Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na viongozi wa kampuni ya Total ambayo ni mwekezaji mkubwa wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania na kuwahakikishia kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kwa kampuni hiyo na washirika wengine katika ujenzi wa mradi huo.

Viongozi wa Total waliokutana na Mhe. Rais Magufuli leo tarehe 05 Desemba, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Rais wa masoko na huduma Bw. Momar Nguer, Rais wa Total Afrika Bw. Stanislas Mittelman, Makamu wa Rais wa Total wa Afrika ya Kati na Afrika Mashariki Bw. Jean Christian Bergeron na Mkurugenzi Mtendaji Total Tanzania Bw. Tarik Moufaddal.

Mhe. Rais Magufuli ameitaka Total kuharakisha ujenzi wa bomba hilo uliopangwa kuanza mwezi ujao na kukamilisha mapema hata kabla ya mwaka 2020 uliopangwa ili wananchi wa Tanzania na Uganda waanze kunufaika na mafuta hayo.

Naye Momar Nguer ambaye ndio wanaojenga bomba hilo amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na rushwa jambo lililosaidia kuimarisha mazingira ya uwekezaji na amemuhakikishia kuwa Total ipo tayari kufanya kazi bega kwa bega na Tanzania katika jukumu la utafiti wa mafuta katika maeneo yote yaliyotajwa.

By Jamhuri