Malezi ya watoto ni mtihani. Maisha ya mtoto ni kama karatasi nyeupe ambapo kila mpita njia anaacha alama. Kwa msingi huo malezi ya watoto ni mtihani, maana kila mpita njia anaweza kuacha alama hasi au alama chanya. Kusema kweli anayetoka kipindi cha utoto anastahili pongezi.

Socrates – mwanafalsafa wa Ugiriki aliwaambia watu wa Athens: “Kwa nini mnasugua kila jiwe (kila aina ya madini) ili kukusanya mali na kutowajali watoto wenu ambao mtawaachia mali hiyo yote?”

Tunachokisoma katika maneno hayo ni kuwa baadhi ya wazazi wanatumia muda mwingi kutafuta mali ambayo watawarithisha watoto ambao hawakuwa na muda mwingi wa kuwafundisha namna ya kuitunza na kuitumia vizuri. 

Kuna mifano mingi ambayo inaonyesha malezi ya watoto ni mtihani. Kuna mtoto ambaye aliambiwa na wazazi wake: “Bisha hodi kwenye mlango wowote kabla ya kufungua.”

Siku moja mtoto alitumwa kuchukua soda kutoka kwenye friji. Jambo la kushangaza alichelewa. Mama yake alipokwenda kuangalia alikuta anabisha hodi kwenye mlango mdogo wa friji.

Kutokana na kisa hiki malezi ya watoto ni mtihani. Kuna mtoto aliyeweka maneno haya kwenye mlango wa chumba cha wazazi wake: “Wapendwa wazazi, kuwa wema kwa watoto wenu nao wakati ujao watakuwa wema kwenu.” Maneno hayo yanabainisha ukweli kuwa ni zamu kwa zamu; wazazi kuwasaidia watoto na watoto kuwasaidia wazazi.

Mtoto ni zawadi ya Mungu kwa wazazi. Mtoto ni mwanafunzi, anajifunza kwa wazazi. Methali ya Kiswahili inasema: “Mtoto akibebwa hutazama kisogo cha mama yake.” Ni kama methali ya Nigeria isemayo: “Ndama hutazama mdomo wa mama yake wakati mama anatafuna nyasi.”

Mtoto ni mlelewa. Wazazi ni mfano wa kwanza wa kuigwa kwa watoto. Wazazi ni walimu wa kwanza. Jambo ambalo mtoto analisema saa sita mchana huenda amelisikia kwa wazazi saa sita za usiku.

Ni wajibu wa wazazi kuwa makini, wanasema nini, wanatenda nini. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Samaki mkunje angali mbichi. Hizo zote ni methali za Tanzania zikibainisha malezi ya watoto ni mtihani.

Watoto wape “dozi” ya upendo. Upendo wa mama na baba ni muhimu sana. Ni vizuri watoto kuonja upendo wa baba na mama. Watoto wenye mama mkaa pweke ni vizuri wakati wa likizo wakaenda ujombani ili kuziba pengo la kutokuwepo baba kama mjomba yupo.

Kuna swali ambalo liliulizwa na mtoto kwenye gazeti. Mpendwa shangazi, tatizo langu ni mama yangu. Ananidekeza. Anapokasirika na kuniadhibu, baadaye ananiomba msamaha.

Kwa nini aniombe msamaha wakati nimekosea na ameniadhibu? Ni mimi Chausiku. Shangazi alijibu: “Mama yako kama kina mama wengine, anaogopa kuwa hautampenda kwa sababu amekuadhibu. (Kwa mtazamo huo amekosea).

Hakuna mtoto anayemchukia mzazi kwa vile amempa adhabu. Adhabu ni uthibitisho wa upendo. Watoto mjue hilo. Natamani wazazi wengi wangetoa adhabu.” Mzazi asimbembeleze mno mtoto. Kwa ufupi mzazi asiogope kuwa ‘adui’ wa mtoto wake katika kumlea vema na kumtakia maisha mazuri mbeleni.

Please follow and like us:
Pin Share