Ndugu Rais, ni lini mwokozi wangu atapita kwangu nami nipate kuligusa
pindo la vazi lake ili haya ninayowalilia waja wake yafike mwisho?
Maskini aliye na raha ya Mungu ana raha ya milele! Chama Cha
Mapinduzi kimepata Katibu Mkuu mpya. Na awe tumaini la wenye mioyo
iliyopondekapondeka!

Katibu Mkuu weka akilini kuwa, umeteuliwa kushika nafasi hiyo kutokana na vile ulivyo sasa. Kusema kwako, kufikiri kwako na kutenda kwako. Ukibadilika utakuwa umepoteza sababu ya kuteuliwa kwako. Utakuwa mzigo mwingine. Kataza chama kilichokuwa cha ukombozi kujiita chama tawala. Tambua kuwa baadhi ya viongozi wamefuga vuvuzela wakidhani ni wapambe. Baadhi wamewamilikisha madaraka na vijisenti.
Ndugu Katibu Mkuu, kazi kubwa ya kwanza iliyoko mbele yako ni
kuwaunganisha Watanzania. Nataraji uliisikia hotuba makini yenye
kuonya na kukaripia aliyoitoa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki
kutoka Kenya.

Akihutubia Bunge la Afrika Mashariki, aliyaiita yale ambayo Mwalimu Nyerere aliyaiita ni maendeleo ya  vitu kuwa ni‘hardware’, vifaa vigumu. Alivitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni kama soko la pamoja, pasipoti, ujenzi wa miundombinu, nk. Mambo ya uongozi bora, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu, uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa raia na kadhalika.

Mambo ambayo Baba wa Taifa aliyaita mabadiliko wanayoyataka Watanzania, yeye aliyaita kuwa nisoftware.
Akasema kukazania hardware peke yake maisha hayana maana kwa
mwanadamu. Software ndiyo utimilifu wa utu wa mtu. Usimtangulize Mungu mbele wewe ukabaki nyuma. Mungu hatangulizwi mbele. Mungu anapaswa kuishi ndani yako!
Nyerere aliposema Watanzania wanataka mabadiliko, aliyataja mabadiliko
yenyewe katika hotuba yake aliyoitoa Mbeya. Alisema, “Tupeni mgombea
atakayekidhi matarajio ya wananchi. Atakayekidhi matarajio ya
Watanzania. Tupeni mgombea anayetambua kuwa nchi hii ni nchi ya
wakulima na wafanyakazi ambao wote ni maskini. Mgombea ambaye atakuwa anaelewa hivyo. Watanzania wanataka mgombea atakayeshughulika na umasikini wao. Atakayeshughulika na hali zao za afya mahospitalini.
“Wanataka mabadiliko katika hali zao za afya mahospitalini. Watanzania
wanataka uhuru wa kutembea na kutoa mawazo yao. Hawataki kuishi maisha ya hofu”.

 Watanzania wanataka software.Hakuna mahali katika hotuba yake hiyo muhimu ambako Baba wa Taifa anasema Watanzania wanataka mabadiliko ya hardware au ya vitu. Na hata katika hotuba nyingine, alidiriki kuyafananisha ya hardwareyaani maendeleo ya vitu na ujinga. Anasema tulifanya ujinga kuitazama Europe na North America tukadhani yale ndiyo maendeleo.

Waliona inamelemeta kwa majengo marefu, ndege zikipishana angani huku chini treni zikitambaa kama chatu. Baba wa Taifa anasema Watanzania wanataka mabadiliko katika software.
Katibu Mkuu, wewe ni mchambuzi mahiri, hii ni kasoro kubwa kwa
Serikali ya Awamu ya Tano. Ni matarajio ya wengi kuwa utakuwa jasiri
katika kuirekebisha. Abdulrahman Kinana alikuwa jasiri kiasi cha kumwambia Rais wake na Mwenyekiti wake kuwa baadhi ya wale aliowateua kuwa mawaziri, walikuwa ni mizigo kwa wananchi. Na aliwataja hadharani. Ni makusudi ya Mwenyezi Mungu kukupeleka hapo ili ukawapunguzie magumu waja wake.
Baba, masikini wa nchi hii wameteseka sana! Kama Awamu ya Nne isingetikiswa mapema, leo Tanzania ingekuwa paradiso kwa sababu ilikuja na kipaumbele chasoftware ambayo ndiyo mabadiliko wanayoyataka wananchi. Ilipoingia tu madarakani, Waziri Mkuu Edward Lowassa akitangaza dira ya Serikali yao, alisema, “Tutajenga shule ya sekondari katika kila kata. Tukimaliza, tutajenga zahanati katika kila kijiji. Lakini kichwa cha Serikali ya Awamu ya Nne ‘Edward’ kiliondoka mapema. Leo Watanzania dira yao ni ipi?
Ndugu Rais, asante kwa kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa barabara
ipitayo kijijini kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ambao
hatujajaliwa kufika Butiama kwake, ndiyo tunajua kuwa kumbe njia
iendayo kwa Baba wa Taifa bado ni ya vumbi hata baada ya miaka 57 ya
Uhuru. Huyu ndiye mwasisi wa Taifa hili na huyu ndiye aliyeleta Uhuru.
Ndiye Rais wetu wa Kwanza kwa miaka zaidi ya 23. Katika miaka mingi
kiasi hicho angetaka kuijenga Butiama ifanane na sehemu ya London ya
Uingereza, nani angemzuia? Baba Nyerere hakuwa mbinafsi. Aliujua na
kuumizwa na umaskini wa Watanzania!
Kujenga uwanja wa ndege kijijini laweza kuwa ni jambo la maendeleo.
Lakini kujenga uwanja wa ndege kijijini wakati maskini wanakufa kwa
kukosa hela ya kununulia dawa wanazoandikiwa na madaktari
hospitalini na  huku maskini mama zetu wakiendelea kuzuiwa katika
hospitali zetu kwa kushindwa kulipa gharama za hospitali za Serikali
za kujifungulia, ni wachache kama wapo watakaosema hiyo ni busara.
Yeyote aliye na hofu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu atasita kufanya
ubinafsi huu hata kama kijiji hicho ndipo alipozaliwa Mtume Mohamad
(SAW)  au Kristu Yesu mwana wa Mungu aliye hai!
Ndugu Rais Julius Kambarage Nyerere aliwapenda watu wote kuliko
alivyojipenda mwenyewe. Aliipenda dunia kama alivyoipenda nchi yake.
Alijua kuwa Mwenyezi Mungu aliwawekea Watanzania urithi mkubwa kabisa ambao duniani kote, hakuna. Urithi ulioko Stiegler’s Gorge. Kwa
mapenzi ya kimungu Nyerere alikubaliana na dunia, urithi huu uwe
wa kuwaletea faraja wana wote wa dunia hii katika umoja wao!

 Anayekuja leo kutaka kupingua uamuzi huu wa kimungu uliobarikiwa na Baba wa Taifa na mwasisi wa Taifa hili, mpisheni apite! Historia ukiigandamiza kwa fikra nzito hutoa majibu yote ya kesho. Wasiojulikana wamewatishia kuwapiga, kuwagalagaza, kuwafunga jela na kuwatemea mate! Mwenyeheri mwenyewe akishakuwa mtakatifu atamhukumu! Utakatifu wake anaoupata, ni pamoja na kuutoa urithi huu wa Stiegler’s Gorge, badala ya kuwa wa Watanzania peke yao akaufanya uwe kwa wana wote wa dunia hii! Kuuita tena mradi huu kwa jina la Julius Nyerere, itafanana sana na kumdhihaki marehemu. Mungu hatakubali!
Akimsomea misa yake ya mwisho, Baba Mwadhama alisema, “Siyo kazi yangu kumtangaza mtu kuwa ni mtakatifu…lakini wakija tokea watu wa kutaka kumdhihaki marehemu huyu, wajue nguo yake ya ndani itamsitiri!”
Mavuvuzela watatesa na kuwaua masikini wengi, lakini je, wao watabaki
milele wakiilinda dunia?

.tamati….

Please follow and like us:
Pin Share