Maisha bila maadui hayana maana (2)

Kutokusamehe kunaweza kukuangamiza wewe binafsi; kucheua ubaya uliotendewa, kulea uchungu, ni kudonoa kwenye donda lililo wazi na kukataa kuliruhusu lipone.

Kuendelea kwetu kucheua kukwazika, kubaki kwetu katika uchungu nafsini mwetu, mawazo yaliyojaa chuki, kutaka kwetu kulipa kisasi, hakumuumizi kabisa mtu mwingine aliyetutesa na hakutuletei sisi jema lolote zaidi ya kutufanya sisi tuharibikiwe milele.

Mawazo haya hufanya nafsi zetu zinywee (hivyo kunena mabaya na yasiyostahili) na kutufanya sisi tusifanane na lengo la kuumbwa kwetu.

Kutosamehe, kucheua maumivu na kulea uchungu kwa kukataa kutii, huleta matokeo mabaya zaidi kwa roho za watu ambao walikwisha kuteseka sana. Ingawa chuki inaweza kutupa aina ya nguvu ya ghafla, kadiri muda unavyokwenda inabadilika kuwa nguvu inayopambana na mwenye chuki. Kusamehe mara zote ni njia pekee ya kumaliza deni.

Ben Carson alisema haya kuhusu msamaha; wazo si kwamba sisi tumesamehewa, kwa hiyo tunatakiwa kusamehe. Lakini kwamba Mungu mwenyewe katika Kristo ametusamehe, kwa hiyo deni letu halipimiki.

Haijalishi ni ubaya mkubwa kiasi gani tuliofanyiwa, ni kidogo ukilinganisha na uovu tuliofanya mbele ya uso wa Mungu. Pamoja na hayo, Mungu katika Kristo akatusamehe sisi.

Watu wengi si kwamba ni wao tu wanakosewa sana, sisi si waathirika pekee. Lakini sisi pia tunawakosea wengine, pia tunawakwaza wengine.

Katika ulimwengu halisi kusamehe ni njia ya maisha unapomuumiza rafiki wa karibu kwa njia ya kumsema isivyo sahihi au kwa tendo (na sisi sote hufanya hivyo), rafiki yetu wa karibu ataumia na kuachilia.

Kwa hiyo, kufuta deni na kuachilia ni njia ya maisha. Maisha yasingewezekana kama watu wasingekuwa wanasameheana kila wakati.

Kutokusamehe ni uchaguzi, kama vile ambavyo kusamehe ni uchaguzi. Tunabagua kuhusu nani tumsamehe na nini tusamehe.

Tunasamehe tu maumivu kidogo na wale waliokosewa na watu wa karibu nao. Hata hivyo, Yesu hakutupa hiari katika kuchagua maumivu au watu ambao tunatakiwa kuwasamehe.

Tumefundishwa kusamehe hata saba mara sabini. Tunatakiwa kuwapenda adui zetu, si tu wale wanaotupenda sisi.

Iwapo unataka msamaha wa Mungu na wewe unashindwa kumsamehe anayehitaji msamaha kidogo, sahau kuhusu msamaha unaotaka.

Kumbuka kwamba hakuna muda wa ziada. Muda ulio nao ni dhamana tu. Hakuna anayeifahamu kesho yake ikoje, yawezekana kifurushi chako cha kuishi hapa duniani kiko ukingoni.

Siku uliyonayo ni leo. Itumie vizuri leo yako. Kama kuna mtu hamuelewani, mmefarakana sameheana naye leo. Kama kuna mtu unatamani kumwambia jinsi gani unampenda mwambie leo. Kama unatamani kuungama, ungama leo.

Wewe hauna kesho yako, aliye na kesho yako ni Mwenyezi Mungu pekee. Mafanikio bora na yenye ushindi ni kuishi kwa kufuata maagizo ya Mwenyezi Mungu kupitia imani yako.

Uwezo wa kuubadilisha ulimwengu huu ni kwa njia ya sala. Katika sala kila kitu kinawezekana, katika sala tunakutana na Mungu aliyeumba sayari, nyota na vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.

Katika sala tunakutana na Mungu aliyetuumba. Katika sala tunakutana na tumaini kuu ambalo kila mmoja anatamani kuliona baada ya maisha yake ya hapa duniani.

Powhatten James alipata kusema: “Mtu wa Mungu anapaswa kuwa na utambuzi kuhusu mambo ya kiroho. Hana budi kuwa na uwezo wa kuona milima iliyojaa farasi na magari ya moto.”

Hana budi kuwa na uwezo wa kufasiri yale ambayo Mungu aliandika kwa kidole chake katika dhamiri na kufasiri alama za nyakati zilizo na maana za kiroho.

Hana budi kuwa na uwezo wa kuwavuta watu kwenye sehemu za utulivu ili kuacha kuangalia mambo ya kidunia na kuelekeza mawazo yao kuona utukufu wa kiroho wa Mungu.