DAR ES SALAAM

NA JUMA SALUM

Kijiografia, Mafia ni kisiwa kilichoko Bahari ya Hindi, kilometa 120 kusini – mashariki mwa Jiji la Dar es Salaam na kilometa 20 mwambao wa pwani ya Wilaya ya Rufiji.
Katika hali ya kushangaza, eneo la katikati la kisiwa hiki kidogo chenye ukubwa unaokadiriwa kuwa karibu nusu ya Kisiwa cha Unguja, wanapatikana wanyamapori aina ya viboko. Kwa kawaida viboko ambao kisayansi hutambulika kama hippopotamus amphibious, huishi kwenye maji ya mito, maziwa na maeneo oevu. Kiboko ana uwezo wa kutembea nchi kavu nyakati za usiku mbali na maji kwa ajili ya malisho ambayo ni majani.
Kiboko dume anaweza kufikia uzito wa tani 4.5 ambazo zinamfanya kuwa mnyama wa tatu kwa ukubwa kwa wanyama wa nchi kavu baada ya tembo na faru weupe.
Kwa kawaida viboko hupatikana maeneo mengi kwa kipindi cha mwaka mzima Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa Tanzania viboko wanapatikana kwa wingi maeneo tofauti tofauti yenye mito na mabwawa kama vile Mto Rufiji, Mto Wami na maeneo ya hifadhi kama Serengeti na Katavi.
Uwepo wa viboko kwenye Kisiwa cha Mafia unakifanya kisiwa hiki kuwa cha kipekee katika Bahari ya Hindi.
Wengi huuliza juu ya asili yao. Wengine wanahoji, je, waliwezaje kuvuka bahari yenye maji chumvi na kufika Mafia?
Makala hii inajaribu kuelezea uwepo wa viboko wilayani Mafia pamoja na hatari zinazowakabili na kutishia uwepo wao kisiwani humo.

Uwepo wa viboko Mafia

Kwa wageni kutoka Ulaya, mwanasayansi na mtafiti wa Kijerumani aliyeitwa Bauman alikuwa wa kwanza kurekodi uwepo wa viboko Mafia mwaka 1896. Viboko wameendelea kuwepo hadi leo wakipatikana katikati ya Kisiwa cha Mafia katika vijiji vya Ndagoni, Chunguruma, Baleni na Kirongwe. Maeneo mengi katika vijiji hivi ni ardhi oevu (wetlands) zinazojumuisha mabwawa na mito isiyokauka mwaka mzima.
Kwa sasa walau unaweza kuwaona viboko katika Bwawa la Kangage linalopatikana Ndagoni Mdodoni, ambalo pia ndiyo mahala ambako watalii hufika kushuhudia uwepo wa viboko kisiwani Mafia. Mbali na Kangage, Chunguruma, Ulungwi na Tanda Nnubi ni mahali ambako pia unaweza kuona viboko.

Asili ya viboko hawa

Je, wapi hasa walikotoka viboko hawa? Labda hili ndilo swali linaloulizwa na watalii wengi. Wengi hudhani wametoka Mto Rufiji ambao upo mkabala na Kisiwa cha Mafia na humwaga maji katika Bahari ya Hindi. Wengine hudhani wamefika Mafia baada ya kusukumwa na mafuriko yaliyotokea Mto Rufiji miaka mingi iliyopita.
Wanaolielezea hili wameendelea kuliamini tu bila kueleza kwa kina ni kwa jinsi gani waliogelea kwenye maji chumvi umbali wa kilometa zaidi ya 20 ambako kiikolojia si maji yake. Ni wazi kabisa jambo hilo ni vigumu kuaminika.

Je, wametoka wapi?

Kulielezea jambo hili ni lazima tuelewe japo kwa muhtasari namna visiwa kama Mafia vinavyotokea.
Kulingana na utafiti wa ‘Continental island formation and the archaeology of defaunation on Zanzibar, Eastern Africa’ uliofanywa na Mary Prendergast na wenzake mwaka 2016, visiwa vya Mafia, Zanzibar na Pemba kiasili ni baravisiwa au continental islands, kwa maana visiwa hivi vimetokana na kumeguka kwa sehemu ya bara (nchi kavu) kisha hicho kipande kilichomeguka huzungukwa na maji na hatimaye kuwa kisiwa.

Hili linafanyikaje?

Katika kipindi ambacho wataalamu wa jiolojia hukitambua kama Pleistocene, yaani kipindi kilichoanza miaka milioni 2.6 iliyopita mpaka miaka 11,700 iliyopita; kina cha maji ya bahari kiliongezeka katika kiwango ambacho maeneo mengi ya mwambao wa pwani yalimegwa na maji na kupata vipande vikubwa vilivyokuja kuzungukwa na bahari na hatimaye kuwa visiwa.
Visiwa vilivyotoka kwa mtindo huu hutambulika kama continental islands. Baadhi ya visiwa hivyo ni visiwa vya Uingereza, Indonesia na Tasmania. Kwa upande wa Afrika Mashariki, continental islands ni kama Lamu (Kenya); Unguja, Pemba na Mafia.
Mchakato mzima wa kipande cha nchi kavu kuwa kisiwa si jambo la siku, wiki, mwaka au miaka michache. Huchukua maelfu ya miaka kukamilika kwake. Hivyo, kulingana na Prendergast, Kisiwa cha Mafia kilitengenezwa kuanzia kipindi cha Pleistocene na mchakato wake ulikamilika kati ya miaka 9,000 na 3,000 iliyopita.
Hivyo, tunaweza kujenga hoja kuwa uwepo wa viboko kisiwani Mafia ulifanyika kipindi hicho ambacho kisiwa kinatengenezwa.
Hapo mwanzo dunia yote ilikuwa bara moja lililoitwa Pangea. Wanyama walitapakaa kila mahali, na lilipogawanyika kuwa mabara saba wanyama nao wakajikuta wakitenganishwa katika vipande tofauti vya mabara kulingana na mahali walipokuwa.
Kwa mfano huo, baada ya Pangea kupasuka, baadhi ya tembo wakajikuta Bara la Asia na wengine wakawa Bara la Afrika.
Vivyo hivyo, wakati kipande cha ardhi kinameguka kutoka bara (Rufiji?) na kutengeneza Kisiwa cha Mafia bila shaka baadhi ya wanyama wakiwamo viboko walibaki katika kipande cha ardhi kilichomeguka kisha kuwa Kisiwa cha Mafia. Kwa maoni yangu hii inaweza kuwa nadharia muhimu inayoelezea asili ya wanyama wengine wanaopatika katika Kisiwa cha Mafia kama vile nguruwe (bush pigs), sengi (elephant shrews) Mafia wanajulikana kama ndoro, kima (blue monkeys) na blue duikers (chesi).
Ushahidi wa jambo hili unaweza kuwa ukweli kwamba Kisiwa cha Mafia kipo mkabala na Mto Rufiji uliopo wilayani Rufiji – eneo lenye viboko wengi. Eneo la katikati ya Kisiwa cha Mafia mahali penye ardhi oevu kunakopatikana mabwawa na mito ya viboko kwa kiasi fulani jiografia yake inafanana na eneo mkabala lenye ardhi oevu na Mto Rufiji.
Kuithibisha nadharia hii ni jambo linalohitaji utafiti wa kina, wa kisayansi na utakaokuja na majibu sahihi ya jambo hili ili kuondoa utata.

Viboko hatarini kutoweka

Hakuna sensa au taarifa rasmi inayotaja idadi ya viboko walioko Mafia. Mwaka 2013 wanafunzi wa kujitolea kutoka Uingereza walifanya sensa isiyo rasmi na walikadiria kuwa viboko kisiwani Mafia ni kati ya 10 hadi 20.
Kwa mujibu wa wazee wa Mafia, wakiwamo wazee Kirobo na Ali Maulid, miaka ya 1970 hadi 1990 Mafia ilikuwa na mamia ya viboko katika vijiji vya Ndagoni, Chunguruma na Kirongwe. Endapo hali hii itaendelea, miezi au miaka michache ijayo Mafia haitakuwa na kiboko.
Wengi wameuawa na wananchi wenyewe au kwa amri ya Idara ya Maliasili – Mafia, baada ya kuvamia mashamba ya mpunga. Mwaka huu (2018) kiboko aliuawa baada ya kumvamia na kumuua mpita njia katika Kijiji cha Chunguruma. Pia kuna matukio kadhaa ya watoto wa viboko kugongwa na magari, hasa nyakati za usiku.
Mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha kukosekana kwa mvua za uhakika, hivyo kusababisha kukauka kwa mito na mabwawa ambayo ndiyo makazi ya viboko.

Hitimisho

Kwa ujumla viboko wana umuhimu mkubwa wa kimazingira hasa katika mabwawa wanamoishi na maeneo ya kuzunguka makazi yao. Takataka zitokanazo na viboko na kinyesi chao ni lishe tosha kwa viumbe wa majini kama samaki na ni mbolea kwa mimea.
Mbali na umuhimu huo wa kimazingira, viboko ni kivutio kwa watalii ambao huja kuwaona. Ujio wao huongeza pato la mtu mmoja mmoja na serikali.
Endapo hatua mahususi hazikuchukuliwa, viboko wa Mafia watatoweka katika uso wa kisiwa hicho. Natoa mwito kwa serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, wananchi wa Mafia, wadau wa uhifadhi na umma kwa jumla kutambua umuhimu wa viboko wa Mafia na kuchukua hatua za kuwahifadhi ili kuhakikisha wanaendelea kuwapo.

Mwandishi wa makala hii, Juma Salum, ni msomi wa masuala ya maliasili aliyehitimu katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka. Anapatikana kwa simu: 0657 972723

..tamati….

Please follow and like us:
Pin Share