NA WAKILI STEPHEN MALOSHA,

DAR ES SALAAM

UTATUZI WA MIGOGORO
Kuanzia kifungu cha 75 hadi 95 ni eneo linalohusu utatuzi wa migogoro, kwanza ni
kutumia majadiliano baadaye kutumia nguvu, rejea kifungu cha 80 na 81. Eneo la
mwisho ni utatuzi wa migogoro ya kikazi kupitia usululuhishi, uamuzi na Hukumu ya
Mahakama ya Kazi.
VYOMBO VYA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI SHERIA ZA KAZI
Kwa upande sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7/2004 zenyewe imejihusisha na uundaji wa
vyombo vya aina mbili, vyombo vya kiutawala na kimahakama, kazi ya vyombo vyote
ni kusimamia utekelezaji wa sheria hizi za kazi.
Vyombo vya kiutawala ni Kamishna wa Kazi, Bodi za Mishahara, Kamati ya Huduma
muhimu na Baraza Ushauri la Kazi.
Vyombo vya kimahakama ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi; na Mahakama ya Kazi.
Sheria hii inaeleza na kufafanua mamlaka na majukumu ya vyombo hivyo.
UTATUZI WA MIGOGORO MAHALA PA KAZI
Chini ya sheria hizi za kazi, zipo namna mbili za kusimamia utatuzi wa migogoro,
kuna vyombo vimewekwa kuzuia migogoro isitokee, na vile vilivyowekwa kutatua
migogoro ikitokea.

1) Vyombo vya kuzuia migogoro isitokee (dispute prevention):
Kwa mujibu wa kifungu cha 45 cha LIA Afisa wa Kazi amepewa mamlaka ya kufanya
ukaguzi mahala pa kazi juu ya ukiukwaji wa sheria na kutoa maelezo ikiwa ni pamoja
na kuwashitaki mahakamani waajiri wanaovunja sheria. Jukumu hilo pia wanafanya
OSHA kwenye eneo la afya na usalama.
Aidha chini ya kifungu cha 73 cha ELRA Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ina wajibu
wa kutoa elimu kwa wafanyakazi na waajiri kuhusu sheria za kazi na mahusiano bora
kazini.
2) Vyombo vya kutatua migogoro mahala pa kazi
* Majadiliano kazini baina ya mwajiri na chama cha wafanyakazi (collective barganing)
 Kamati za matawi ya chama cha wafanyakazi wakishirikiana na mwajiri (secrion
64 of ELRA)
 Kamati ya nidhamu.
 Kusikiliza manunguniko ya wafanyakazi kwa mujibu wa kanuni ya 2 ya
mwongozo ukurasa wa 79 GN.42/2007.
 Mabaraza ya wafanyakazi
3) Vyombo vinavyofanya kazi nje ya mahali pa kazi
 Tume ya Usuluhishi na uamuzi
 Mahakama ya Kazi
 Mahakama ya rufaa
MAMLAKA YA TUME YA USULUHISHI NA UAMUZI (JURISDICTION)
i. Mamlaka ya kifedha, hakuna ukomo wa kifedha, rejea Misc Act No.3/2010.
ii. Mamlaka ya kieneo, mgogoro utasikilizwa mahala mgogoro ulipotokea labda
Tume iwe imeagiza vinginevyo.
Mamlaka ya ki-maswala, Tume ina mamlaka kwa suala lolote la kikazi, rejea kufungu
cha 4 cha ELRA, na kifungu cha 88 kama kilivyorekebishwa na Act No. 8/2006

MAMLAKA YA MAHAKAMA YA KAZI
Mahakama Kuu haina ukomo wa kiwango cha Kifedha au kieneo au kimasuala katika
kusikiliza migogoro ya wafanyakazi lakini mgogoro yote lazima ianzie Tume. Kazi za
kila siku za Mahakama Kuu ya Kazi ni kupitia na kuangalia usahihi wa Tuzo za Tume
yaani (Revisionary Power) na kukazia uamuzi wa Tume (execution of awards). Hata
hivyo, Mahakama Kuu ina mamlaka ya kipekee kwenye kutafsiri sheria za kazi,
kusikiliza maombi ya zuio (injunction) na maombi ya tamko declaration).
MAMBO YANAYOWEZA KUFANYIWA MAREJEO NA MAHAKAMA YA
KAZI
Uamuzi (Tuzo) ya Arbitrator inaweza ikapingwa Mahakama Kuu ya kazi ndani ya siku
42 kwa sababu zifuatazo: –
• Arbitrator alifanya utovu wa nidhamu kwenye kufikia uamuzi
• Tuzo ilipatikana kwa njia zisizo halali, rejea kifungu cha 91 cha ELRTA.
• Kama Tuzo haieleweki (illogical),
Kama Tuzo ilifikiwa bila kuzingatia ushahidi uliotolewa au uamuzi umezingatiwa
ushahidi ambao haukutolewa.
• Uamuzi haukuzingatia sheria, mfano kuchukua ushahidi wa kusikia (hearsay).
KUPINGA UACHISHAJI USIO KUWA HALALI (UNFAIR
TERMINATION COMPLAINT)
Lalamiko hili linakuja kwa mujibu wa kifungu cha 88(i)(d) cha ELRA. Ni dhana ngeni
duniani kote, imeletwa na mwongozo wa Shirika la Kazi Duniani kupitia tangazo
namba 119, lengo ni kwanza kutambua kwamba mfanyakazi na mwajiri ni pande
zisizo na nguvu sawa, aidha kwamba ajira ni rasilimali sawa na rasilimali nyingine kwa
hiyo lazima ilindwe, ulinzi uliowekwa ni kuwa mfanyakazi ataachishwa kazi kama kuna
sababu ya kufaa, rejea kifungu cha 37 cha ELRA, sababu lazima itokane na utovu wa
nidhamu, kushindwa kufanya kazi kwa ugonjwa au kukosa uwezo, kushindwa
kuendana na mazingira na kupunguzwa kazi.
NAMNA YA MWAJIRI KUTHIBITISHA UWEPO WA KOSA LA UTOVU
WA NIDHAMU (MISCONDUCT)

Makosa ya Kinidhamu: Kanuni GN 42/2007 imetoa mfano wa makosa ya kinidhamu,
orodha hiyo sio kamili kwani makosa yatategemea aina ya kanuni na sera ya mwajiri,
rejea ukurasa wa 74 wa GN 42/2007 kuhusu makosa mbalimbali yanayoweza kutokea
mahala pa kazi.
MZIGO WA KUTHIBITISHA
Kwa mujibu wa kifungu cha 39 cha ELRA mwajiri ana wajibu wa kuthibitisha uwepo
wa kosa la kinidhamu. Kosa linapande 2 yaani kosa lenyewe na utaratibu wa kutambua
uwepo wa kosa.
NAMNA YA KUTHIBITISHA UWEPO WA SABABU
Kwa mujibu wa kifungu cha 37(2)(a)(b) ili mfanyakazi aachishwe lazima kuwepo
sababu halali na ya kufaa. Mwajiri utathibitisha uwepo wa sababu hiyo kwa kuonyesha
kwamba kanuni fulani ya kazi ilivunjwa, kanuni hiyo yaweza kutokana na sera ya
mwajiri, sheria za nchi na kanuni za jumla zinazokubalika (implied duties) au mazoea
(customs and traditions), rejea kanini ya 12(1) ya GN.42/2007.
Aidha ili kosa lithibitike kutosheleza kuachisha, matakwa yafuatayo lazima yazingatiwe:
⁻ Mfanyakazi alivunja hiyo kanuni
⁻ Mfanyakazi aliijua hiyo kanuni
⁻ Kanuni hiyo ni ya kufaa
⁻ Kanuni hiyo inatumika sawa kwa watu wote
⁻ Kosa la kwanza sio lazima limfukuzishe kazi mfanyakazi
⁻ Mazingira ya kosa lilivyotendeka
⁻ Rekodi ya nyuma ya mfanyakazi ikoje
⁻ Majukumu ya kifamilia ya mfanyakazi

AMNA YA KUTATHMINI ILI KUONA KAMA KWELI KOSA
LILITENDEKA

Kwa msingi wa kutomfanya mwajiri awe hakimu kwenye kesi yake mwenyewe,
anatakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 37(2)(c) cha ELRA kama kilivyofafanuliwa na
kanuni ya 13 ya GN.42/2007 kuunda kamati ya nidhamu kumsaidia kuchunguza
kupendekeza juu ya uwepo wa tuhuma (kosa ama la).
Katika kutekeleza kanuni hii mwajiri ametakiwa afanya yafuatayo: –
⁻ Uchunguzi (Investigation)
⁻ Akiona kuna tuhuma aandae charge – sheet
⁻ Ampatie mfanyakazi chaji si chini ya masaa 48 kujiandaa kuja kwenye kamati,
⁻ Aje na mwakilishi
⁻ Mfanyakazi aruhusiwe kuhoji mashahidi.
⁻ Mfanyakazi aruhusiwe kupeleka ushahidi wake.
⁻ Mfanyakazi atoe utetezi kuhusu adhabu (mitigation)
⁻ Mwenyekiti wa kamati awe kiongozi wa juu
⁻ Baada ya uamuzi wa mwajiri kufuatia mapendekezo ya kamati akate rufaa mamlaka
ya juu.
⁻Mwajiri hawezi kutamka kuwa kosa la nidhamu lilifanyika bila kuunda kamati ya
kumshauri
TATHMINI YA KOSA LA KUSHINDWA KUFANYA KAZI (POOR
PERFORMANCE)
Arbitrator atatakiwa aangalie endapo mfanyakazi alipewa malengo/viwango, akavijua,
akashindwa kutekeleza, endapo viwango vinafaa na endapo alipewa fursa ya kufikia
viwango hivyo. Aidha, kama alipewa miongozo au mafunzo husika, je amepewa muda
ajirekebishe, kama kabla ya kuachishwa alipwe fursa ya kujitetea akiwa na mwakilishi
rejea kanuni ya 17 – 18 ya GN 42/2007.
TATHMINI YA KUACHISHA KAZI KWA SABABU YA UGONJWA
Ili mfanyakazi aachishwe kwa ugonjwa au kuumia mwajiri anatakiwa azingatie
yafuatayo; –

• Sababu ya kuumia.
• Kiwango cha kuumia / ulemavu.
• Uwezo wa kuvumilia mfanyakazi.
Kama lazima aachishwe kazi atafuata kwanza mbadala kwa kumpa kazi nyingine
ikishindikana anaweza kuachishwa kwa kuzingatia ushauri wa daktari.
TAHMINI YA UACHISHAJI KWA SABABU ZA KIUCHUMI
(OPERATIONAL NEED OF THE EMPLOYER)
Mwajiri anaweza kupunguza wafanyakazi ama kufunga kabisa shughuli kama ana
sababu ya kufaa, sababu ambayo lazima itokane na sababu za kiuchumi, mabadiliko ya
teknolojia ama mabadiliko ya muundo. Hata hivyo, ili uachishaji uwe halali lazima
sababu ithibitike, na kuwa imeshindikana kuzuia ‘zoezi’ la kupunguza.
NAFUU ZINAZOTOLEWA KAMA ITABAINIKA MFANYAKAZI
ALIACHISHWA ISIVYO HALALI
Sheria imetoa nafuu kuu tatu kama itabainika mfanyakazi aliachishwa isivyo halali.
Nafuu hizo ni kama ifuatavyo: –
• Kurudishwa kazini
• Kupewa kazi nyingine
• Kulipwa fidia, fidia siyo chini ya mishahara ya miezi 12
KUACHISHWA KAZI KUTOKANA NA UVUNJWAJI WA MKATABA
(BREACH OF CONTRACT)
Dhana ya mkataba kuvunjwa inahusu pande zote za uhusiano, mwajiri anaweza
akafanya vitendo vya kuvunja mkataba na mfanyakazi naye akavunjwa mkataba. Kwa
mujibu wa kifungu cha 88 cha ELRA kama kilivyorekebishwa, wafanyakazi na waajiri
wa mkataba waweza wakapinga uvunjwaji wa mkataba wa aina yoyote, kupinga
kuvunjwa mkataba kunafanana kimsingi na kupinga kuachishwa, tofauti iliyopo ni
kwenye nafuu, mfanyakazi wa mkataba wa muda maalumu huwezi akaomba kurudi
kazini bali atadai fidia ya muda uliosalia wa mkataba.
UVUNJAJI WA MKATABA UNAOWEZA KUFANYWA NA MWAJIRI

• Kusitisha mkataba wa ajira wa muda maalum (fixed term contract)kabla ya muda
kuisha bila sababu na utaratibu kufuatwa.
• Kusitishwa mkataba wa kazi maalumi bila sababu ya kufaa na utaratibu kufuatwa
(specified task)
• Kutolipa mshahara ama marupurupu ya mkataba rejea kanuni ya 6(4)GN 42/2007
• Kusimamishwa kazi kusiko halali (Unlawful suspension).
• Kushushwa cheo (demotion) bila sababu au makubaliano au kushusha mshahara.
• Kusitisha utekelezaji wa mkataba kabla ya ajira kuanza (anticipatory breach of
contract).
• Mkataba kuingia katika hatua ya kushindwa kutekelezeka (supervening impossibility
or frustraction of contract) mfano ugonjwa wa muda mrefu.
• Kubadilisha mkataba bila ridhaa ya mfanyakazi. (Unilateral variation contract).
• Kukata mshahara bila sababu ya kufaa.
• Tathimini ya utendaji isiyo halali (unfair appraisal)
UVUNJAJI WA MKATABA UNAOWEZA KUFANYWA NA MFANYAKAZI
• Kuachishwa kazi bila sababu ya kufaa kabla ya mkataba wa muda maalum (fixed
term contract) kwisha muda.
• Kutomaliza kazi maalum (specific task bila sababu ya kufaa.
• Kuharibu mali za mwajiri (damage to property).
• Mgomo usio halali na uvunjaji mkataba kwa mfanyakazi.
• Mfanyakazi kufanya kazi kwa mwajiri mwingine wakati bado mkataba haujaisha kwa
mwajiri mwingine.
• Mfanyakazi kuacha kazi bila kutoa taarifa (notisi).
NAFUU (REMEDIES) KWA UVUNJAJI MKATABA

Nafuu kadhaa zinatolewa na sheria yetu kwa uvunjaji wa mkataba, nafuu zipo katika
sheria ya mikataba sura 433 (R.E. 2002) Kifungu cha 73 na uamuzi wa Mahakama ya
Kazi.
• Uvunjaji wa mkataba wa muda maalum (fixed term contract) nafuu yake ni kulipwa
muda wa mkataba uliosalia.
• Mfanyakazi akiacha kazi na kusababisha madhara atalipia gharama ya kumchukua
mfanyakazi mbadala.
* Gharama nyingine mfano mateso, majonzi na uchungu wa kuvunjiwa mkataba
zinalipwa zikithibitika.
* Amri ya kurudishiwa makato, kulipwa mshahara n.k
Kuomba Mahakama kuzuia uvunjaji wa mkataba (injuction) rejea kifungu cha 94(i)(ii)
cha ELRA.
Kuomba tamko (declaration) kuwa kitendo anachotaka kutanya (mfanyakazi au
mwajiri) ni uvunjwaji wa mkataba, rejea kifungu cha 94(i) (f)(i) of ELRA.
• Mkataba wowote wa kazi ukiwamo wa muda maalumu unatakiwa usitishwe baada ya
mfanyakazi kupewa haki ya kusikilizwa.
• Mwajiri kudai alipwe hasara inayotokana na kuvunjwa mkataba (counter claim)

MAMBO MENGINE MUHIMU KATIKA SHERIA ZA KAZI
MIKATABA YA KAZI ILIYO BATILI
Ifuatayo, pamoja na mengine ni mikataba batili (void contracts).
1) Mkataba kumzuia mfanyakazi asifanye kazi inayofanana na ya mwajiri au
kufanya kazi kwa mshindani wa kibiashara baada ya kuacha kazi (contract in restraint
of trade).
2) Kufanya kazi za kuajiriwa hapa nchini bila ‘work permit class B”
LALAMIKO KUHUSU MADHIRA (TORTIOUS LIABILITY)

Kutokana na marekebisho ya Sheria Na.6/2004 yaliyofanywa kupitia Misc, Act
No.8/2006, sasa wafanyakazi na waajiri wanaweza wakadai fidia itokanayo na madhira;
neno Tort limetafsiriwa na mwanazuoni Dk. Kapour kuwa ni Breach of a duty fixed by
law to all persons generally which is not exclusively a breach of contract, pg.7, (kitabu cha law of
Torts, 1986.
Madhira yafuatayo yanaweza kudaiwa na mfanyakazi na fidia kutolewa. Tayari eneo
hili limeshuhudia kesi nyingi, mfano ni zifuatazo; Tort ya mtu kupigwa akiwa kazini
(battery) huyu alikuwa ni HR alipigwa na kuumizwa (battery).
Tort ya mtu kuchafuliwa jina lake (defamation) mfano kuna mfanyakazi alichafuliwa
kwa maandishi (libel) kwa kuambiwa ana pepo la ngono uzinzi, anajihusisha na
masuala ya ngono sehemu ya kazi, Tume ilimpatia fidia ya Sh milioni 70 na kuamuru
arudishwe kazini.

DHANA YA KUFUKUZWA KAZI KWA KUFANYA MAZINGIRA YA KAZI
KUWA MAGUMU(WORKING RELATIONSHIP INTOLERABLE)
Mazingira kama kumlazimisha mtu kufanya kazi saa 48 au zaidi ya 24 mfululizo bila
sababu ni sawa na kufanya mtu aone mazingira magumu ili aache kazi. Mazingira
kama hayo yakitokea na mfanyakazi akalazimika kuacha kazi, basi uachishaji huo
utakuwa umefanywa na mwajiri na utakuwa sio halali; rejea kufungu cha 3(a)(ii) cha
ELRA.
DHANA YA MIGOMO KWA WAFANYAKAZI NA KUFUNGIA NJE
WAFANYAKAZI (STRIKE AND LOCKOUT)
Sheria inaruhusu kwa mujibu wa kifungu cha 75 wafanyakazi kugoma kufanya kazi na
waajiri kuwafungia nje wafanyakazi ili kuweka shinikizo la kukubaliwa kwa jambo
linalojadiliwa.
Hata hivyo, mgomo au kufungia nje wafanyakazi kumeruhusiwa kisheria kama
mgogoro unakuwa unaohusu mgogoro wa maslahi siyo unahusu haki. Mgogoro wa
haki unatakiwa uende ukaamuliwa na vyombo vya kimahakama.
DHANA YA KUREJEREWA MKATABA (RENEWAL OF CONTRACT BY
DEFAULT NA EXPECTATION TO TENEWAL OF CONTRACT

Mkataba wa kazi wa muda maalum (fixed term contract) unaweza ukarejelewa kwa
namna tatu:
• Renewal, hii ni kwa makubaliano, haki za mkataba wa kwanmza zinakuwa
zimelipwa au kutnzwa na maktaba unaanza upya.
• Renewal by default, mkataba wa awali umeisha lakini pande bila kukubaliana
wanaendelea na kazi: mkataba huu utachukua masharti ya ule wa kwanza, kanuni ya
4(3) GN 42/2007
Expectation for renewal, mfanyakazi anaweza akawa ametumainishwa kuendelea na
mkataba wake kabla ya ule wa awali haujaisha sasa kama mwajiri atabadilisha mawazo
na kutamka kuwa hataendelea na mkataba basi hiyo itakuwa “unfair termination” na
mfanyakazi atathibitisha atasthili fidia ya mishahara 12, rejea kifungu cha 36 cha
ELTRA, wajibu wa kuthibitisha uwepo wa matumaini upo kwa mfanyakazi
SABABU NYINGINE ZA KUPUNGUZA WAFANYAKAZI
Mfanyakazi ambaye wateja mahala pa kazi hawamtaki kwa sababu ya kutokuendana
nao kwa tabia zake au sababu nyingine muhimu, mfanyakazi huyu atapungzwa kazi
kwa “similar needs of employer”.
HAKI ZA VYAMA VYA WAFANYAKAZI
Vyama vya wafanyakazi zilivyosajiliwa vina haki ya kutetea wanachama na wafanyakazi
kwa ujumla. Katika kutekeleza haki ya kutetea vinaruhusiwa na sheria kuingia mahala
pa kazi kwa ajili ya kutafuta wanachama, kufanya majadiliano na mwajiri kuhusu
maslahi ya wafanyakazi kupitia vikao, kukusanya michango kutoka kwa wancahama
wao kupitia kwa mwajiri, viongozi kupewa muda wa kufanya masuala ya chama chao
wakati wa kazi.
Kufunga mikataba ya hali bora na mwajiri kurejea kifungu cha 60 – 71 cha ELRA.
UHAMISHO
Uhamisho wa mtumishi toka shemu moja kwenda sehemu nyingine inatakiwa
ufanywe baada ya majadiliano naye ili kuzuia madhara kwa mfanyakazi na familia.
MALIPO YA OVERTIME

Suala la malipo ya ‘overtime’ limekuwa kwa muda mrefu linaloleta usumbufu katika
kutolea uamuzi pale linapofika kwenye Tume au Mahakama. Utata umekuwa unaletwa
na kukosekana ushahidi kutokana na madai mengine kuwa ya muda mrefu.

MALIPO YA KIINUA MGONGO
Kwa mujibu wa marekebisho ya sheria, misc. amendment Act No.2/2010 wafanyakazi
wa mkataba wa muda maalumu hawastahili kulipwa kiinua mgongo baada ya mkataba
wao kukoma au mtu kustaafu kwa umri.
Makala hii imeandaliwa na Stephen Malosha & Valerian Msola (Mawakili) –
MALOSHA & MSOLA ADVOCATES, wa S.L.P 6276 Dar es Salaam.
Anapatikana kupitia simu: 0767722298 / 0718544555

3873 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!