Nazungumzia Serikali inayoendesha mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Nionavyo mimi ni mzaha mtupu. Ni sawa na kukumbuka kujifunika shuka wakati kumeshakucha.

Tayari vijana wetu wengi wameharibika ndani na nje ya nchi yetu. Tayari Jina la Tanzania limechafuka sana kama kituo kikuu cha dawa za kulevya barani Afrika.

 

Na tayari tunalaumiwa kwa kugeuza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jina la Baba wa Taifa, kuwa uchochoro wa kupitisha dawa za kulevya. Tunarudi nyuma kabla  Amina Chifupa hajaondoka duniani mwaka 2007, alitoa orodha ya watu waliokuwa wakijishughulisha na biashara ya dawa za kulevya. Lakini  haikufanyiwa kazi.

 

Kabla ya hapo, mwaka 2006 Askofu William Mwamafango wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste Tanzania, Kanda ya Mbeya, alimpelekea Rais orodha ya watu wapatao 58 waliokuwa wakijihusisha na dawa za kulenya. Rais alikiri kupokea orodha hiyo lakini hakuifanyia kazi. Hapa mtu hakosi kujiuliza maswali mawili.

 

Kwanza, swali la msingi kwa nini wakati wote huo orodha zote za watu waliokuwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya hazikufanyiwa kazi, si kweli kuwa mapambano haya tunayoyaendesha dhidi ya dawa  za kulevya ni mzaha mtupu?

 

Pili, nani alizuia wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuwachukulia hatua Rais ama Jeshi la Polisi au Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya? Sasa tumeletewa orodha ya wauza ‘unga’ 255.

 

Kabla hatujaletewa hiyo orodha tuliambiwa kuwa wanaojishughulisha na biashara ya dawa za kulevya ni viongozi  wakubwa,  watoto wa wakubwa, viongozi wa siasa, wabunge, viongozi wa dini na wafanyabiashara wakubwa.

 

Sisi sote tunayajua majina ya wakubwa, tunayajua majina ya watoto wa wakubwa na tunayajua majina ya wabunge. Tumeyaona mangapi katika orodha tuliyoletewa? Kama huku si kuendesha mapambano haya kwa mzaha ni kitu gani?

 

Halafu kauli ya Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamanda Godfrey Nzowa, ukitaka kusema ukweli ni kichekesho kitupu na ni ushahidi mwingine usioweza kutiliwa shaka unaothibitisha jinsi Serikali inavyoendesha mapambano haya ya kidhihaka.

 

Nzowa anatwambia kuwa kuna watu ambao kitengo chake kimepeleka mahakamani ambako wamekuwa chini ya uangalizi wa Mahakama na Jeshi la Polisi. Eti wanatakiwa waripoti polisi kila wiki kutia saini kwenye kitabu maalum na kuthibitisha kuwa wamejirekebisha na wameacha tabia hiyo ya kuuza ‘unga’

Nasema hiki ni kichekesho.

 

Leo kuna vijana wetu wengi wanasota gerezani kama mahabusu kwa kukutwa na bangi. Hawa wametakiwa kuripoti polisi na kudai wenyewe mbele ya polisi kwamba wamejirekebisha na wameacha tabia hiyo ya kuuza ‘unga’; haki iko wapi? Kwamba huo ndiyo mwisho wa Tanzania kuwa soko kuu la dawa za kulevya barani Afrika? Hapana.

 

Huko nje vijana wetu wanakatwa shingo kwa kujihusisha na dawa za kulevya na wanaonusurika wanaswekwa gerezani. Hapa nyumbani wamewekwa kwenye uangalizi wa Mahakama na Polisi huku wakiendelea kuuza ‘unga’ wao.

 

Lakini pia kuna hisia au mawazo kuwa sehemu kubwa ya orodha ya watu 255 tuliyoletewa ni ya kupikwa. Kwanini watu hao waliochangia kwa kiasi kikubwa katika kuharibu jina la Tanzania na tabia za vijana wetu wapelekwe mahakamani kwa siri? Kwanini wasioneshwe mbele ya umma pale mahakamani?Tunafanya mzaha mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

 

Nionavyo mimi  wakati umefika kwa wanaharakati kuitisha na kuongoza maandamano ya kupinga jinsi Serikali inavyoshughulikia suala la dawa za kulevya, tunahitaji kujua majina ya mamba wanaojihusisha na dawa za kulevya si majina haya ya kenge watupu tulioletewa mwisho, sisi tunajua kuwa nchi yetu inafuata utawala wa sheria.

 

Katika utawala wa sheria kuna mgawanyiko wa madaraka, kwa ajili hiyo tuna kitengo cha kupambana na rushwa ambacho watu wake wamepewa na Rais madaraka ya kuendesha vita dhidi ya dawa za kulevya, lakini pamoja na ukweli huo Rais ana nafasi yake katika vita hivyo.

 

Rais hahitaji kuambiwa jinsi Taifa letu linavyoendelea kudhalilika duniani katika hali hii ya dawa za kulevya barani Afrika, kwa hivyo umma wa Tanzania unatazamia kumuona Rais akitumia nafasi ya hotuba zake mwisho wa mwezi kuzungumza kwa kirefu masuala ya dawa za kulevya.

 

Kama tujuavyo katika Afrika haishindikani kutoa sababu ya jambo lolote hata kama haina ukweli, kwa hivyo Rais avunje ukimya azungumzie dawa za kulevya.

1175 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!