Na Mwandishi Wetu

Siku moja baada ya Gazeti la Jamhuri, kuandika kuhusu wazazi kuombwa michango wanapowapelek watoto wao shuleni huko wilayani Butiama, Mara.  Rais John Magufuli amepiga marufuku shule za msingi na sekondari nchini kuwafukuza wanafunzi kwa sababu ya kutochanga michango mbalimbali ya shule.

Akizungumza Jumatano ya wiki iliyopita, Ikulu jijini, Dar es Salaam baada ya kukutana na mawaziri wanaohusika na sekta hiyo amesema ikitokea katika wilaya mwanafunzi akarejeshwa nyumbani kwa kushindwa kulipa michango, mkurugenzi wa wilaya atafukuzwa kazi.

Kwa taarifa hii mkawaeleze wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi. Nikisikia kuna shule katika wilaya fulani ambayo watoto wanarudishwa kwa sababu hawajachangia kitu fulani, huyo mkurugenzi ajihesabu hana kazi,” amesema Rais Magufuli na kuongeza,

Hii waanze kutekeleza kuanzia leo. Maofisa elimu wote wakasimamie hili, haiwezekani tukawa tunatoa elimu bure halafu tutengeneze kero kwa watoto wanaosoma.”

 Gazeti la Jamhuri lina taarifa kwamba, baada ya Rais Magufuli kusoma habari iliyoandikwa na gazeti hili, haraka aliwaita Ikulu, mawaziri wawili wanaohusika na sekta ya elimu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo.

Mawaziri hao walipewa maagizo mazito na Rais, kuhakikisha wanasimamia vizuri sera ya elimu pamoja na ilani ya uchaguzi, iliyosisitiza kuwepo kwa elimu bure kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi sekondari, kidato cha nne.

Michango ya madawati yaliza wazazi Butiama

Wazazi na walezi wenye wanafunzi katika Shule ya Sekondari Butiama, iliyopo Butiama mkoani Mara, wanahaha kupata Sh 35,000 za mchango wa madawati kwa kila mwanafunzi anayeanza kidato cha kwanza.

Baadhi ya wananchi hao wameonekana wakipita huku na kule, hasa katika familia wanazodhani zina uwezo, wakiomba msaada ili watoto wao waweze kuanza masomo.

Mchango huo ni mbali na mwingine wa Sh 20,000 kwa kila kaya kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wananchi kadhaa wameeleza kusikitishwa na michango hiyo, wakisema inakwenda kinyume cha agizo la Serikali la kutowachangisha wazazi na walezi.

Tulipoambiwa elimu bure tulijua tunabaki na kazi ya kununua sare na viatu vya wanafunzi, hatukujua kama bado tutadaiwa michango ya madawati au madarasa,” amesema mmoja wa wazazi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Avemaria Semakafu, amezungumza na JAMHURI na kusema michango hiyo haipaswi kuwapo, isipokuwa kama wananchi wenyewe watakuwa wameridhia.

Amesema mpango wa Serikali wa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne unalenga kuhakikisha watoto wengi wanapata elimu hiyo bila vikwazo.

Haturuhusu michango ya lazima, lakini kama ni ya hiari, sawa. Ni makosa kumzuia mwanafunzi kuanza masomo kwa sababu tu mzazi au mlezi wake ameshindwa kutoa mchango.

Nimeagiza suala hilo [la Butiama] lifuatiliwe na majibu niliyopewa ni kuwa mpango huo umezuiwa ili ubaki wa hiari kwa wale wanaoweza kuchangia tu. Tusaidieni kuhakikisha watoto wanapata elimu maana ni haki yao na ndiyo maana Serikali ikatangaza utoaji elimu bure uliolenga kuondoa kero za michango,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Butiama, Anna-Rose Nyamubi, amezungumza na JAMHURI na kusema mchango unaozungumzwa ni wananchi wao wenyewe waliokaa kwenye vikao vyao na kukubaliana kuchangia kiasi hicho.

Ofisi yangu kama Mkuu wa Wilaya haikuhusishwa, lakini niliambiwa kuwa wananchi wenyewe (wazazi na walezi) walikutana na uongozi wa sekondari wakaafikiana kutoa mchango huo. Kama waliafikiana wao wenyewe sioni kama kuna shida, ila kwa wale ambao hawawezi kutoa kiwango hicho hapo ndipo kwenye matatizo,” amesema.

Amesema Sekondari ya Butiama ina upungufu wa vyumba 10 vya madarasa na idadi kubwa ya madawati. Hakutaja idadi.

Amesema upungufu huo umesababishwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu wa 2018.

Idadi ya wanafunzi imetriple [imeongezeka mara tatu]. Idadi ni kubwa sana, tuna upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati. Hii ni changamoto kubwa na naamini Serikali inaifanyia kazi,” amesema.

Uchumi wa wananchi wengi wa Butiama unategemea kilimo cha kujikimu cha muhogo na mahindi. Hata hivyo, kilimo cha muhogo kimepotea baada ya zao hilo kushambuliwa na wadudu.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Butiama yenye wakazi zaidi ya 15,000 ina shule moja pekee ya sekondari.

2600 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!