Nilifurahi mno Jumatano ya Septemba 5, mwaka huu nipoona katika runinga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gilasius Byakanwa, akiwa katika Kiwanda cha Korosho Tandahimba akitoa uamuzi wa serikali (kwa barua rasmi) kwa mwekezaji wa kiwanda kile kununua korosho kwa kufuata maelekezo ya serikali kupitia mnada wa stakabadhi ghalani.
Na kwamba amalizapo kubangua afuate sheria za ununuzi wa korosho kama ilivyoelekezwa na serikali kupitia minada na si kujinunulia kwa watu binafsi kwa ‘kangomba’! Jambo hili limeshamiri sana kule Kusini licha ya serikali kuamuru ununuzi wote wa korosho ufanyike mnadani na kwa stakabadhi ghalani.
Nikafikiri sana juu ya tatizo la zao hili la korosho hasa mikoa ya Kusini, yaani Mtwara, Lindi na Ruvuma (Wilaya ya Tunduru). Kwanini daima kunazuka kelele za ununuzi holela wa korosho?
Wakati wa Bunge la Bajeti, Juni, mwaka huu, nusura bajeti ya serikali ikwamishwe bungeni kutokana na sokomoko la korosho. Ilifika wakati Spika Job Ndugai aliita ‘Bunge la Korosho’, kwa jinsi mjadala ulivyotikisa Bunge.
Sababu za sokomoko lote lile bungeni ni kutokana na fedha za ushuru wa mazao ya korosho nje ya nchi. Serikali iliamua fedha zile za mauzo – Sh bilioni 800 ni maduhuli ya serikali – ziwekwe kwenye kapu kuu la serikali – yaani Hazina. Kumbe wabunge wa Kusini zinakolimwa korosho walidai uamuzi ule wa serikali haukuwa sahihi. Wao wanaona ile 65% ya zile Sh bilioni 800 zilizochukuliwa na serikali zirejeshwe kwa wakulima wenyewe mikoani wala serikali isiwaingilie!
Nikaja kuona katika gazeti picha za wabunge na waliyotamka bungeni; kwa Mbunge wa Mtwara imeandikwa: “Kwetu mambo yote ni korosho tu.”
Hapo nikajiuliza, hizi korosho bado zinagonga vichwa vya watu wa Kusini mpaka leo hii? Ndipo Nikaamua kuandika makala hii: ‘Kumbe korosho bado ni ‘umiza kichwa!”.
Kama sote tunakumbuka vizuri, jioni ile ya kupiga kura bungeni, Spika Ndugai, alitoa angalizo hili: “…Waheshimiwa wabunge kabla hamjapiga kura zenu tukumbuke, tusipoipitisha bajeti ya serikali usiku huu, kwa mujibu wa sheria, Rais kesho atalivunja Bunge hili na Bunge likishavunjwa maana yake tutarudi majimboni kuomba kura upya kwa wananchi wetu. Endapo tutafikia hatua hiyo, sidhani kama sote sisi tutarudi katika Bunge hili…”
Hapo kukawa na kijasho chembamba miongoni mwa waheshimiwa wabunge. Wakafikiria mara mbili (had to rethink their positions).
Si hivyo tu, bali na Mheshimiwa Rais aliulizia, kwani humo bungeni kuna wabunge wangapi wa CCM wa kutoka Kusini? Akajulishwa wapo wabunge kadhaa, pamoja na Mbunge wa Ruangwa ambaye ni Waziri Mkuu! Akaona potelea mbali hao wote wakisema “hapana” bungeni kutokana na huo u-Kusini wao bado CCM waliopo wanatosha kuivusha bajeti hii! Basi na yeye (Rais) akawa anangojea matokeo ya kura juu ya bajeti ya mwaka 2018/2019. Usiku ule kwa hamu kubwa (with great anxiety).
Matokeo ya kura usiku ule, sote tunajua. Bunge lilipitisha ile bajeti kwa kishindo. Nchi ikasalimika.
Lakini hii umiza kichwa ya korosho haikuanza mwaka huu. Mimi leo hii ni mzee wa miaka 88. Ni mtu wa Kusini huko huko (mkazi wa Tunduru), lakini nimezaliwa na nimesoma katika Wilaya ya Masasi na nimefanyia kazi zangu kama mwalimu huko huko Masasi katika shule iliyokuwa ikijulikana kama ‘Abbey School Ndanda’ miaka ile ya 1950 kabla ya ule utaifishwaji wa ‘VA schools’ pale mwaka 1970.
Leo hii nasikia shule ile inaitwa Ndanda High School na lile jina la ‘Abbey School’ limepewa shule nyingine na ya binafsi iliyojengwa kule Mwena, huko huko Wilaya ya Masasi.
Katika uzalendo wangu nina uchungu wa kukosa zao la biashara sisi wa Kusini tangu enzi za mkoloni Mjerumani aliyetupiga wakati wa Vita ya Maji Maji na kutushindisha njaa wakati wa vita ile kama mbinu ili atushinde. Kisha ukaja wakati wa ukoloni wa Mwingereza mwaka 1918-1961, tukaachwa hivyo hivyo bila barabara za lami, bila zao kuu la biashara na wala hatukuwa na shule za kutosha.
Ndipo kwa uchungu ule nilipokuwa Mjumbe wa Bodi ya Korosho (1996 – 2000) enzi za hayati mzee Kitwana Kondo na Meneja Mkuu Mandari niliwahi kuandika: ‘Adha ya zao la korosho’ hapa nchini mapema mwaka 2001. Nilitoa historia ndefu ya zao hili na kwa bahati nzuri Gazeti la RAI, toleo Na. 395 la tarehe 10 – 16 Mei, 2001 lilichapisha makala ile chini ya kichwa cha habari: ‘Korosho: Sasa sote tunalia kwa kuwa miiko haikufuatwa.’
Juni, mwaka huu nilipoona sokomoko la korosho linajadiliwa bungeni na baadhi ya wabunge wa Kusini, hasa kutoka Lindi (Kilwa) na kutoka Mtwara (Mtwara na Tandahimba) wamelivalia njuga hata Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT – WAZALENDO) analizungumzia, nikafikiri sana. Hilo zao la korosho lina ukichaa gani hapa nchini?
Sasa, Septemba 5, mwaka huu nilipoona kwenye runinga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gilasius Byakanwa, anatoa mwongozo, tena kwa barua rasmi, nikasema kwanini nisiwakumbushe vijana wetu wa Kusini namna zao hili lilivyokuja kule Kusini? Kwanini sisi wazee tusiwaonyeshe angalau jitihada za serikali kuinua hali ya wa Kusini kupitia zao hili la biashara?
Wenzetu kule Tanga, Morogoro na Pwani walikuwa na zao la mkonge. Wenzetu Wachaga na Wahaya wana zao la kahawa. Wale wa Southern Highlands (Iringa – Njombe na Mbeya) walikuwa na zao la chai na pareto, Wasukuma na Wanyamwezi walikuwa na pamba, tumbaku na ng’ombe.
Enzi zetu miaka ile ya 1940 – 1960 kule Mtwara hakukuwa na mifugo yoyote kama ng’ombe, ilivyo siku hizi. Mtu ukiona ng’ombe, ujue ni wa misheni ya Ndanda tu.
Serikali ilijaribu kuleta karanga na njegere, lakini wapi – vilishindikana. Tukabaki wakulima wa ufuta tu na kurina asali kutoka kwa nyuki wa misituni kisha tukapata nta tukaiita SERA tukiwauzia Wahindi.
Basi, nimeomba Gazeti hili la JAMHURI warudie ile makala yangu niliyotoa mwaka 2001 kuhusu KOROSHO kwa kichwa cha habari kile: ‘Korosho sasa sote tunalia kwa kuwa miiko haikufuatwa’ kama ilivyotolewa kwenye Gazeti la RAI, toleo Na. 395 la 10 – 16 Mei 2001.
Hadi leo hii inaonekana ile miiko bado haifuatwi, bado watu tunakubali kuuza korosho kisirisiri kwa kipimo cha ‘kangomba’. Hivyo ndivyo nilivyoandika miaka 17 iliyopita juu ya korosho. Nitashukuru sana kama Spika Ndugai atapata muda wa kusoma makala yangu ile, pia waheshimiwa wabunge wa Kusini ile ya Southern Province nao wakasoma ili iwasaidie kujua tulivyoanza miaka ile ya 1950 (nineteen fifties) wakati zao la korosho lilipoanzishwa kule Southern Province.

Nukuu ya makala halisi

Katika miezi ya hivi karibuni kuanzia Desemba 2000 na kufikia Aprili 2001 hii, magazeti kadhaa ya humu nchini yamekuwa na habari za korosho. Makala kadhaa zimekuwa na vichwa mbalimbali kulitangaza zao hili la korosho. Magazeti ya Kiingereza na ya Kiswahili hayakutofautiana katika kutoa ujumbe unaohusu korosho. Je, zao hili limetangazwa kwa uzuri wake au kwa ubaya wake?
Yametolewa mawazo ya lawama kwa serikali na Bodi ya Korosho, pia yametolewa mawazo ya namna ya kuliboresha zao hili kwa manufaa ya wakulima wa zao lenyewe. Kwa vyovyote vile magazeti hayo yametoa picha maalumu juu ya korosho na kuamsha hisia za watu kadhaa juu ya korosho zinavyouzwa, adha yake kwa wakulima na uchumi wa taifa unavyoathirika. Kwa kuelewa zaidi uzito wa zao hili inafaa tu mtu kuangalia vichwa vya habari viliyyotolewa katika magazeti mbalimbali kama hivi:
“Bei ya korosho inashushwa kwa njama” (Uhuru Jumatatu 25 Desemba, 2000 uk. 6), “Cashew nut Industry in Crisis” (Business Times, Ijumaa tarehe 2 Machi 2001 ukurasa wa mbele); “Korosho: Soko huria au soko holela?” (Rai, Alhamisi 4 – 14 Machi, 2001 Upembuzi Yakinifu uk. 7); “Korosho: Biashara kichaa Tanzania” (Rai, Alhamisi 15 – 21 Machi 2001 ukurasa wa mbele); “Serikali yaokoa wakulima wa korosho” (Majira Jumapili 18 Machi 2001, uk. 3); “Kahama akubali mambo si sawa kwa zao la korosho” (Mtanzania Jumapili 18 Machi 2001 uk. 5); “Bodi ya Korosho yawafuta machozi wakulima (Alasiri Jumatatu 19 Machi 2001 uk. 6); “Masasi MP accuses Asian traders of exploitation” The African, Monday 26 March, 2001 from page); “Ukichaa wa biashara ya korosho ni matokeo ya uroho wa wafanyabiashara” (Rai, Alhamisi 29 Machi – 4 Aprili, 2001 uk. 11);
“Korosho biashara kichaa Tanzania” (Rai, Alhamisi, Aprili 5 – 11 Aprili 2001 uk. 7); “Serikali ituokoe wakulima wa korosho Mtwara” (Mwananchi Jumatatu Aprili 11, 2001 uk. 7); “Wakulima wa korosho Mtwara tumeyumbishwa” (Mtanzania Jumanne 17 Aprili 2001 uk. 11); “CBT: Kwa wenzetu korosho ni biashara, mpango wa ajira, sisi?” (Mtanzania Jumatano Aprili 18, 2001 uk. 7).
Vichwa hivi vya habari kuhusu korosho vinatoa ujumbe kwa serikali na kwa Watanzania wote kulishughulikia zao hili la korosho kikamilifu. Kila mtu anayo haki ya kutafsiri vichwa hivyo vya habari za korosho anavyoona yeye.
Mimi binafsi ninajiuliza swali kubwa akilini mwangu, katika msimu huu wa 2000/2001 “Korosho: Kulikoni?” Kutokana na swali hili nimeona niwakumbushe Watanzania wenzangu historia ya zao la korosho tangu miaka ile ya 1940 lilipoanzishwa katika nchi yetu.

Itaendelea…

By Jamhuri