Na Mwandishi Wetu

Makontena aliyoingiza nchini Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
yameleta ‘shida sana’ bandarini na sasa
mfumo wa kutoa na kuingiza makontena
kwenda kwenye ICD utabadilishwa,
JAMHURI limebaini.
“Kwa kweli hapa tulikuwa tunaangalia bill of
lading na taarifa za mzigo (cargo manifest).
Lakini pia kule TICTS walikuwa bado
wanaweza kutoa makontena kwenda
kwenye ICDs (Bandari Kavu) bila
kutushirikisha.
“Hata haya makontena ya Makonda kwenda
DICD yalipitia TICTS. Sasa kwa kweli
utaratibu huu tumeona hapana. Sisi Bandari
tayari sheria imebadilishwa na kutuongezea
madaraka, hivyo kuanzia sasa tutatoa

utaratibu utakaomtaka kila mteja
kuorodhesha mali au bidhaa zilizomo
kwenye kontena.
“Utaratibu wa sasa unaweza kukuta
tunaingiza hadi mabomu bila kujua, maana
scanner huwezi kufahamu kama zinatumika
vilivyo. Mkurugenzi Mkuu [Deusdedit]
Kakoko amekuwa akisema mara zote na
sasa naona hili litatekelezwa kwa jinsi alivyo
mkali.
“Baadhi ya watu aliowakuta hapa bandarini
walikuwa wanasema analeta utaratibu mpya
usiokubalika, hautafanya kazi, lakini angalia
mapato ya bandari yalivyopanda. Tunahitaji
fikra mpya, hivyo hata hii akitaka vitu vyote
viorodheshwe kimoja baada ya kingine
vilivyomo ndani ya kontena lazima ifanyike.
“Sasa si umeona kwa makontena ya
Makonda tunaambiwa ni viti vya shule
kumbe kuna hadi masofa kama alivyosema
Mheshimiwa Rais [John] Magufuli. Hii ni
hatari, inabidi orodha ya bidhaa kwenye
kontena itolewe,

” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI limemtafuta Injinia Kakoko
kufahamu utaratibu huu mpya utaanza

kutekelezwa lini, akasema: “Hili ni muhimu,
ila nakwenda safari, ngoja nikirudi
tutalizungumza kwa kina. Lazima bandari
zetu ziwe salama na muda wote nimekuwa
nikibana ninapobaini ulegevu,

” amesema

Injinia Kakoko.
Wiki iliyopita Gazeti la JAMHURI lilichapisha
habari kuhusu Rais Magufuli akimkemea
Makonda na kumtaka alipe kodi kwa
maelezo kuwa serikali haijaomba msaada
wa viti kwa walimu. Rais Magufuli alisema
ndani ya makontena taarifa alizonazo kuna
hadi masofa, ambayo hayawezi kuwa vifaa
vya walimu.
Fikra hizi za Bandari zinakuja siku chache
baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.
Philip Mpango, kuzulu eneo la kuhifadhia
makontena – Bandari Kavu Dar es Salaam
(DICD), na kukagua makontena 20
yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda, kisha
akaiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kuendelea na mnada wa makontena
hayo ili kupata kodi ya serikali inayokadiriwa
kufikia Sh bilioni 1.2.

Hata hivyo makontena hayo kwa wiki tatu
mfululizo sasa yamekosa wateja, huku
Makonda akitoa tishio kuwa yeyote
atakayeyanunua Mungu atamlaani.
Dk. Mpango alisema kodi hiyo inadaiwa kwa
mujibu wa sheria za nchi baada ya mwenye
mali kushindwa kulipa kodi na kwamba
amesikitishwa na vitisho vinavyotolewa na
mkuu huyo wa mkoa na vilivyonukuliwa na
baadhi ya vyombo vya habari
nchini, akitumia vifungu vya Biblia kwamba
yeyote atakayenunua mzigo huo
atalaaniwa.
“Sheria za nchi hazichagui sura wala cheo
cha mtu, na mimi ndicho nilichoapa,
kutekeleza sheria za nchi, sheria za kodi,
ndiyo dhamana niliyopewa. Kwa hiyo
Kamishna, simamia sheria za kodi bila
kuyumba,

” alisisitiza Dk. Mpango akitoa

maelekezo kwa Kamishna wa Forodha, Ben
Usaje.
Alifafanua kuwa mzigo wa samani
ulioagizwa kutoka nje ya nchi hauna
msamaha wa kodi na kwamba huyo
aliyeagiza (RC Paul Makonda) alipe kodi

stahiki na asipolipa kodi hiyo mchakato
unaoendelea wa kuyapiga mnada
makontena hayo uendelee.
“Napenda niwaombe viongozi wenzangu
serikalini, ni muhimu tukachuja maneno!
Unasema mtu anayekuja kununua samani
atapata laana, tena laana ya Mungu, kwa
nini tunamhusisha Mungu kwenye vitu vya
namna hii?” alieleza kwa masikitiko Dk.
Mpango.
Dk. Mpango alitoa wito kwa Watanzania
wanaotaka kununua bidhaa hizo ambazo
nyingi ni vifaa vinavyoweza kutumika
shuleni ama ofisini kama vile viti, meza na
makabati, kujitokeza bila hofu kununua mali
hizo.
Aliwaomba walimu na wanafunzi wasiwe
na wasiwasi na kwamba Serikali ya Awamu
ya Tano imejipambanua na kuwekeza
kwenye elimu kwa kutenga zaidi ya Sh
bilioni 20 kila mwezi kulipa ada ya
wanafunzi wasome bila kulipa ada na ina
mpango madhubuti wa kuboresha
miundombinu ya elimu nchi nzima, ikiwemo
ujenzi wa madarasa na ofisi za walimu.

“Tunawapenda na kuwathamini sana
walimu wetu, asitokee mtu yeyote akaanza
kuwaambia hadithi kama vile serikali hii
inawapuuza! Si kweli hata kidogo,

aliongeza Dk. Mpango.
Kwa upande wake, Kamishna wa Forodha
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Ben Usaje, alimweleza Dk. Mpango
kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda, aliwasilisha maombi ya
kutaka kupewa msamaha wa kodi wa
makontena 36 yenye samani kutoka kwa
Diaspora nchini Marekani.
Alisema miongoni mwa makontena hayo
yaliyoingia nchini ni makontena 20 ambayo
yanadaiwa kodi ya Sh bilioni 1.2 na kwamba
utaratibu kwa kumtaka Makonda alipe kodi
hiyo aruhusiwe kuyachukua makontena
ulifanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba
mpaka sasa hajayachukua ndiyo maana
yanapigwa mnada.
Aliwatahadharisha watu wanaotumia
masuala ya siasa na uongozi serikalini
kutaka kukwepa kulipa kodi kwamba suala
la kodi za samani zinaonekana ziko juu kwa

sababu Bunge lilitunga sheria hiyo kulinda
soko la ndani la samani na kuweka sheria
ya kutokuwepo kwa msamaha wowote wa
kodi kwenye bidhaa kama hizo.

Historia ya makontena

Historia ya makontena hayo ni kwamba,
TRA ilichapisha orodha kwenye Gazeti la
Serikali la Daily News la Mei 12, mwaka huu
ikiwataka wamiliki wa mali zilizokaa
bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza
kuzilipia.
Tangazo hilo lilionyesha kuwa TRA
inakusudia kufanya mnada wa wazi Juni,
mwaka huu kwa mizigo iliyokaa bandarini
muda mrefu bila kukombolewa yakiwamo
makontena ya Makonda.
Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa Mei
12, mwaka huu na Kaimu Kamishna wa
Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye
na kuchapishwa na Daily News, wamiliki
walitakiwa kuitoa mizigo hiyo ndani ya siku
30 kuanzia siku ilipotangazwa.
Katika tangazo hilo lililokuwa na orodha ya

makontena zaidi ya 800, jina la Paul
Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa
mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika
Bandari Kavu ya ICD yakiwa na bidhaa
kadhaa kama samani.
Ingawa hakukuwa na uthibitisho kuwa
Makonda ndiye mwenye makontena hayo,
Februari 16, mwaka huu Makonda
alikaririwa katika mtandao wa Gazeti la
Serikali la HabariLeo kuwa alipokea
makontena 20 yenye samani
zitakazotumika katika ofisi za walimu
zinazoendelea kujengwa. Mzigo huo
ulikuwa sehemu ya shehena ya makontena
36.
Samani hizo za ofisini zina thamani ya Sh
bilioni 2 ambazo zilitolewa na Watanzania
waishio Marekani wanaojulikana kama Six
Region Diaspora Council.
Baadaye, Mei 20, mwaka huu, ilisambaa
barua ya TRA ikionyesha makontena ya
Paul Makonda yana thamani ya Sh bilioni
1.4.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share