MATATIZO YANAPOZIDI UKOMBOZI UNAKARIBIA

Na William BHOKE

Aliyewahi kuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Yohane Paul I, amewahi kusema, “Eee Bwana nichukue nilivyo, lakini unifanye niwe kama unavyotaka wewe.”

Kama wewe unapumua, kuwa na matatizo ni kanuni ya maisha. Matatizo katika maisha ni kama usingizi. Huwezi ukaukwepa usingizi. Ni lazima utalala tu.

Mwandishi Hugh Miller amesema, “matatizo ni fursa zenye miiba.’’ Wana wa Israeli waliokuwa utumwani Misri waliweza kupata fursa ya ukombozi baada ya Mungu kusambaza matatizo kwa Wamisri.

Baada ya kuona matatizo yamezidi katika taifa lake, Farao aliwaruhusu Wana wa Israeli waondoke. Matatizo yanapozidi ukombozi unakuwa uko karibu sana. Wana wa Israeli walipata fursa ya kuondoka Misri baada ya matatizo kutokea.

Ndiyo kusema, kama matatizo yasingetokea Misri, Farao asingewaruhusu Wana wa Israeli kuondoka Misri. Penye matatizo kuna neema. Wana wa Israeli walipata neema ya kuondoka Misri kwa sababu ya matatizo.

Fikiri jambo hili: Wavuvi wanajua wazi kwamba, bahari ni hatari na ina dhoruba ya kuogopesha, lakini hawajawahi kuona hatari hiyo kama sababu tosha ya kuwazuia kuingia baharini kuvua.

Usiyatazame matatizo katika maisha yako kama laana. Yatazame matatizo kama  fursa ya kufanya jambo fulani. Matatizo katika maisha ni mwalimu wa pili.

Mwalimu wa kwanza ni Mwenyezi Mungu. Januari mosi, 2016 kuna mtu alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu yangu ya kiganjani. Ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi:

William, nimechoka na maisha.’’ Nilimjibu, “Usiuanze mwaka kwa kulalamika.’’ Kuna njia mbili za kufukuza maisha ya baraka katika maisha. Njia ya kwanza ni kulalamika.

Ukilalamika kwa kila jambo huwezi kutoka mahali ulipo na kwenda mahali unapotamani uwe. Njia pili ni woga. Ukiwa mwoga huwezi kuyatazama matatizo kama fursa, bali utayatazama matatizo kama laana. Matatizo ni giza la kukusaidia kuona nyota.

Mwandishi Shrikant G. Talager anashauri, “Mtu yeyote asiogope mateso kwa sababu ni jiwe la kuvukia la kuiendea furaha.’’ Uko hivyo ulivyo leo kwa sababu ya namna unavyoishi.

Maisha ni kujifunza. Kila jambo linatokea kwa wakati wake na hubeba fundisho lake. Tunachopaswa kufanya ni kuwa tayari kujifunza. Katika kuishi kwetu kuna nyakati mbalimbali tunakumbana nazo.

Kuna wakati wa kufurahi na wakati wa kuhuzunika. Kuna wakati wa kushinda na wakati wa kushindwa. Kuna wakati wa kusema na wakati wa kukaa kimya. Kuna wakati wa kutembea na wakati wa kukimbia.

Kuna wakati wa shibe na wakati wa njaa. Kuna wakati wa kupata na wakati wa kukosa. Kuna wakati wa haraka na wakati wa polepole. Katika kila vipindi fumbo la maisha linajifunua kwetu.

Barack Obama, aliyepata kuwa Rais wa 44 wa Marekani, ana asili ya kutokea kijiji cha Kogelo huko nchini Kenya. Hakutokea New York. Hakutokea Paris, Ufaransa. Hakutokea Tel Aviv, Israel.

Kwa nini Obama atokee kijijini Kogelo na kwenda kuwaongoza Wazungu? Obama alithubutu. Aliamini anaweza na kweli akaweza. Nawe nakuhamasisha, thubutu.

Makaburi mengi yamejaa watu ambao walikuwa na uwezo wa kupaa na kuwa matajiri wakubwa duniani, lakini wamezikwa hivyo hivyo bila kutoa mchango wowote katika dunia hii.

Tafadhali usizikwe bila kuacha alama yako katika dunia hii. Umepewa maisha kama zawadi jifanye zawadi kwa maisha. Kuna methali ya Kilatini inayosema (kama inavyotafsiriwa kwa Kiswahili), “Mungu hakatai kutoa neema kwa yule anayefanya analoweza.’’

Zione fursa katika matatizo. Binadamu yeyote anayefanikiwa ni yule anayetambua kwamba kuna tofouti ndogo  kati ya matatizo na fursa, na ambaye yu tayari kuyatumia yote mawili kwa manufaa yake.

Usipendelee kuyatumia maneno kama; ‘mimi ni maskini’, ‘mimi sipendwi’, ‘mimi siwezi kupanda cheo’, ‘mimi siwezi kusamehe’, ‘mimi siwezi kupona’, ‘mimi siwezi kufanikiwa’ na kadhalika.

Mitazamo kama hiyo inafifisha nguvu na shauku ya kujenga mawazo yenye ubunifu wa kufanikiwa. Unapokuwa kwenye hali ngumu au unapokuwa na tatizo, toa uamuzi mmoja. Chagua fursa moja miongoni mwa nyingi zilizopo. Kama unaona utata kuchagua, bado hujajua unachotaka.

Usikimbilie kuona kikwazo fulani kuwa ni hatima ya mambo yote. Palipo na shida pana ushindi. Wakati wengine wanaona shida na kukwama, wewe tazama ushindi katika kila shida. Vikwazo vinapoibuka siyo kwamba vitukatishe tamaa.

Vinaibuka tuweze kuvishinda. Usiwe na utamaduni wa kuyakimbia matatizo, bali kabiliana nayo. Mazingira pingamizi ndiyo yanapaswa kukujengea nia thabiti ya kupambana na changamoto unazokutana nazo.

Binadamu bila mateso ya kiroho, kiuchumi, kimwili, kisiasa, kifamilia hawezi kukua. Mwanamke mmoja aliyejimbulisha kama kahaba alipoisoma makala yangu ya ‘Nguvu ya sala katika maisha’, iliyochapishwa na gazeti la JAMHURI, alibadilisha historia ya maisha yake.

Aliacha ukahaba. Baada ya kuisoma makala ile alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu yangu ya kiganjani. Ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi; Leo imekuwa siku njema kwangu na ni siku ambayo historia ya maisha yangu itaandikwa upya. Nimeisoma makala yako ya ‘NGUVU YA SALA KATIKA MAISHA’. Kiukweli kazi yangu ilikuwa ni ukahaba, lakini makala yako nimeisoma kwa umakini na nimeamua kubadilisha historia ya maisha yangu kuanzia leo. Sitakuwa tena kahaba. Asante sana William, Mungu akubariki sana na akupe nafasi nyingine ya kuwasaidia watu.

Huo ndiyo uamuzi thabiti na sahihi. Unasubiri nini wewe ambaye bado hujachukua uamuzi sahihi? Siku pekee uliyo nayo ya kubadilisha historia ya maisha yako ni leo.

Fanya uamuzi leo. Usisubiri kesho. Usisubiri wiki ijayo. Usisubiri mwezi ujao. Usisubiri mwaka ujao. Siku yako ni leo, na siku uliyo nayo ni leo. Imeandikwa, “Wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ndiyo sasa” (2Kor 6:2). Ya Mungu ni mengi huwezi kujua kama kesho utakuwepo au la. Ratiba yako ya kuishi hapa duniani anayo Mwenyezi Mungu.

Tumruhusu Mungu ayaongoze maisha yetu. Mpe Mungu ratiba ya maisha yako. Uliumbwa kwa ajili ya Mungu, na siyo kinyume chake, na maana ya maisha ni kumruhusu Mungu akutumie kwa malengo yake, siyo wewe umtumie Mungu kwa malengo yako.

Zawadi pekee tunayoweza kumpa Mwenyezi Mungu ni kumpa nafasi ya kufanya kazi ndani mwetu kwa kurekebisha mambo yetu yawe kama tunavyotamani yawe.

Hii itatuwezesha sisi kuwa wanadamu wenye utashi, badala ya kuwa kama binadamu wa mwanzo ambaye hakutii maagizo ya Mwenyezi Mungu.

Naomba kukunong’oneza jambo hili: ‘Mwenyezi Mungu anakupenda sana‘. Ni kweli, kuna watu katika maisha yao wamejeruhiwa kiroho, kimwili, kiakili, kiuchumi, kimahusiano na kiungozi.

Wamejeruhiwa sana. Wamejeruhiwa na kujeruhika. Pole kwa kujeruhiwa. Usihuzunike, usiogope, usisononeke. Kama umejeruhiwa na mke ama mume wako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’.

Kama umejeruhiwa na mtoto wako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na rafiki yako, jirani yako, serikali yako, kiongozi wako wa kiroho, mwajiri wako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’.

Narudia kusisitiza kwa msisitizo uliojaa ukweli na hekima kwamba: ‘Mungu hajakukataa. Mungu hajakuacha. Mungu anakupenda sana’.

Kumpiga chura teke ni kumwongezea mwendo. Waliokujeruhi walifikiri wanakukomoa, kumbe walikuwa wanakupiga msasa.

Kwa ufasaha kabisa mwandishi Sariajy Rathi anaandika, “Wakati wowote maisha yanapodondosha pini na sindano kwenye njia yako unayopita, usikae mbali. Badala yake zikusanye pini zilezile ili zisikuumize tena”.

Na mwigizaji Chris Colfer anasema hivi juu ya kuumizwa, ”watu wanaokuumiza mara nyingi wachukulie kama msasa, wanakuumiza kidogo lakini mwisho wa siku utang’aa”.

Pokea ushauri huu: ”wasamehe wote waliokujeruhi katika maisha yako”. Tazama mfano wa kuigwa kutoka kwa Yesu Kristo. Yesu Kristo aliwapa maadui zake zawadi ya msamaha akiwa msalabani.

Zawadi yake ilikuwa katika maneno haya, ”Baba uwasamehe”. Kwa nini wasamehewe? Kwa kuwa hawajui walitendalo (Luka 23:34). Shinda ubaya kwa wema. Usilipize kisasi.

Ni rahisi kwa mtu mwema kutendewa usiyoyapenda. Wakati mwingine utajikuta unakosolewa hadharani hata kama uko sahihi. Unachekwa isivyostahili.

Unadharauliwa na kutukanwa waziwazi. Unaimbiwa taarabu za kila aina. Tafadhali vumilia. Usilipe ovu kwa ovu. Chukia tabia ya kuwa na maadui wengi.