Na Alex Kazenga

Dar es Salaam

Wafanyakazi zaidi ya 30 wa Kituo cha Mafunzo ya Kompyuta (UCC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamo hatarini kupoteza kazi baada ya kituo hicho na matawi yake yote nchini kutakiwa kufungwa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni mbinu zinazoratibiwa na menejimenti kukiua kituo hicho.
Anayetuhumiwa kufanya mbinu hizo ni Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk. Ellinami Minja, kwa manufaa binafsi pamoja na baadhi ya watu walio karibu naye.
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la JAMHURI umebaini baadhi ya matawi ya kituo hicho tayari yamefungwa likiwemo Tawi la Mbezi Beach na City Center, yote ya jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kufungwa kwa matawi hayo, vitendea kazi vyote vimehamishiwa makao makuu ya kituo hicho (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) ambako vimetelekezwa na vingine kuharibiwa kwa makusudi.
Kuharibiwa kwa vitendea kazi hivyo ambavyo ni pamoja na kompyuta, viti, viyoyozi (AC), vifaa vya kuzimia moto na meza, ambavyo vimegharimu mamilioni ya shilingi za walipa kodi, inaelezwa kuwa ni mkakati mahususi ulioandaliwa na Dk. Minja ili kuvinufaisha vyuo binafsi vinavyotoa mafunzo ya kompyuta vinavyomilikiwa na baadhi ya walimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Hata hivyo mkakati huo unaofanywa kwa usiri mkubwa tayari unatajwa kuwakosesha masomo ya kompyuta zaidi ya wanafunzi 300 waliokuwa wakisoma katika matawi hayo.
Wakati mkakati huo haramu ukifanyika, athari zake zitawagusa zaidi ya wafanyakazi 30 wakiwemo walimu, wahasibu na watumishi wengine wa kada mbalimbali ambao tayari menejimenti imetishia kuwafuta kazi.
Kigezo kinachotumiwa na menejimenti hiyo kufuta kitengo hicho ni kwamba mafunzo ya kompyuta kwa sasa yanatolewa hadi shule za msingi, hivyo kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hayana tija yoyote na badala yake yatakiingiza chuo katika hasara.
Sababu nyingine ya kufunga matawi hayo ni kile kinachoelezwa kuwa ni agizo la Rais John Magufuli kwamba taasisi zote za umma zisiendeshe shughuli zake katika majengo ya watu binafsi nje ya maeneo yanayomilikiwa na kituo hicho.
Baadhi ya wafanyakazi wa kituo hicho wameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa menejimenti imekuwa ikitoa sababu za uongo kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa kituo hicho kinajiendesha kwa hasara wakati kilikuwa kinapata wanafunzi wengi wanaolipa ada kwa uaminifu.
Wafanyakazi hao ambao hawakutaka majina yao kuandikwa gazetini wamesema kuwa menejimenti ya kituo hicho imehusika pia kuwagawa katika makundi mawili ambayo ni wale ambao si wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (THTU) na waliojiunga na chama hicho.
“Ukiwa mwanachama unatishiwa kufukuzwa kazi, lakini wale ambao si wanachama wanapandishwa madaraja na kupata fursa ya kujiendeleza kielimu.
“Ubaguzi huu ni kinyume cha sheria za kazi, na umeibua mgogoro mkubwa kwa kuwaita wale wanaokubaliana na mkakati huo kuwa huyu ni mwenzetu (aliye mwanachama) na yule si mwenzetu (asiyekuwa mwanachama),” anasema mmoja wa wafanyakazi hao.
JAMHURI limefahamishwa kwamba menejimenti inawatungia tuhuma za uongo wafanyakazi wake na kuibua vigezo vya uongo, lengo likiwa ni kutafuta sababu za kuwafukuza na wengine kupunguzwa kwenye kituo hicho.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (THTU), Salifius Mligo, ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba ni kweli menejimenti ya kituo hicho inanyanyasa wafanyakazi wake, hasa walio wanachama na kwamba imetoa tangazo la kupunguza wafanyakazi wake.
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba migogoro katika kituo hicho imedumu kwa miaka miwili, migogoro hiyo inachangiwa na uongozi wa Dk. Minja na Makamu wake, Dk. Elias Mturi, ambao wamekuwa wakiendesha kituo hicho jinsi wanavyotaka bila kuzingatia maadili wala sheria.
Mligo anasema kutokana na tangazo hilo la kufukuza wafanyakazi, Chama cha Wafanyakazi chuoni hapo (THTU) kimeandika barua ya kuomba ufafanuzi kwa vielelezo kwanini menejimenti inataka kuwafukuza wafanyakazi.
“Juzi tumekaa kikao, tulimwambia kama anasema anataka kubadilisha muundo kwa kuyafunga matawi ya Arusha, Mbeya na Mwanza kwa sababu yanaleta hasara, atuonyeshe ni wapi yanaleta hasara, lakini ameshindwa kuonyesha vielelezo,” anasema Mligo.
Anasema utafiti uliofanywa na chama hicho kuhusu kufungwa kwa matawi ya Mbezi Beach na City Center pamoja na yale ya Mbeya, Mwanza na Arusha kimegundua hakuna hasara yoyote, hali inayoonyesha utofauti katika maelezo yanayotolewa na menejimenti.
Ubaguzi unaotajwa kuendelea kushika kasi katika kituo hicho ambapo wanachama wa Chama cha Wafanyakazi (THTU) hubaguliwa na menejimenti, unatokana na Dk. Minja kuhisi kwamba chama hicho kinaingilia masilahi yake, hivyo ili kuepuka kusumbuliwa na chama hicho huwalazimisha wafanyakazi kujitoa kwenye chama ama kuacha kazi.
“UCC ni mali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho ni mali ya serikali, kwa hiyo kwa namna moja au nyingine watumishi wa kituo hiki ni watumishi wa umma, sisi watumishi wa umma tuna miiko na maadili yetu.
“Na mali ya umma si kitu cha siri, kwa hiyo wafanyakazi walio wanachama wa THTU wanapotaka kufanyiwa udhalimu wanakuja kulalamika, sisi tunachukua hatua.
“Kuna kesi zililetwa zikihusu yale ambayo Dk. Minja anawafanyia wafanyakazi wake, kuna waliokuwa wanachama wetu tumewatetea na kushinda kesi na kurudi kazini,” anasema Mligo.
Anasema hata Naibu Mkurugenzi, Dk. Elias Mturi, anashiriki kuwanyanyasa wafanyakazi ambavyo anashinikiza wafanyakazi walio wanachama wa THTU kufukuzwa kazi kwa sababu anawatuhumu kutozalisha (non-performers).
Hata hivyo mwenyekiti huyo amehoji kwanini kituo hicho kinasema hakina fedha za kujiendesha wakati jamii ya Watanzania kwa asilimia kubwa ina imani na mafunzo yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na inatamani watoto wao kupata mafunzo katika kituo hicho.
Mligo anasema sababu za kukosa wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya kompyuta katika kituo hicho ni za uongo, kwani jina na sifa za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vinakibeba kituo hicho.
Anasema kama menejimenti imeshindwa kuendesha kituo hicho kulingana na mahitaji ya soko yaliyopo kwa sasa viongozi wanatakiwa kujiuzulu ili wengine wenye ujuzi wakiongoze kituo hicho kuliko kuwasumbua wafanyakazi.
“Dk. Minja amekuwa na tabia ya kuwafukuza wafanyakazi anavyotaka yeye, sisi tukimuuliza anaona kama tunamnyima uhuru.
“Kuna kesi ya wafanyakazi walipata tenda ya kukata viingilio katika maonyesho ya Sabasaba ikapatikana hasara, yeye alikuja akavurugavuruga bila kuhoji chanzo cha hasara hiyo, huku akisema wameiba, lakini ukweli wa kile kilichojitokeza ni kwamba mashine ilikuwa mbovu, lakini yeye akalazimisha kuwa wafanyakazi wameiba,” anasema Mligo.
Hata hivyo Dk. Minja anatuhumiwa kuwabagua wanawake katika kituo hicho, imebainika kuwa wapo walionyimwa fursa za kwenda masomoni na wengine kunyimwa haki ya kupanda vyeo kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe.
“Yupo aliyeomba kwenda masomoni akamruhusu kwa kumpa dhamana ya barua, lakini ulipofika muda wa kwenda alimnyima kibali, hata alipoomba kupewa likizo bila malipo ili aweze kwenda masomoni napo pia alikataa kwamba hana vigezo,” anasema Mligo.
JAMHURI limemtafuta Dk. Minja kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa tuhuma zinazomhusu, hata hivyo alitoa maelekezo kwamba apatiwe barua yenye maswali na kutumiwa kwa njia ya barua pepe (e-mail) na kwa mkono, huku ikiwa imesainiwa.
Maelekezo hayo yalifuatwa, Gazeti la JAMHURI liliandika barua na kuifikisha ofisini kwake Agosti 27, lakini cha kushangaza tangu barua hiyo ifike ofisini kwake ushirikiano ulipungua, kwani hakusema ni lini anaweza kukutana na mwandishi wa Gazeti la JAMHURI ili kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo.
JAMHURI limefika Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, kwa lengo la kupata ufafanuzi wa tuhuma hizo, ambaye ameelekeza ofisi ya mawasiliano ya chuo hicho itoe ufafanuzi kwa niaba yake.
Ofisa Habari wa chuo hicho, Jackson Isdory, ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba tuhuma hizo zimefika kwenye uongozi wa chuo na kwamba imeundwa tume kwa ajili ya kufanya uchunguzi, huku akiahidi kwamba baada ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za UCC na Dk. Minja kukamilika uongozi wa chuo utatoa taarifa kwa umma.

Mwisho

By Jamhuri