NA ALEX KAZENGA

DAR ES SALAAM

Wananchi wa Kata ya Makangarawe, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wameulalamikia ujenzi wa barabara za mitaa unaofanywa kwa kiwango cha lami katika mitaa hiyo wakidai kuharibu makazi yao.
Ujenzi huo umeanza kutekelezwa hivi karibuni chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), mradi huo unafanyika pasipo kuwahamisha wananchi walio karibu.
Kutokana na ujenzi huo wa barabara ambao unahusisha mitambo mizito ya kushindilia, imesababisha nyumba kadhaa kupata nyufa huku nyingine zikibomoka kuta zake kutokana na mitikisiko.
Manispaa ya Temeke ndiye msimamizi wa mradi huo, huku akituhumiwa kuhujumu fedha za mradi.
Wananchi walioguswa na mradi huo wameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa hujuma hiyo inatekelezwa na viongozi wa manispaa hiyo kwa kuruhusu ujenzi wa barabara hizo kutekelezwa katikati ya makazi ya watu.
Wamesema kutokana na ujenzi ambao umeanza kutekelezwa hawaamini kama vitu hivyo vitawekwa, kwani baadhi ya kuta za nyumba zao zimegeuka kuwa mipaka ya barabara hizo.
Baadhi ya wakazi wa kata hiyo wameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa baadhi ya viongozi wanaoratibu mradi huo wamekuwa wakimueleza mkandarasi kulipua ujenzi huo wakidhani wananchi hawawezi kuhoji juu ya ujenzi huo.
“Nilimsikia ofisa mmoja wakati amekuja kukagua huu ujenzi akimweleza Mchina kwa Kiingereza kwamba; hizi barabara zijengwe kwa kiwango cha kawaida ili tuwahi muda, hakuna kiongozi atakayezitumia hizi barabara,” amesema mmoja wa wakazi hao.
Mratibu wa mradi wa DMDP katika Manispaa ya Temeke, Edward Simon, amesema wananchi wanaolalamikia ujenzi wa barabara hizo huo si uzalendo.
Amewatahadharisha wananchi hao kuwa suala lolote la maendeleo limebeba sura mbili, ambazo ni sura ya faida na hasara.
Simon amesema wananchi wa Makangarawe wanatakiwa kuunga mkono ujenzi huo huku wakijiandaa kukabiliana na changamoto ya uharibifu utakaotokana na ujenzi wa barabara.
“Sisi tunajua muundo wa barabara zetu utakuwa na mitaro na yapo maeneo mengine hayatakuwa na mitaro na mengine kuwa nayo upande mmoja. Kuna sehemu nyingine mitaro tutaiweka chini ya ardhi (underground).
“Si lazima watu kuhamishwa katika makazi yao ili kupisha ujenzi wa barabara, sisi tutajenga kwa umakini kwani tunajenga katikati ya makazi ya watu,” amesema Simon.
Ametoa mfano kuwa haiingii akilini barabara yenye urefu wa chini ya mita 600 kugharimu Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya kulipa fidia wakati ujenzi wake haugharimu hata nusu ya fedha iliyotumika kulipa fidia.
Katika mradi wa DMDP, jumla ya dola za Marekani bilioni 19.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali katika Kata ya Makangarawe huku dola za Marekani takriban bilioni 4 zikielekezwa kwenye ujenzi wa barabara za mitaa ya kata hiyo.
Barabara hizo ni Abiola yenye urefu wa km 0.9 ambayo itajengwa kwa gharama ya Sh milioni 818, Sheraton yenye urefu wa km 0.97 ambayo inajengwa kwa gharama ya Sh milioni 961 na barabara ya Iramba yenye urefu wa km 1.7 ikijengwa kwa Sh bilioni 1.3.
Barabara nyingine ni Gonja yenye urefu wa km 0.8 ambayo inajengwa kwa gharama ya Sh milioni 659 pamoja na Kwa Mwenyekiti yenye urefu wa km 0.33 ambayo itajengwa kwa gharama ya Sh milioni 35.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Baraka Mwasaka, amesema mradi huo unatekelezwa katika barabara ambazo hazihitaji ulipaji mkubwa wa fidia.
Amesema hali hiyo imetokana na ukata unaoikabili Manispaa ya Temeke, halmashauri hiyo haiwezi kupata fedha za kuwalipa fidia watu watakaoathirika.
Ofisa Habari wa Manispaa ya Temeke, Lynn Chawal, amesema ujenzi huo bado uko kwenye hatua za awali lakini utekelezaji wake bado haujafanyiwa upembuzi yakinifu, ikiwa ni pamoja na kuyabaini maeneo ambayo yanahitaji ulipaji wa fidia.
Amesema fedha ambazo zimetolewa na Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kufadhili mradi wa DMDP zitatumika kutekeleza miradi lakini suala la kulipa fidia linasimamiwa na manispaa.
“Wananchi wa Makangarawe wasifikirie tuna mradi katika kata yao peke yake, tuna miradi mingi inaendelea katika Manispaa ya Temeke, kule shughuli haijaanza rasmi, tukianza kazi wao wenyewe watajionea kwa macho yao,” amesema Chawal.
Kampuni inayofanya ujenzi wa barabara za mitaa ya kata hiyo ni MHJANGFIGEO-Engineer (group) Corporation, kutoka China. Kampuni hiyo imesaini mkataba wa kujenga barabara hizo ndani ya miezi 15 kuanzia Julai mwaka huu.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share