*Tamisemi, Hazina, CCM wahusishwa

Madiwani watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa Halmashauri ya Mji wa Geita, kwa kushirikiana na mmoja wa Viti Maalum wa Halmshauri ya Wilaya ya Geita, wametoa nyaraka katika mkutano hadhara uliofanyika Julai 14, mwaka huu, zinazoonesha wilaya hiyo kupokea Sh bilioni 11 kwa ajili ya ununuzi wa madawati lakini matumizi yake hayajulikani.

Katika kile kinachoaminika kuwa ni ufisadi wa fedha za umma, imebainika kuwa halmashauri hiyo mwaka 2012 ilipokea shilingi 11,131,035,000 kwa ajili ya kununua madawati kwa shule zote 271 za msingi lakini fedha hizo hazikufika kwenye shule husika.

 

Nyaraka hizo zinaonesha kuwa fedha hizo zilipangiwa matumizi na kuingizwa katika akaunti za shule husika katika Benki ya NMB Tawi la Geita.

Madiwani hao – Peter Donald (Kata ya Kalangalala), Fabian Mahenge (Kasamwa) na Marcellina Simbasana (Viti Maalum) wamesema:  “Tumepata nyaraka hizi, pesa zililetwa kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kununua madawati kwa shule za msingi lakini wamepanga matumizi wakaita walimu wakuu wakasaini zikaenda mifukoni mwa wajanja wachache….”

 

Uchunguzi wa mwandishi wa habari hii umebaini kuwa hakuna shule yoyote iliyopokea fedha hizo kwenye akaunti za shule hizo mwaka 2012 kwa ajili ya ununuzi wa madawati kama mgawo huo unavyoonekana katika nyaraka hiyo.

Taarifa hizo zinakuja mwezi mmoja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magallula Said Magallula, kuagiza wananchi wote wachangie fedha kupitia kwa watendaji wa mitaa na vijiji kwa ajili ya kununua madawati ili kumaliza tatizo la madawati katika shule za msingi mkoani humo.

Uchunguzi umebaini pia kuwa nyaraka hiyo inayoonesha mgawo huo wa bilioni 11.1 kwenda akaunti za shule hizo, inafanana kwa kila kitu na nyaraka nyingine zilizopo katika halmashauri hiyo zilizotumika kupanga migawo mbalimbali ya fedha za shule za msingi.  Tofauti iliyopo ni kiwango cha pesa lakini vitu vingi vinafananaa.

 

Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, kwenye ukuta wa jengo la ofisi za Idara ya Elimu ya msingi wilayani Geita, kulikuwa na tangazo linaloonesha mgawo wa fedha kwa shule zote ambao umepangwa kwa mfanano ule ule kama nyaraka hii ya Sh bilioni 11.1.

Chanzo chetu cha habari kutoka katika halmashauri hiyo Idara ya Uhasibu kimedai; “Kuna madudu mengi yanafanywa na ni mtandao mrefu unaohusisha watu fulani wa Tamisemi, Hazina na viongozi fulani wa CCM, hata wewe angalia yawezekana ukifuatilia hili utapambana na matatizo makubwa sana.”

Baadhi ya walimu wakuu wa shule zilizopo Geita Mjini wameiambia JAMHURI kuwa kuna wakati wanaitwa na maafisa wa Idara ya Elimu na kulazimishwa kusaini fomu za kukiri kupokea fedha kwenye akaunti za shule, lakini fedha hizo huwa haziingizwi kwenye akaunti za shule zao na wakiulizwa wanajibiwa kuwa pesa hizo zilipangiwa kazi nyingine.

“Kuna wakati walimu wakuu wote wilaya nzima tuliitwa na tukalazimishwa kusaini fomu fulani za kukiri kupokea pesa za kuendesha shule kwa makubaliano kuwa pesa zitaingizwa kwenye akaunti za shule zetu, lakini hadi leo mwaka umekwisha hizo pesa hazijaingizwa, sasa huu kama sio wizi ni nini wakati tulishasaini kukiri kuzipkea?” Amesema mwalimu mmoja.

Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Dankan Tebas, amesema “Hakuna fedha kubwa kiasi hicho iliyotolewa kwa ajili ya madawati mwaka 2012, sisi tulipokea milioni 11 tu mwaka huo na kama tungepokea hata bilioni tatu tusingekuwa na tatizo la dawati hata moja.”

Alipoulizwa nyaraka ziliandaliwa kwa malengo gani na kuwapo ofisini kwake na zinaonesha kupokea Sh bilioni 11.1 za madawati na zinaonesha namba zote za akaunti za shule zote, idadi ya wanafunzi na kiasi cha pesa kila shule lakini yeye anaikana wakati inaonesha zimeandaliwa kama zile zilizomo ofisini kwake, haraka haraka amejibu:

“Labda atuambie afisa elimu, lakini mimi nakumbuka tulipokea milioni 11 tu hizo nyingine sizijui.”

Diwani wa Kata ya Kalangalala, Peter Donald (Chadema) amesema; “Hata mimi hizo taarifa ninazo, lakini bado nakusanya ushahidi mwingine ili nione nianzie wapi maana pale halmashauri pananuka rushwa na ukienda vibaya unakwamishwa, hata madiwani wenzako kuna mtandao wa wizi unaohusisha hata madiwani wenzetu,  kuna ubadhirifu.”

Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina historia ya kupata hati zenye mashaka kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mfululizo wa miaka miwili, ambapo CAG amependekeza hatua mbalimbali za kisheria na kiutawala zichukuliwe dhidi ya viongozi wa halmashauri hiyo.

Juni 2013, Takukuru iliwapandisha mahakamani watumishi watano kwa makosa mbalimbali likiwamo la kuhujumu uchumi akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Benson Tatala, wakituhumiwa kwa kuiba Sh 18,750,000 zilizotengwa kugharimia ujenzi wa zahanati.

By Jamhuri