Home MakalaAfya DAWA BANDIA TISHIO AFRIKA

DAWA BANDIA TISHIO AFRIKA

by Jamhuri

NA MTANDAO

Ongezeko la biashara ya dawa bandia limekuwa janga kubwa barani Afrika linalokua kwa kasi, huku ikiripotiwa kusababisha vifo vya watu wapatao 100,000 kwa mwaka.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimarekani linalojihusisha na dawa za magonjwa ya tropiki, limesema kuanzia mwaka 2015 watoto 122,000 walio chini ya umri wa miaka 5 walikufa barani Afrika kwa kutumia dawa bandia za malaria.

Taarifa hiyo imebaini kuwa baadhi ya chanjo za ugonjwa wa uti wa mgongo zilizotumiwa miaka mitatu iliyopita nchini Niger zilikuwa bandia, hali iliyosababisha wengi wao kupoteza maisha na wengine kupata madhara zaidi.

Mkuu wa kitengo cha kupambana na dawa bandia katika kiwanda cha dawa cha Sanofi nchini Ufaransa, Geoffroy Bassaud, amesema dawa bandia zimeendelea kuwa biashara kubwa duniani, hali inayoendelea kutishia afya za wananchi.

Amesema, “Uwekezaji wa dola 1,000 unaweza kutoa faida ya hadi dola 500,000, wakati uwekezaji kama huo katika biashara ya dawa za kulevya aina ya heroin ama fedha bandia, unaweza kutoa faida ya kiasi cha dola 20,000.

Amesema, kwa mfano, mwezi Mei mwaka jana, Serikali ya Ivory Coast ilichoma tani 40 za dawa bandia katika mji wa Adjame, ambao ni maarufu zaidi kwa biashara ya dawa bandia Afrika Magharibi.

Amesema nchini Ivory Cost kuna soko linalofahamika kwa jina la Roxy lililoko mjini Abidjan, lililo maarufu kwa uuzaji wa dawa bandia na kila mara mamlaka zimekuwa zikililenga eneo hilo na kuchoma kiasi kikubwa cha dawa bandia.

Agosti mwaka jana, Polisi wa Kimataifa (Interpol) ilitangaza kukamata tani 420 za dawa bandia huko Afrika Magharibi, ilipofanya operesheni kali iliyohusisha takribani polisi 1,000, wafanyakazi wa idara ya forodha na maofisa afya kutoka nchi 7 za Benin, Burkina Faso, Ivory Coast, Mali, Niger, Nigeria na Togo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa dawa moja kati ya 10 duniani ni bandia, lakini idadi hii inaweza kuwa ni ya juu zaidi inayoweza kufikia dawa 7 kati ya 10 katika baadhi ya nchi, hususan barani Afrika.

You may also like