DAR ES SALAAM

NA WAANDISHI WETU

Kishindo kikubwa kinatarajiwa kuanza kusikika wiki hii baada ya mabadiliko ya uongozi katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Mtikisiko huo, pamoja na mambo mengine, utawahusisha baadhi ya vigogo wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi.
Tayari kuna orodha ndefu ya majina ya watu wanaokusudiwa kufikishwa kwenye ‘Mahakama ya Mafisadi’ kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kwenye orodha hiyo wanatajwa kuwamo vigogo wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi kwenye zabuni za usambazaji umeme vijijini awamu ya III.
Chanzo cha habari kimeliambia Gazeti la JAMHURI kuwa orodha ‘iliyokaliwa’ na Valentino Mlowola kwa miaka zaidi ya miwili, sasa itaanza kuonekana kwa wahusika kufikishwa mahakamani.
Wakati hayo yakisubiriwa, wale waliokwisha kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa ya ufisadi na utakatishaji fedha, wanaonekana kudhoofu; hali inayoashiria kuwa mahabusu si sehemu ya mchezo.
Mabadiliko ya utendaji kazi wa Takukuru ni utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli, aliyompa Mkurugenzi Mkuu mpya wa taasisi hiyo, Diwani Athumani, alipomwapisha Ikulu, Dodoma, wiki iliyopita.
Diwani, ambaye ni Kamishna wa Polisi, aliteuliwa Septemba 6, akijaza nafasi ya Valentino Mlowola, ambaye ameteuliwa kuwa balozi.
Rais amemtaka Diwani aangalie upya muundo wa Takukuru ili uweke bayana majukumu ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo; ametaka watendaji wa taasisi wanaojihusisha na rushwa waondolewe na wafikishwe mahakamani.
Akasema vijijini wananchi wanateseka mno, wananyanyaswa na kuna dhuluma nyingi ambazo chanzo chake kikuu ni rushwa.
Agizo jingine kubwa alilompa ni kuongeza kasi ya kushughulikia rushwa, hasa rushwa kubwa kubwa, kwa kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa mahakamani.
Rais Magufuli akiwa mkoani Mara alisema amemwondoa Mlowola kwa kushindwa kushughulikia tuhuma za rushwa zilizowasilishwa kwake kutoka Mkoa wa Mara.
Tangu aingie madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli ameongoza mapambano dhidi ya rushwa, kwa kuhakikisha baadhi ya watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha wanafikishwa mahakamani.

Harry Kitilya

Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (EGMA), Harry Kitilya na waliokuwa maofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Sumari wako rumande wakituhumiwa kutakatisha fedha.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola milioni 550 za Marekani kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Chartered Uingereza.
Wanadaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia dola milioni sita za Marekani, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya EGMA (T) Ltd.
Wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha dola milioni sita za Marekani katika akaunti tofauti tofauti za benki.

Rugemalira na Sethi

Mfanyabiashara Harbinder Sethi na James Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi na matano ya kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh 309,461,300,158.27.
Kesi hiyo ipo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu Kisutu. Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia serikali hasara na kutakatisha fedha.
Katika shtaka la kwanza, Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa Independent Power Tanzania Limited (IPTL), na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Pan-African Power Solutions (PAP), wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.
Kwa upande wa shtaka la tatu, Sethi anadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio, Ilala jijini Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu Na. 887 Mtaa wa Mrikau, Masaki wakati akijua ni uongo.
Sethi katika shtaka la nne anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14a ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera, kwa njia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.
Katika shtaka la tano, washtakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Novemba 28/29, 2011 na Januari 23, 2014 Makao Makuu ya Benki ya Stanbic, Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi la St. Joseph, kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh 309, 461,300,158.27.
Katika shtaka la sita la kusababisha hasara, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic Tawi Kuu Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya USD 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Inadaiwa kuwa Novemba 29, 2013 katika Tawi Kuu la Benki ya Stanbic Tanzania, Wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua BoT dola 22,198,544.60 za Marekani wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Malinzi, Aveva

Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, pamoja na Katibu wake, Mwesiga Celestine, wanakabiliwa na kesi ya kutakatisha fedha.
Kati ya mashtaka hayo, Malinzi pekee anakabiliwa na mashtaka 22 ya kughushi risiti mbalimbali zinazoonyesha kuwa aliikopesha TFF fedha kwa nyakati tofauti.
Mashtaka mengine yanawahusu Selestine na Nsinde Mwanga, huku shtaka moja likiwahusu wote.
Pia, aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evance Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange (Kaburu), nao wanatuhumiwa kwa makosa matano likiwamo la kughushi nyaraka na kutakatisha fedha.
Aveva na Nyange wanakabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha, dola 300,000 za Marekani.

Hanspope

Takukuru imetangaza donge la fedha kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hanspope.
Mbali na Hanspope, Mkurugenzi Mtendaji na mmiliki wa Kampuni ya Ranky Infrasture and Engineering, Franklin Lauwo, naye ametakiwa kujisalimisha Takukuru ili ahojiwe.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbung’o, aliwambia waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa Hanspope kwa kushirikiana na washtakiwa wengine – Evans Aveva na Geofrey Nyange – walitoa maelezo ya uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu ununuzi wa nyasi bandia.
Inadaiwa kwamba washtakiwa walisema uongo kuwa walinunua nyasi bandia kutoka kwa Kampuni ya Ninah Guangzhou Trading kwa dola 40,577 za Marekani (Sh milioni 92.5); na kwamba ukweli ni kuwa walinunua kwa dola 109,499 za Marekani (Sh milioni 249.6).
Lauwo anakabiliwa na kosa la kufanya biashara ya ukandarasi bila kusajiliwa kwenye Bodi ya Makandarasi nchini. Inadaiwa kuwa alijenga Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Simba uliopo Bunju, Manispaa ya Kinondoni na kulipwa Sh milioni 249.9.
Hanspope ambaye anadaiwa kuwa na hati tatu za kusafiria, aliondoka nchini Aprili, mwaka huu kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga kwa kutumia hati ya kusafiria ya Afrika Mashariki.

.tamati…

Please follow and like us:
Pin Share