Na Padre Dk. Faustin Kamugisha
Kujali ubora (excellence) ni sababu ya mafanikio. Kutia fora ni sababu ya mafanikio. Ni kufanya jambo liwe bora zaidi. “Hakuna aliyewahi kujutia kwa kutoa kitu kilicho bora zaidi,” alisema Sir George Stanley Halas (1895 – 1983). Huyu aliitwa “Bwana Kila Kitu” alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu, kocha na mmiliki wa Timu ya “Chicago Bears” ya Marekani.
Majuto ni mjukuu, lakini huwezi kujutia ubora. Sally Baucus Boydstun alisema, “Nilipokabiliana na changamoto ya mradi mpya kazini, nilitafuta ushauri wa meneja wetu namna ya kusonga mbele. Baada ya kupitia mapendekezo yake, nilimuuliza aniambie kanuni yake ya mafanikio. Alijibu kwa tabasamu: ‘Ninalolifanya, nalifanya vizuri sana. Na lile ambalo sifanyi vizuri, silifanyi kabisa.” Kufanya vizuri sana ni siri ya mafanikio. Mwanafunzi akipata maksi za juu mwalimu anamwandikia maneno: umefanya vizuri na si umesema vizuri.
Mwanamuziki wa kweli anajitahidi kufanya vizuri sana mbele ya watazamaji wake, hata kama wasikilizaji wanajua mambo ya muziki au hawajui. Kamati ya harambee ya kusaidia maskini ilimuomba Enrico Caruso aliyekuwa na sauti nyembamba, kuimba kwenye maonyesho ya muziki au burudani ambayo ilikuwa kwa ajili ya kuchangisha pesa ya kusaidia watu.
Mwenyekiti alisema, “Bwana Curuso hatutegemei mengi kutoka kwako kwa vile ili ni jambo la ukarimu. Jina lako tu litavuta umati wa watu unaweza kuimba nyimbo chache ambazo zinahitaji juhudi kidogo na utaalamu kidogo.” Curuso alijiweka sawa na kujibu: “Curuso hafanyi kazi ya kiwango cha chini kuliko anavyoweza kufanya vizuri sana.” Curuso alitilia mkazo ubora wa kazi na kazi kufanywa vizuri sana.
Andrew Carnegie mmiliki mkubwa wa viwanda na mfadhili mkubwa alitoa hotuba kwa wanafunzi waliokuwa wanahitimu huko Marekani. Alisema kuwa vijana wako katika makundi matatu: wale ambao hawafanyi kazi zao zote, wale ambao wanadai kufanya kazi zao kwa maneno, na wale ambao wanafanya kazi na kufanya kitu kidogo zaidi.
Alisema, “Ni kitu kidogo zaidi kinachoshinda. Fanya kazi yako na kazi kidogo zaidi, kesho itajishughulikia yenyewe.” Jambo kubwa hapa ni neno “zaidi.” Jambo unalolifanya livuke kiwango kwa sifa kama ukubwa, uzuri sana. Unachofanya kivuke kiwango kinachotakiwa. Unavyozalisha vivuke idadi inayohitajiwa.
“Zaidi” ionekane katika kila kitu maishani. Usiwepo tu, ishi. Usisikie tu sikiliza. Usitazame tu, ona. Usisikilize tu elewa. Usifikiri tu, tafakari. Usitembee tu, talii. Usile tu, furahia chakula. Usipange tu tekeleza. Usinene tu bali neno litwae mwili.
 
Hata usipokuwa Mama Teresa wa Calcutta, kwa mazuri unayofanya wewe kuwa zaidi. Kuwa Damian zaidi. Kuwa Jacinta zaidi. Kuwa Nassor zaidi. Kuwa Yakobo zaidi. Kuwa Abu-Bakr zaidi. Kuwa Aishati zaidi. Katika uwanja wa kompyuta hata usipokuwa Steve Jobs bali kuwa wewe zaidi.  “Kila kazi ni kujichora kwa mtu aliyeifanya. Weka sahihi yako kwenye kazi yako kwa ubora,” alisema Jessica Guidobono. Kila kazi unayoifanya inabeba jina lako.
Tunafanyaje mambo vizuri zaidi? Kwa kawaida tunajifunza kusimama kwa kusimama. Tunajifunza kutembea kwa kutembea. Tunajifunza kukimbia kwa kukimbia. Tunajifunza kufanya vizuri kwa kufanya vizuri. Rudia rudia kufanya vizuri zaidi mpaka kuwe desturi. Ukweli huu ulibainishwa na mwanafalsafa wa Kigiriki Aristotle:
“Tunakuwa kile tunachofanya kwa kurudiarudia, ubora, si tendo bali desturi.” Confucius (551 KK – 479 KK) wa China alisema, “Nia ya kushinda, shauku ya mafanikio, hamu kubwa ya kufikia uwezo wako wa juu wa lile unaloweza kufanya… hizi ni funguo za kufungua mlango wa mtu binafsi kufanya vizuri zaidi.”
4918 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!