*Akiri kuwa kazi hiyo si nyepesi

Kukifuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) si rahisi; amethibitisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

Kauli ya Wasira imekuja huku wahafidhina ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakishinikiza Chadema ifutwe kwenye Daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kwa madai kuwa inakusudia kuifanya nchi isitawalike.

 

Hivi karibuni Chadema ilisema itaimarisha kikosi chake cha Red Brigade ili ichukue dhima ya kuwalinda viongozi wake baada ya Polisi kushindwa kufanya hivyo.

 

Wasira ambaye amewahi kuwa mbunge kupitia pande zote mbili – CCM na upinzani – anasema badala ya kuwaza kuifuta Chadema, ni vema wananchi wakashiriki maombi ili Mungu awape (Chadema) mawazo yatakayoafikiana na hali halisi ya kisiasa na maendeleo nchini.

 

Anasema kitendo cha chama hicho kutangaza hadharani kuanzisha ‘jeshi’ la kuwahami viongozi wake, ni uvunjaji wa wazi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mwishoni mwa mwaka jana, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alisema ana mamlaka ya kukifuta chama chochote kinachohatarisha amani, hata kama kina wabunge. Kauli yake iliilenga Chadema.

 

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 147 (1) inatamka, “Ni marufuku kwa mtu yeyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania jeshi la aina yoyote.

 

(2) Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza, kwa mujibu wa sheria, kuunda na kuweka Tanzania majeshi ya aina mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wa Tanzania.

 

(3) Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kama atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii.

 

(4) Kwa madhumuni ya ibara hii, “mwanajeshi” maana yake ni askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa.”

 

Katika mahojiano na JAMHURI, Wasira amewataka viongozi na wafuasi wa Chadema wakae, watafakari vema msimamo wa Watanzania juu ya mustakabali wa amani hapa nchini.

 

“Sidhani kama Watanzania wataunga mkono Chadema ifanye inayotaka kufanya, nawashauri wasome alama za nyakati, wasome mood (hisia) ya Watanzania waone kama wanachotaka kukifanya kinaingia katika akili au hisia za kawaida,” amesema.

 

Waziri huyo amesema Chadema hawawezi kuunda jeshi na wakati huo huo wakawa wanataka kuiondoa CCM madarakani.

 

“Huwezi kuunda jeshi eti kwa sababu huamini Polisi, JWTZ na majeshi mengine yaliyopo kikatiba. Huwezi kutaka kuingia madarakani, hapo hapo unataka kuwang’oa Polisi na JWTZ halafu uunde Red Brigade. Nadhani hapo wameenda mbali. Hawa ni wa kuwaombea kwa Mungu wapate mawazo yanayoafikiana na hali halisi,” amesema.

 

Anasema kuanzishwa kwa Red Brigade kwa kigezo kuwa CCM ina Green Guard, si sahihi kwa kuwa Green Guard ni tawi ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

 

“Wao wana BAVICHA. Hakuna anayewazuia kuwa na vijana ndani ya Bavicha kama ilivyo kwa UVCCM. Lakini kuwa na military training (mafunzo ya kijeshi) hairuhusiwi, ni illegal (haramu) kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi,” amesema.

 

Alipoulizwa Serikali itachukua hatua gani hasa baada ya Chadema kutangaza kuwa inaendelea na mpango wake wa kuwapa mafunzo ya kijeshi vijana wake, Wasira akasema, “Ngoja wasonge na polisi wasonge, wataonana mahali.” Ingawa hakufafanua kauli hiyo, yaelekea alimaanisha kuwa watakutana na mkono wa dola.

 

Tamko la Chadema

Kamati Kuu ya Chadema ilikutana katika kikao cha dharura kuanzia tarehe 6-7 Julai mwaka katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali yakiwamo ya ulinzi na usalama wa viongozi na wanachama wake.

 

Taarifa iliyotolewa baadaye na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ilisema Kamati Kuu imesikitishwa na vitendo vya fujo walivyofanyiwa viongozi, wagombea pamoja na wanachama katika sehemu mbalimbali palipofanyika uchaguzi.

 

“Kamati Kuu imesikitshwa na kulaani vitendo hivyo vikiwamo vya watu kukatwa mapanga, kuchomwa visu na kubakwa kwa akina mama na vijana wahuni walioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi. Kamati Kuu imelaani vitendo hivyo vya kinyama vilivyofanywa mbele ya Jeshi la Polisi na wakuu wa wilaya.

 

“Ili kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, wanachama na viongozi wa Chadema, Kamati Kuu imeagiza kwamba kitengo cha ulinzi cha chama “Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade nchi nzima wanapewa mafunzo maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika makambi maalum katika mikoa yote.

 

“Kamati Kuu imejadili maandalizi ya Uchaguzi wa Madiwani katika kata nne (4) katika Jiji la Arusha. Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa juu mipango inayofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, na viongozi wengine wa CCM mkoani Arusha, katika kuhujumu zoezi la Uchaguzi kwa kuwatisha wapiga kura kwa kutumia polisi na vijana wa Green Guard siku ya uchaguzi.”

 

Msimamo wa Polisi

Punde baada ya Chadema kutoa taarifa hiyo, Jeshi la Polisi, kupitia Msemaji wake, Advera Senso, lilitoa taarifa ya kuionya Chadema.

 

“Kitendo cha chama chochote cha siasa ikiwamo Chadema kuanzisha kikundi cha kujihami ni kinyume cha sheria za nchi na endapo watafanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Jeshi la Polisi nchini limeanza uchunguzi na litachukua hatua kulingana na ushahidi utakaopatikana.

 

“Jeshi la Polisi litamshughulikia mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha sheria bila kujali wadhifa wake,” ilisema taarifa hiyo.

Please follow and like us:
Pin Share