KHALIF MWENYEHERI NA CATHERINE LUCAS, TUDARCO

Jeshi la Polisi nchini limekamata silaha 187 katika kipindi cha Juni mwaka jana hadi Septemba mwaka huu, huku vitendo vya mauaji vikipungua kutoka 1,538 na kufikia 1,311 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Jeshi la Polisi, silaha hizo zilizokamatwa katika maeneo mbalimbali nchini zilikuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria na kutumika katika matukio ya uhalifu ikiwa ni asilimia 8.7.
Akizungumza na JAMHURI, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa, amesema kukamatwa kwa silaha hizo ni jitihada zilizofanywa na jeshi hilo kwa ushirikiano na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
ACP Mwakalukwa amesema pia mauaji yamepungua kwa asilimia 14.8, ikiwa ni tofauti ya watu 227 waliouawa mwaka jana ikilinganishwa na matukio kama hayo yaliyofikia idadi ya vifo vya watu 1,538.
Ametaja matukio mengine ya uhalifu yaliyopungua mwaka huu kuwa ni ubakaji ambao umepungua kwa asilimia 8.1 kutoka matukio 3,897 mwaka jana hadi kufikia matukio 3,583 mwaka huu, kulawiti kumepungua kwa asilimia 4.7 kutoka matukio 574 hadi 547 mwaka huu.
Matukio mengine ni wizi wa watoto ambao umepungua kwa asilimia 6.3 kutoka matukio 63 hadi 59, utupaji wa watoto wachanga umepungua kwa asilimia 10.8 ikilinganishwa na mwaka jana ambako kulikuwa na matukio 65 hadi 58 mwaka huu, unajisi umepungua kwa asilimia 33.3, kutoka matukio 15 hadi 10.
Matukio mengine ni biashara ya usafirishaji wa binadamu ambao umepungua kwa asilimia 42 kutoka matukio 19 katika kipindi cha mwaka jana hadi 11 mwaka huu, wahamiaji haramu ambao wameongezeka kwa asilimia 7.7 kutoka matukio 558 mwaka jana hadi 601 mwaka huu.
Amesema matukio ya ajali za barabarani yamepungua kwa asilimia 28 mwaka huu, mwaka jana jumla ya ajali za barabarani 3,090 zilitokea ikilinganishwa na mwaka huu matukio ya ajali 2,220.
Kutokana na ajali hizo 1,089 zilisababisha vifo mwaka jana, ambapo watu 1,308 walifariki dunia, mwaka huu matukio ya ajali yaliyosababisha vifo ni 785 na idadi ya vifo ni 1,051 na idadi ya majeruhi imepungua kwa asilimia 21.3, kutoka watu 2,976 hadi 2,341.
Mwakalukwa amesema jeshi hilo halina uwezo wa kutoa ulinzi kwa kila mwananchi kutokana na idadi ndogo ya askari waliopo, hivyo limeanzisha vikundi vya kujilinda ikiwemo sungusungu na kutoa mafunzo kwa kutumia ulinzi wa wanyama kama mbwa.
“Kwa upande wa jamii za wafugaji tunakusudia kuanzisha mafunzo maalumu kupitia wanyama kazi ili kulinda vitendo vya wizi wa mifugo yao,” amesema Mwakalukwa.
Msemaji huyo wa Jeshi la Polisi amewataka wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mikononi kwa kuwapiga watu wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu, badala ya kuwapeleka katika vituo vya Polisi ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mwakalukwa amewaonya sungusungu kuacha kuwapiga watu wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu, badala yake wawafikishe katika vituo vya Polisi kwa ajili ya taratibu za kuwafikisha mahakamani ili wakabiliane na mkono wa sheria.
Amesema Jeshi la Polisi halina huruma na mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya ujambazi au uhalifu wa aina yoyote na kwamba huruma yao iko kwa wananchi ambao wameathiriwa na uhalifu, ikiwemo kuibiwa mali zao.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share