Na Pd. Dk. Faustin Kamugisha

Mtandao chanya wa watu ni sababu ya mafanikio. Huwezi kupiga makofi kwa mkono mmoja. “Ukitaka kwenda kwa haraka sana, nenda peke yako. Ukitaka kwenda mbali, nenda pamoja na wengine.” (Methali ya Kiafrika).
Hawa wanaotajwa kama ni wengine ni wale ambao wana mtazamo chanya. Ni wale ambao wanapiga makasia mtumbwi wako wa mafanikio ufike ufukweni. Ni wale ambao hawaogopeshwi na kufanikiwa kwako. Hakuna mtu aliye na kila kipaji.
Kila kipaji kina thamani yake. “Kama mwili wote ungekuwa jicho, ungewezaje kusikia? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, ungewezaje kunusa?” aliuliza Paulo wa Tarsus.
Baadhi ya wanamuziki wanaweza kuporomoka si kwa sababu kuimba kwao kumepoteza mvuto, bali timu waliyonayo haijatoa ushirikiano mzuri. Gayton MacKenzie analiona hilo katika kitabu chake: ‘A Hustler’s Bible.’
“Nimeona wasanii wakubwa sana wakishuka si kwa sababu imba yao imekuwa mbaya sana, bali kwa sababu timu inayowaunga mkono haiendani na kipaji cha msanii. Mara ya kwanza tunapofanikiwa mwelekeo ni kujizungushia na wale ambao wamekuwa karibu nasi njia yote. Kwa kufanya hivyo tunaweza kutoa nafasi kwa ambao hawana uzoefu. Tunafikiri tunarudisha fadhila lakini tunalipa gharama ya kuanguka kwetu.” Watumie watu wenye ujuzi hata kama si rafiki zako. “Ukiishi mtoni fanya urafiki na mamba.” (Ni methali ya India).
“Tunazaliwa kwa ajili ya ushirikiano, kama ilivyo miguu, mikono, kope na taya la juu na chini,” alisema Marcus Aurelius Antoninus.
Mfumo wa mtandao wa mwili ni picha tosha ya mtandao chanya. Mwili wote ungekuwa pua jicho lingekuwa wapi? Pua inanusa, macho yanatazama, ngozi inahisi, ulimi unaonja, miguu inatembea, mikono inashika, mate yanalainisha. Moyo unasukuma damu, kutaja mifano michache.
Macho yanatazama. Macho yanaona. Unahitaji jicho la tatu. Macho yanayotazama ni mengi. Macho yanayoona ni machache. Penye miti hakuna wajenzi. Kuna macho yanatazama, lakini hayaoni. Unamhitaji mtambuzi. Unahitaji mtu atakayemaizi na kuona lile ambalo hulioni.
Unahitaji mtu atakayesoma lile ambalo lipo katikati ya mistari ambalo halionekani. Unahitaji mtu mwenye maono. Unahitaji mtu wa kuona mbele na kwa upeo. Katika maandiko matakatifu mtumishi wa Elisha aliona tu jeshi kubwa la wanadamu lililowazunguka, lakini Elisha aliona kwa dhahiri jeshi la mbinguni (2 Wafalme 6: 15-17).
Mikono inatoa, unahitaji mfadhili, humchagui mfadhili, mfadhili anakuchagua. Mungu ametupa mikono miwili: mmoja wa kutoa na mwingine wa kupokea. Kama unatoa unastahili kupokea. “Anayenipa ananifundisha kutoa,” ndivyo isemavyo methali ya Kidenishi (Denmark).
Kila mtu anamhitaji mwingine. Bwana Yesu Kristu alikuwa tayari kupokea marashi kutoka kwa mwanamke. Bwana Yesu alikuwa tayari kupokea mwana punda kutoka kwa tajiri rafiki yake. Bwana Yesu alipokea mtumbwi kutoka kwa Simoni Petro. Hao walikuwa wafadhili. Unaweza kusema fulani ana kila kitu, lakini ukichunguza vizuri kuna kitu anachohitaji. Wafadhili kumbuka kuwashukuru, washikilie kwa mikono miwili.
Ulimi unafisha na ulimi unahuisha. Unahitaji watu wa kukutia moyo au kukuhuisha. “Hakuna kitu kizuri zaidi kama kutiwa moyo na rafiki mwema,” alisema Katherine Butler Hathway. Kila moyo una njaa, njaa ya kutiwa moyo. Kuwa karibu sana na watu wanaokutia moyo.
Midomo inalaani, midomo inabariki, midomo inaombea. Unahitaji waombezi. Sala za maombezi ni upendo uliopiga magoti. “Usiwaweke watu chini labda kama ni kwenye orodha yako ya sala,” alisema Stan Michalski. Paulo wa Tarsus alisisitiza hilo: “Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua na sala na maombezi na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote.”
Mikono inashika, unahitaji watu “wakupe” mikono. Unahitaji watu wakupe ushirikiano. “Kukutana pamoja ni mwanzo; kuendelea kuwa pamoja ni maendeleo; kufanya kazi pamoja ni mafanikio,” alisema Henry Ford. Unahitaji msherekeaji. Unahitaji mtetezi. Unahitaji mratibu. Unahitaji mwanamtandao, yaani mtu wa kukuunganisha na watu wengine.

Mwisho

By Jamhuri