Kampuni ‘hewa’ zakomba mamilioni

*CAG atakiwa aingie kazini mara moja

Kampuni tatu kati ya nane zilizozawadiwa zabuni tata za vifaa na huduma kwenye Mkutano wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue), zimebainika kuwa ni ‘hewa’.

Kwenye daftari la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kampuni hizo hazimo, licha ya kushinda zabuni za mamilioni ya shilingi.

 

Habari za uhakika kutoka Ikulu zinasema ufujaji fedha kwenye mkutano huo imeishtua Serikali, na kwamba Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapelekewa taarifa ya kuanza uchunguzi maalum mara moja.

 

Mkutano huo uliomalizika wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam, umegharimu Sh bilioni 8 zikiwa ni mbali na michango kutoka kampuni na mashirika mbalimbali.

 

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kampuni tata ambazo usajili wake hauko wazi ni True Colour Entertainment Group, iliyoshinda zabuni ya Sh milioni 50 kwa ajili ya kuandaa na kuonesha jarida linalohusu vivutio vya utalii vya Tanzania .

 

Nyingine ni Kampuni ya Wild Cat Publishing, iliyoshinda zabuni ya Sh 278,409,409 kwa ajili ya kuandaa machapisho mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, fedha, teknolojia, mawasiliano, usafirishaji, kilimo, ujenzi, afya, elimu na utalii.

 

Aidha, usiri umegubika kampuni nyingine ya Big Mama’s Woodworks, iliyoshinda zabuni ya Sh milioni 29.96 kwa ajili ya kutengeneza zawadi za vinyago 60 yenye urefu wa sentimita 15 na upana wa sentimita 12 kila kimoja. Pia ilitakiwa itengeneze vinyango vinne vyenye urefu wa sentimita 150 na upana wa sentimita 35.

 

“Haya makampuni hayajasajiliwa kwetu, kwa kawaida ukiingia tu katika mtandao unaandika jina la kampuni linakuja, sasa hapa nimehangaika sijayaona hayo makampuni,” alisema mmoja wa watumishi wa Brela.

 

Kukiwa na utata kwa walioshinda zabuni, habari zaidi zinaonesha kuwa wengi waliopata kazi hiyo ni wale walio karibu na watoto au viongozi waandamizi serikalini.

Wakati hayo yakiendelea, imebainika kuwa kulikuwapo harufu ya ufujaji mamilioni ya shilingi kwenye ukodishaji magari yaliyotumiwa kwenye ugeni huo.

 

Habari za uhakika zinaonesha kuwa uamuzi ulipitishwa ‘kisanii’ kwa kuamua kukodi magari binafsi, ilhali kulikuwapo magari mengi ya umma ambayo gharama pekee ingekuwa kwenye mafuta na kuwalipa madereva.

 

“Kilichofanyika ni kuhakikisha magari ya kampuni binafsi yanapata kazi hata kama magari ya Serikali yalikuwa mengi. Wahusika walilipwa fedha zao, lakini kwa makubaliano ya ‘ten per cent’, hata kwenye malipo walioanza kulipwa ni wenye magari ya kukodi ili wakishapata wawape ten per cent waliowapa kazi hiyo serikalini,” kimesema chanzo chetu.

 

Aidha, imebainika kuwa baadhi ya madereva walilipwa hadi Sh 700,000 lakini wengine walipunjwa kwa kulipwa Sh 350,000 kwa siku za mkutano. Kuna orodha ya magari ambayo hayakusafiri, lakini yakalipwa kwa kigezo kwamba tayari Serikali ilikuwa imeshaingia mkataba na wamiliki.

 

Ofisa aliyeshughulikia usafiri, Hassan Mabula, amekataa kuiambia JAMHURI kiwango cha fedha kilichotumika kwa kukodi magari.

 

“Siwezi kusema magari kiasi gani tulikodi na tulitumia kiasi gani kuwalipa. Siwezi kueleza hadi tutakapokaa maana tulikuwa wengi. Lazima nijiridhishe kwanza,” amesema Mabula na kuahidi kuweka hadharani kiasi cha fedha kilichotumika.

 

Katika mkutano huu, walialikwa marais 11 na wakuu wa nchi watano, hivyo kufanya idadi ya viongozi wakuu kufikia 16 waliotarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

 

Wahusika wakuu kwenye ulaji huu ni maofisa kadhaa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliokuwa waratibu wa ugeni huo. Katibu wa Bodi ya Zabuni katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Onesmo Suka, ni miongoni mwa maofisa wanaoelekezewa lawama, ingawa kuna habari kwamba amekuwapo wizarani hapo kwa miezi kadhaa.

 

Sokomoko la matumizi mabaya ya fedha

Uchunguzi umethibitisha kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, hakuridhishwa kabisa na namna zabuni zilivyotolewa.

 

Kwenye kikao cha mwisho, Sefue, kwa maandishi, alisema ingawa yeye ameshiriki katika Kamati ya Uendeshaji, hakubaliani na bajeti pamoja na mchanganuo wa zabuni ulivyokosa uwazi.

 

Amenukuliwa akisema ni jambo gumu kwake kukubaliana na ununuzi huo, kwa vile hapakuwapo mchanganuo wa kuthibitisha namna mamilioni ya shilingi yalivyotengwa kuwalipa wazabuni na bei za vifaa vilivyohitajika.

 

Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya kikao kilichofanyika Juni 17, vinasema Balozi Sefue aliweka wazi msimamo wake baada ya kuona taratibu za ununuzi zikiwa zimekiukwa, na kuwa baadhi ya vitu vilivyoorodheshwa vilikuwa ni “vichekesho”.

 

“Mimi sitaki nihusishwe na jambo hili, waliolifanya wanapaswa wenyewe wabebe msalaba huu, mchanganuo uletwe ili kuonesha nini kinanunuliwa kwa kiasi gani badala ya utaratibu huu wa kuorodhesha vitu na kuweka gharama,” alinukuliwa aking’aka Balozi Sefue.

 

Kampuni zilizopata zabuni

Kampuni ya Luma International Ltd ilipewa zabuni ya kusambaza vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 391.1. Baadhi ya vitu hivyo ni vipeperushi, bendera za Tanzania (kubwa na ndogo), suti kwa watu wa itifaki, sare kwa watu wa mapokezi, mabegi kwa wageni mashuhuri na wageni wa kawaida, na beji.

 

Kampuni ya Softel Trading Company Limited ilipewa zabuni ya Sh milioni 392.6 kusambaza picha za mapambo ukumbini, miavuli (1,500), chupa za kahawa (800), vikombe vya kahawa (800), kalamu za zawadi (2,000) na vishikio vya funguo (800).

 

Kampuni hiyo hiyo ilipewa zabuni nyingine ya Sh milioni 48.25 kwa ajili ya kufanya kazi za usanifu kwa kutumia kompyuta na uchapaji wa mabango madogo madogo.

 

Kana kwamba hiyo haitoshi, kampuni hiyo hiyo ya Softel Trading Company Ltd ilipewa zabuni ya thamani ya Sh milioni 254 kwa ajili ya kutengeneza mabango makubwa 40. Wakati mkutano ukiwa unafanyika Dar es Salaam, iliamuriwa kwamba mabango hayo yasambazwe katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar.

 

Kampuni ya Wild Cat Publishing ilishinda zabuni ya Sh 278,409,409 kwa ajili ya kuandaa machapisho 1,000 ya mkutano. Yalitakiwa yahusu masuala ya kisiasa, kiuchumi, fedha, teknolojia, mawasiliano, usafirishaji, kilimo, ujenzi, afya na elimu, utalii, n.k.

 

Kwenye masuala ya burudani, kampuni ya Prime Time Promotion ilijipatia zabuni ya Sh milioni 194.7.

 

Zabuni ya nane ilitolewa kwa kampuni ya Simply Computers (T) Ltd. Iligharimu Sh milioni 187.478. Ilitakiwa kusambaza kompyuta kubwa mbili, idadi kama hiyo kwa kompyuta za ukubwa wa kati na projekta nne.

 

Kampuni hiyo hiyo ya Simply, ilipata zabuni nyingine yenye thamani ya Sh milioni 210.198 kwa ajili ya kusambaza kompyuta tano za mezani, komputa mpakato (laptops 5), komputa mpakato za sekretariati na mkutano (14), mobile computing equipment (14), black and white printer (2), colour printer (2), kompyuta za mezani (nyingine 5), colour printer (nyingine 2) na flash disks (32).

Please follow and like us:
Pin Share