Mafanikio katika akili yangu (13)

Katika toleo lililopita sehemu ya kumi na mbili tuliishia katika aya isemayo: “Mimi ninaitwa Penteratha,” alisema. Profesa alipokuwa akiwatazama nyuso zao akagundua walikuwa na furaha halisi kutoka mioyoni mwao. Sasa endelea… 

Penteratha akiwa anaendelea kuzungumza na Noel, profesa alimuuliza: “Hivi ulifanyaje mpaka kuchapisha vitabu vyako?’’ Penteratha akamjibu profesa wake kwa ukweli na uhalisia: “Nilipeleka maombi yangu nikaambatanisha na vitabu vyangu kwa mfumo wa nakala laini.” 

“Sasa Noel utamsaidiaje, maana na yeye anaandika kitabu chake?” Profesa alikuwa akitaka Noel aweze kuchapa kitabu chake. Alihitaji kutumia njia tofauti ili kulifanikisha hilo. “Nafikiri profesa unipe muda niongee na wachapishaji wangu kisha nitakupa jibu,’’ alitoa ahadi hiyo Penteratha kisha akamuachia Noel mawasiliano yake. 

“Sawa Penteratha tutawasiliana,’’ alizungumza Noel kwa furaha akiwa mwenye kujawa tabasamu usoni mwake. Lifti ikaja, profesa akaingia katika lifti pamoja na Noel huku wakizungumza. “Noel, huyu binti anaandika riwaya sana pengine anaweza kuwa na msaada kwako, si unajua haya maisha!’’ Noel alielewa profesa alikuwa na nia ya dhati kwake. 

“Ni kweli profesa,’’ aliitikia Noel. “Katika maisha yako usije kumdharau mtu, utakuwa unatenda kosa,’’ profesa alitoa nasaha zake kwa kijana Noel.

Lifti ilichukua muda mfupi kushuka chini, profesa akatoka ndani ya lifti akiwa na Noel, safari ikaanza kuelekea ofisini kwa profesa. “Noel, twende ofisini kwanza unisubiri niingie kwenye kipindi halafu tuondoke,’’ alisema profesa huku akimtazama Noel. 

“Sawa profesa,’’ alijibu Noel. Noel ilibidi akubali kwa kuwa alikuwa mgeni katika mji wa Moscow, lakini pia profesa ndiye alikuwa kama baba yake na mwangalizi wake kwa kipindi ambacho Noel alikuwa nchini Urusi. 

Noel alipokuwa akitembea alikuwa akipishana na mabinti wa Kizungu waliokuwa wazuri kwa sura na hata maumbile yao. Kila aliyekuwa akipishana naye alikuwa na begi mgongoni au mkononi. Noel akawa akifikiria akilini mwake kuhusu walichobeba, kisha akagundua walikuwa wamebeba kompyuta zao. Fikra za Noel zilimtuma kwamba ni lazima itakuwa hivyo wala si kitu kingine, lakini pia watu hao walikuwa wenye haraka kuelekea sehemu walizokuwa wakienda.

***

Ni siku ambayo mkurugenzi wa redio ambayo alikuwa akifanyia kazi Noel na kufukuzwa akawa amewasili ofisini akiwa  mwenye furaha. Alipofika ofisini alikaa kwenye kiti chake kisha akachukua lile gazeti lililokuwa na makala aliyoandika Noel. Akachukua namba za simu zilizomo kwenye hiyo makala na kuzipiga akiamini Noel atakuwa akipatikana, nambari ya simu ikawa haipatikani, akabaki kutahamaki. 

“Mbona hapatikani!’’ alikuwa akifikiria huku akiwa ameshikilia simu yake ya mkononi, akiwa anawaza kwa nini Noel hapatikani. Mara yule meneja mzalishaji vipindi akaingia ofisini akamtazama mkurugenzi akiwa mwenye huzuni na mshangao.

“Noel hapatikani sijui tutampata vipi?’’ alikuwa akimueleza huku akiwa anamwangalia meneja mzalishaji vipindi. “Lakini kama hapatikani Fatuma, rafiki yake si yupo?’’ likawa wazo ambalo mkurugenzi aliona linafaa. “Ni kweli tumtafute Fatuma.’’ Wakaitafuta namba ya Fatuma ili kumpigia awasaidie katika jambo hilo. Wakapiga simu kwa Fatuma.

Fatuma muda huo alikuwa yumo njiani na Zawadi dada yake Noel wakitembea kuelekea ofisi za ofisa utamaduni wa mkoa ili kuangalia namna ya kusajili kampuni yao ya mitindo waliyokuwa wanataka kuianzisha.