Ni muhimu kutahadharishana kuhusu jambo hili. Kitaalamu jambo hili huitwa ‘adverse possession.’ Ni kanuni ya kisheria. Ni wakati ambapo mtu au watu wanavamia ardhi yako, lakini baada ya muda wanahesabika kuwa ni wamiliki halali. Na wanatambuliwa hivyo na sheria na wewe mmiliki halisi unageuka kuwa mvamizi.

Lakini hoja kubwa hapa si lazima mtu awe mvamizi. Anaweza kuwa mpangaji au mtu anayekulindia eneo. Lengo la hoja ni kutaka kuwatahadharisha wamiliki wa ardhi hasa wale wanaowaacha watu wawalindie maeneo au wanaowapa watu kukaa bure bila utaratibu maalumu. Ifahamike kuwa si kosa mtu kukulindia eneo na wala si kosa mtu kukaa bure kwenye eneo lako, ila ni kosa tena kubwa kufanya hivyo bila utaratibu maalumu wa kisheria. Na hapa ndipo kugeukana kunapokuja.

Ni rahisi huyo mtu kukugeuka na wapo watu wamegeukwa, na kwa kutumia kanuni hii na wameruhusiwa na mahakama kuwa wamiliki halali.

Kawaida sheria zetu za ardhi Tanzania zinatambua aina au namna mbalimbali ambazo mtu anaweza kupitia katika kupata ardhi kihalali. Moja ni kununua; pili, kupewa zawadi; tatu, kurithi; nne, kutwaa eneo lisilo na mwenyewe; tano, ni hii ya kuingia katika eneo kama mvamizi ama vinginevyo na baadaye ukabadilika na kuwa mmiliki.

Namna zote hizi ni za kisheria na zinakubalika kama njia halali za kupata na kumiliki ardhi.

1. Wakati ambao mvamizi atatambulika kama mmiliki

Wote tunajua kuwa mvamizi ni yule mtu ambaye ameingia kiharamu katika ardhi ya mtu mwingine. Ardhi inaweza kuwa nyumba, kiwanja au shamba na vile vilivyomo. Kuingia kiharamu ni kuingia bila ridhaa ya mmiliki na bila sababu za kisheria.

Lakini hata mpangaji au mtu uliyemuacha akulindie eneo anaweza kuhesabika kama mvamizi katika kanuni hii iwapo wewe mmiliki utakosa ushahidi wa maandishi au vinginevyo kuthibitisha kuwa ni mpangaji au ni mtu uliyemuacha akulindie eneo.

Kesi ya Buckinghamshire cc v Moran [1990] Ch 623 (CA) imeeleza misingi ya kanuni hii ya mvamizi kugeuka kuwa mmiliki. Kadhalika Mahakama ya Rufaa katika rufaa namba 193/2016 kati ya The Registered Trustee of the Holy Spirit Sisters Tanzania VS January Kamili Shayo na wengine 136 nayo imeeleza jambo hili na kuweka misingi yake.

Kesi hizi mbili zinaeleza kuwa ikiwa mtu ataingia na kukaa  kwenye ardhi yako, iwe nyumba, kiwanja, shamba au vinginevyo kwa kipindi ambacho kinazidi miaka 12, basi mtu huyo mvamizi atageuka kutoka hadhi yake ya uvamizi na kuwa mmiliki halali.

Kwa msingi huu, kumbe si salama mtu au watu kuendelea kukaa katika eneo lako bila taratibu maalumu  zinazotambuliwa na sheria.

Hata hivyo, hoja ya kukaa zaidi ya miaka 12 pekee haitoshi kuthibitisha umiliki, bali pia mvamizi athibitishe pia kuwa wakati anaingia hakuwa na ridhaa yoyote kutoka kwa mmiliki; mfano, hakuomba kukaa au kutumia hiyo ardhi au hakuwa mpangaji. Pia athibitishe kuwa hakuwa na haki yoyote kukaa humo. Mfano, si mtoto au mke wa mmiliki au hakuwa na haki nyingine, nk.

Tunachotaka kusisitiza ni kuwa tuwe makini na watu ambao wanakaa kwenye maeneo yetu kwa muda mrefu na hata wapangaji wa aina hiyo pia.

2. Namna ya kuweka ardhi yako salama kuepuka kanuni hii

Kwanza, yeyote utakayempa ardhi yako kwa ajili ya kulima, kufuga, kuishi, kupanga au shughuli nyingine yoyote, hakikisha mnaandika na kusaini na kuweka picha ikiwezekana na mashahidi. 

Mara nyingi walinzi wa maeneo hasa mashamba makubwa na viwanja wamekuwa wakigeuka. Unaweza kudhani si rahisi kufanyiwa hivyo na ni masihara, lakini waliokutwa na haya wanajua ninazungumzia nini.

Wapo wengi wametumia kanuni hii kuchukua maeneo ya watu na muda huo kama hakuna maandishi mtu anakukataa kuwa hukumruhusu aingie, bali aliingia mwenyewe baada ya kukuta hamna mtu.

Pili, ni muhimu kuyawekea uzio maeneo yetu ili kuepuka wavamizi. Kadhalika kuweka vibao hasa kwenye mashamba vinavyokataza uvamizi, kwa mfano kibao kinaweza kuandikwa: ‘Hairuhusiwi kuingia eneo hili bila kibali maalumu’ nk.

Please follow and like us:
Pin Share