokana na ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni za uchimbaji madini na katika uingizaji bidhaa na kuuza nje.

Udanganyifu mkubwa umebainika kuwapo kwenye uingizaji mafuta ya kuendeshea mitambo na magari katika migodi mbalimbali nchini.

Kiwango hicho cha ukwepaji kodi kwenye eno hilo ni sawa na asilimia 16 ya bajeti ya Serikali na ni mara tatu ya kile ambacho Serikali ilitangaza kukopa kupitia mashirika ya mikopo yenye masharti nafuu katika bajeti yake ya mwaka 2014/2015.

 

Kifo cha Ofisa wa EWURA utata

 Meneja Biashara wa Petroli wa EWURA, Mei mwaka jana alikutwa amekufa hotelini katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kutoka Dodoma ambako alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti.

Meneja huyo, Julius Gashaza, alikuwa mpangaji bei za mafuta za kila mwezi. Alihudhuria kikao hicho mjini Dodoma kwa siku mbili kuhusu mambo mbalimbali, yakiwamo kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na EWURA kwenda kwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Mfuko wa Barabara.

Alikutwa amejinyonga kwa kutumia tai kwenye hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo Vituka, Temeke.

Kamati ya Bunge ya Bajeti, iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ilikutana na maofisa wa EWURA, akiwamo Gashaza na wale wa TRA na kugundua kuwapo kwa tofauti katika takwimu za kiwango cha mafuta kilichostahili kutozwa kodi.

Takwimu za EWURA ziliashiria kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi ya zile zilizoelezwa na TRA, lakini Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe takwimu za TRA.

Baada ya kurejea Dar es Salaam Gashaza hakwenda nyumbani kwake na badala yake alikwenda kwenye hoteli iliyo karibu na nyumbani ambako mkewe na ndugu yake mmoja walimfuata na akawambia kuwa anatishiwa maisha, kisha baadae akakutwa amefariki.

By Jamhuri