Na Pd. Dk. Faustin Kamugisha

Kwenda maili moja zaidi ni sababu ya mafanikio. Kufanya jambo zaidi ni sababu ya mafanikio. “Hakuna msongamano wa magari kwenye maili moja zaidi,” alisema Zig Ziglar. Maili moja zaidi haina umati wa watu. Maana yake ni kuwa kuna watu wachache wanaofanya mambo zaidi ya yanayotakiwa.
“Mafanikio yanaanzia kwenye maili moja zaidi,” alisema Yulkan Shirlk. Mtu anayefanikiwa ni yule anayefanya jambo zaidi kuliko kiwango kinachotakiwa. Kuna aliyesema: “Amini wakati wengine wanakuwa na shaka. Panga wakati wengine wanacheza. Amua wakati wengine wanachelewa. Andaa wakati wengine wanaota ndoto za mchana.
“Anza wakati wengine wanasitasita. Fanya kazi wakati wengine wanatamani. Weka akiba wakati wengine wanatapanya ovyo. Sikiliza wakati wengine wanaongea. Tabasamu wakati wengine wanabibidua midomo. Sifia wakati wengine wanalaumu. Ng’ang’ania wakati wengine wanaacha kazi.”
Kama ni kujitahidi, jitahidi zaidi na zaidi. Neno ‘zaidi’ maana yake mambo yanayopita kiwango cha kawaida. Neno zaidi linamaanisha: iliyovuka idadi au kiwango kinachotakiwa, nyongeza, iliyovuka kiwango kwa sifa kama ukubwa au uzuri. Bwana Yesu alisema: “Na kama mtu akikusonga umsindikize maili moja, nenda naye maili mbili.” (Mathayo 5:41).
Tofauti ya mtu ambaye amefanikiwa na yule ambaye hakufanikiwa ni maili moja zaidi. Kila mtu anasimama, lazima usimame uonekane. “Ukitaka kufanikiwa katika kazi yoyote, uwe mtu wa manufaa. Nenda maili zaidi; wafanye watu washindwe kufikiria maisha bila wewe yatakuwaje,” alisema Rose Mathews. Toa huduma zaidi. Toa huduma bora zaidi.
Fanya jambo zaidi ya kutazama, ona. Fanya jambo zaidi ya kusikia, sikiliza. Fanya jambo zaidi kufikiri, tafakari. Fanya jambo zaidi ya kuongea, sema kitu chenye maana. Fanya jambo zaidi ya kuwepo, ishi. Fanya jambo zaidi ya kuishi, penda. Fanya jambo zaidi ya kupenda, toa.
“Biashara ni kama toroli. Hakuna kinachotokea mpaka uanze kusukuma,” alisema Robert Kiyosaki, mwekezaji na mfanyabiashara. Lazima kufanya kitu zaidi. Unaposambaza huduma ya vitu ni vizuri kuwa na vitu lakini lazima kuuza. Lazima kutoa huduma. Robert Kiyosaki anapendekeza: “Ukitaka kuwa tajiri hudumia watu wengi zaidi.”
Andrew Carnegie, mwanaviwanda mkubwa na mtu mkarimu sana katika hotuba yake kwa wahitimu alisema kuwa kuna aina tatu za vijana: wale ambao hawakutimiza wajibu wao wote, wale ambao walisema kwa mdomo kuwa watatimiza wajibu wao, na wale ambao walitimiza wajibu na kufanya jambo la ziada, “jambo dogo zaidi.” “Ni jambo dogo zaidi ambalo linashinda,” alisema. Alizidi kushauri: “Fanya kazi yako na jambo kidogo zaidi, na wakati ujao utajishughulikia mwenyewe.”
Kuna kampuni ambayo inajivunia kuandika jina la mteja kwenye kikombe cha kahawa. Kampuni hiyo inaitwa Starbucks. Mwajiriwa mmoja ameipeleka mbali kampuni hii. Aliamua kujifunza lugha ya ishara kuweza kumsaidia mteja wake kiziwi. Sasa hivi kampuni hii imekuwa ni gumzo mitandaoni kwa ufanisi wake. Lakini mwajiriwa mmoja tu ndiye katenda yote hayo.
Ukianza kwenda maili moja zaidi katika kila unalolifanya, fursa zitakufuata kama kivuli kimfuatavyo mtu. Kuna aliyesema hivi: “Kuwa juu kule wanapokaa watu asilimia moja uwe tayari kufanya lile ambalo asilimia tisini na tisa hawafanyi.” Kwenda maili moja zaidi kunakufanya uwe na mtazamo chanya.
Kunakufanya ufanikiwe na ujitegemee. Kwenda maili moja zaidi kunakufanya kuipa mgongo na kwa heri tabia ya kusitasita. “Mtu anayefanya zaidi ya anacholipwa muda mfupi ujao atalipwa zaidi ya analolifanya,” alisema Napoleon Hill. Kwenda maili moja zaidi kunaongeza kipato.

Mwisho

By Jamhuri