url-2Umewahi kukaa na kutafakari mashairi ya wimbo wa Mrisho Mpoto uitwao Sizonje? Umewahi kuhisi anayeimbwa katika mashairi ya wimbo huo ni nani? 

JAMHURI imegundua kwamba Sizonje ni Rais John Magufuli, huku akikiri kwa kinywa chake, mbele ya wahariri pamoja na msanii wa wimbo huo uliojaa fasihi.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, baada ya kuwaalika wahariri, alimwambia Rais Magufuli, yupo msanii Mrisho Mpoto, ambaye ameandaa wimbo mpya unaoeleza aliyoyafanya kwa mwaka mmoja.

“Mheshimiwa Rais, Mrisho Mpoto ameandaa wimbo maalumu kwa ajili yako, amesema kwenye wimbo huo amekuita kaka, mtangulizi wako alimwita mjomba,” anasema Msigwa.

Rais Magufuli huku akitabasamu anasema “Sipendi Mpoto aniite kaka…kuna ule wimbo wangu ambao tayari alishanitafutia jina tena ukaniimba, unaniita Sizonje…”

Katika wimbo huo wa Sizonje, msanii Mrisho Mpoto ameghani mashairi akisema ‘karibu sana Sizonje, hii ndo nyumba yetu, tulipoficha mundu za kupondea wezi, kwani, makaburi yaliofukuliwa lazima yazikwe upya?

‘Nyumba hii Sizonje ina vyumba vine, vitatu havifunguki, kimoja hakina mlango, japo kuwa kina watu ndani, na hawaongei Kiswahili, wenyeji wanalala sebleni na walishazoea, Sizonje kule tulipotoka panaitwa jikoni, huna haja ya kwenda kule, kumejaa mafundi wa kupika, sasa hivi wanakupikia wewe ili ule ulale, ukiamka muongee nini hasa ujio na dhima ya safari yako.

‘Wanashangaa mbona ghafla, samahani sana mgeni, wapishi wameniomba kwamba, nikuulize tena kwa kukuomba kwamba, eti unapenda vya mafuta au vya nazi? Wanataka kukuonesha madoido katika mapishi yao Sizonje, Sizonje chumba hiki naomba usiingie.

‘Ukimaliza nitakwambia kwa nini, kuna sauti inajirudia mara kwa mara, na hapa mlangoni kulikuwa na picha mbili kubwa, moja picha, nyingine mchoro wa picha wa kwanza, ninachokumbuka iliwahi kuandikwa usiyemtaka kaja, hatukuwahi kuelewa maana yake, labda kwa sababu ya ujio wako unaweza kutusaidia.’

Akizungumza na JAMHURI, mtunzi wa wimbo huo, Mrisho Mpoto, anasema amefurahi sana kuona Rais Magufuli ni shabiki wa muziki wake, ambao mashairi yake huwa yanakosoa utawala na kuelezea matarajio ya wananchi kwa Serikali.

“Nina furaha kubwa sana leo, nakosa maelezo sahihi ya kuelezea furaha yangu, Rais anaposema anapenda kazi zangu, wakati Tanzania tupo wasanii wengi, hilo ni jambo la faraja na sitabweteka nitaendelea kutoa tungo zenye kubeba matumaini ya wanyonge,” anasema Mpoto.

Anaongeza; “Rais Magufuli alikuwa anatafsiriwa kama mtu asiyependa muziki, huu ni mwanzo mzuri kwetu wasanii.”

Mrisho Mpoto amezaliwa Oktoba1 978, ni msanii wa muziki wa dansi, sanaa ya jukwaani, mwandishi wa vitabu vya mashairi na hadithi zenye mafunzo na ni msanii wa ngoma za asili.

Anafahamika sana kwa jina lake la utani kama ‘Mjomba’, pia anafahamika kwa kuimba nyimbo kama vile Salam Zangu Mjomba, Nikipata Nauli, Adela, Chocheeni Kuni, Samahani Wangangu, Mtu Huru, Waite na Njoo Uichukue, alizoimba na Banana Zorro.

Mrisho Mpoto ni mmoja wa waanzilishi wa kundi la muziki la Parapanda, baadaye Mpoto Theatre

3621 Total Views 4 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!