MAGUFULIKampeni za mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli, zinazoendelea kwa sasa zinaonesha kitu kimoja ambacho ni kama hakijatamkwa bayana. Nadhani hakijatamkwa kutokana na kuhofia kukwazwa katika hatua hizi za awali.

Sababu pamoja na chama tawala, kuamini kwamba Dk. Magufuli ndiye anayefaa kukipeperushia bendera katika uchaguzi wa mwaka huu yeye anaonyesha kutokiamini chama hicho hata kidogo. Hatamki kitu hicho, ila ukisikiliza kauli zake kwa umakini yote anayoyasema yanaonyesha kutokuwa na imani na chama chake.

Dk. Magufuli anasema nchi imefika hapa ilipo, kwa maana ya wananchi kukata tamaa ya maisha, kutokana na uovu ulio katika mfumo wa kiutawala, mfumo uliosimamiwa na chama chake, ambacho ndicho chama tawala. Yeye anatumia usemi wa “…nasema ukweli, nasema ukweli kabisa…”

Mara zote anakofanya mikutano ya kampeni anaonekana akilalamikia rushwa, ufisadi, uzembe, ubinafsi, kutowajibika na kutumia madaraka pamoja na mamlaka kufanya mambo yaliyo nje ya utumishi wa umma, kwa maana ya mambo yaliyo na maslahi kwa watendaji badala ya maslahi ya nchi na wananchi.

Mfano anasema wagojwa wanapoenda hospitalini wanaambiwa wakanunue dawa pale, nje ya hospitali. Wagojwa wanalala zaidi ya mtu mmoja kwenye vitanda vya hospitali, wanaotaka wakalale salama kutokana na kuumwa kwao wanaambiwa wakaende hospitali za binafsi.

Anasema pesa za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu zinatengwa lakini kupatikana kwake ni matatizo matupu. Anasema hayo na mambo mengine mengi ambayo yanalalamikiwa kihalali na wananchi atahakikisha anapambana nayo pindi akipewa ridhaa ya kuingia Ikulu.

Lakini wakati anasema hivyo haoneshi ni kitu gani kilichosababisha hali hiyo ambako tungeweza kukitambua na kuamini kwamba kweli anaweza kuyamaliza matatizo hayo baada ya kuwa amekishughulikia kitu hicho kinachoyasababisha hayo yote yanayowafanya wananchi kukata tamaa ya maisha.

Wakati yeye akisema hivyo chama chake kilichomkabithi bendera ya kuwania urais dhidi ya vyama vingine, CCM, kinajinadi kwa mapambio kikiwadhihirishia Watanzania kwamba “…CCM ni ileile…” kwa maana ya kwamba haiwezi kubadilika hata jua lidondoke chini!

Inapaswa ieleweke kwamba anayoyalalamikia na kuyalaani Magufuli katika kampeni zake hayakutokana hata kidogo na wale anaopambana nao katika kinyang’anyiro hiki, wapinzani. Ni kwamba haya yote yamekuwepo kwa baraka za chama chake, hasa baada ya azimio bubu la chama hicho, Azimio la Zanzibar la mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Anayoyasema Magufuli ni ya kweli kabisa, mfumo alioupitia kuitafuta nafasi hiyo ya kuutaka ukuu wa nchi yetu unahitaji kufanyiwa ukarabati wa nguvu. Lakini je, inawezekana? Sababu wakati akisema kwamba ataufanyia marekebisho, ambayo kwa lugha nyingine ni mabadiliko, sauti kutoka kwenye mfumo huo zinahimiza kwamba CCM ni ileile! Hiyo ni kuonyesha kwamba anayoyasema ama anawadanganya wananchi au anajidanganya yeye mwenyewe, hakuna kitakachobadilika!

Isingekuwa chama chake kinamuunga mkono kwa anayoyasema halafu kikaendeleza kaulimbiu hiyo ya CCM ni ileile. Kama chama hicho kingekuwa kinaamini katika mabadiliko kingesita kuitumia katika mapambio kauli hiyo ya CCM ni ileile. Kingetafuta maneno mengine yanayoonyesha kwamba hii ya sasa ni CCM ya mabadiliko.

Hivi katika hali ya aina hiyo tunaweza kuamini kwamba kweli Magufuli anakipenda chama chake na kukiona kinafaa kuendelea kuongoza nchi huku akiwa anapambana kiuhakika na wapinzani katika kinyang’anyiro hiki cha kutaka kukabidhiwa ukinara wa kuliongoza taifa letu?

Kama Magufuli anaweza kuchukua kaulimbiu za upinzani na kuzigeuza ili zionekane ni za kwake, kama ile ya mabadiliko na M4C,  ambayo yeye ameibadilisha na  kuiita “Magufuli for Change”, anawezaje kutuaminisha kwamba anapingana na upinzani badala ya kutufanya tumuelewe kuwa anapingana na mfumo wake uliomuweka kwenye nafasi hiyo ya kuutafuta ukuu wa nchi? 

Kiufupi, kama kweli Magufuli amekidhamiria anachokifanya kwa sasa, naweza kusema kwamba anapambana na CCM. Sababu hawezi kusema yeye anataka mabadiliko katika mfumo wa nchi hii ilihali chama chake kinatamba kuwa ni kilekile, kisichobadilika,  halafu tukaona kwamba yeye na chama chake ni kitu kimoja.

Swali ambalo ingefaa kila mwananchi ajiulize ni la kwamba hivi kweli Magufuli anaipenda CCM au anaitumia tu kama daraja la kumuingiza Ikulu? Akishaingia Ikulu upo tena uwezekano wa Magufuli kuendelea kuihitaji CCM kwa namna anavyoinanga hadharani? Kusema ukweli kaichoka hata kama hajatamka.

Kwa vile Dk. Magufuli hawezi kufanya kazi ya urais wa nchi peke yake bila mfumo wowote, kinachojionyesha ni kwamba akishaingia Ikulu, kama atakuwa amepata nafasi hiyo, upo uwezekano mkubwa wa yeye kujitenga na chama hicho na kuamua kuanzisha cha kwake kwa mtindo wa Dk. Bingu wa Mutharika, rais wa zamani wa Malawi.

Mutharika kwa kushirikiana na mtangulizi wake, Bakili Muluzi, walianzisha chama cha UDF ambacho ndicho Muluzi alikitumia kuingia madarakani na baadaye kurithiwa na Mutharika.

Lakini baada ya Mutharika kuingia Ikulu, bila shaka akiwa hapendezwi na baadhi ya mambo yaliyofanyika wakati wa Muluzi, lakini huku Muluzi akiendelea kushikilia usukani wa chama hicho, ndipo Mutharika akaamua kuunda chama chake kipya akiwa Ikulu, chama cha DPP. Lengo lilikuwa ni kufanya mabadiliko bila kuingiliwa na chama chake cha zamani, UDF,  kilichomuweka madarakani.

Kwa namna ninavyouona mwenendo wa kampeni za Magufuli, nauona uwepo wa kitu cha aina hiyo ya Bingu wa Mutharika. Sababu anayoyasema na kuyaonesha Magufuli naona kwamba yanakinzana kabisa na yale ya chama chake. Yeye na chama chake wanacheza ngoma mbili tofauti kabisa.

Mfano tumemuona Magufuli akicheza sarakasi katika maeneo mbalimbali ya kampeni ikiwa ni pamoja na kupiga “pushups” jukwaani. Wakati mwingine ameamua kutumia wito wa Chadema wa “people’s”! 

Sidhani kama mambo hayo yamo kweli Ilani ya uchaguzi ya CCM. Ni mambo ambayo yeye Magufuli kaamua kuyatumia baada ya kuchoshwa na yale ya CCM ambayo miaka nendarudi yametumiwa na chama hicho bila kuonyesha tija yoyote.

Kinachonipa imani hiyo ya kwamba si ajabu Magufuli akayafanya kweli mabadiliko yasiyotegemewa na yeyote, hasa ndani ya CCM, ni ile kauli yake ya kwamba yeye sio mwanasiasa. Anasema yeye ni mtu wa kazi tu.

Kwa maana hiyo mabadiliko hayo anayoyasema yanaweza yakawa ni ya kuipumzisha CCM akishaingia Ikulu, kama hilo litakuwa limewezekana, jambo ambalo ndilo wapinzani wote wanalitaka. Sababu Magufuli haonyeshi kupambana na wapinzani isipokuwa anapambana na chama chake.

 

[email protected]

0784 989512

By Jamhuri