Siku za karibuni hapa Dar es Salaam, jiji letu kioo cha Taifa hili, kumeonekana mabasi kadhaa yaliyoandikwa “INDIAN SCHOOL BUS” na mengine “YEMEN SCHOOL BUS”.
 Baadhi yetu walimu wa zamani tumeshtuka na kufikiria mbali kule tulikotoka enzi za ukoloni. Bado tukawa na maswali zipo kweli shule za mataifa hayo?


  Tukaja kugundua kumbe kweli hapa Dar es Salaam kuna shule maeneo ya Kurasini nyuma ya viwanja vya Saba Saba (au kwenye viwanja vya maonesho vya Mwalimu Nyerere). Shule hii ni ya Wahindi na ndiyo yenye hayo mabasi ya Indian School Buses. Inasomesha watoto Wahindi kutoka sehemu zote za jiji hili hapo.
  Papo hapo maeneo ya Chang'ombe kuna shule ya Waarabu wa asili ya Yemen nayo ina vibasi vyake vimeandikwa Yemeni School Buses. Hizo ni shule za mataifa. Aidha hapa nchini zipo shule kadhaa zinazofundisha kwa lugha ya Kiingereza. Hizi zinajulikana sana kama ENGLISH MEDIUM SCHOOLS. Aina zote hizo za shule zinabagua Watanzania. Baba wa Taifa aliziita shule za matabaka (racial schools)).


  Mshtuko wangu ni kuona Taifa letu kupitia Wizara yake ya Elimu tumeruhusu katika nchi hii kurejeshwa kwa aina za shule wakati wa ukoloni tulizitambua kama shule za matabaka au ubaguzi wa rangi na wa dini.
 Mara baada ya kupata Uhuru, utaratibu wa shule namna hii ulifutwa kwa sheria ya Elimu ya 1969 na hatimaye shule zote za mataifa na za madhehebu za dini katika nchi yetu ya Tanganyika zilitaifishwa na zikawa ni shule kwa ajili ya watoto wote na zikawekwa chini ya usimamizi wa Serikali. Mkurugenzi wa Elimu alitawala mfumo mzima wa elimu katika Taifa.


   Bado sielewi hizi shule za mataifa “Indian School” na “Yemeni School” zimewezaje kusajiliwa kwa mfumo ule wa matabaka! Ni vizuri wasomaji vijana wakajua mimi mzee naongelea kitu gani maana wakati zilipotumika shule za matabaka, hawa vijana hawakuwapo na wanapoziona sasa kwao wanaona ni jambo la kawaida tu. Basi naona ninapaswa kuelezea kidogo kihistoria mambo yalikuwaje kwenye ukoloni.


 Miaka ile tuliyokitawaliwa na Wazungu wakoloni, katika nchi yetu kulikuwa na mifumo tofauti ya elimu kwa watoto wa nchi hii. Zilikuwapo shule chache za watoto wa wananchi. Hizi zikiitwa shule za Waafrika. Zilikuwapo shule kwa watoto wa wageni wa aina mbili. Wageni Wazungu walikuwa na shule zao, na wageni wa kutoa Asia nao walikuwa na shule zao.


Aina hizo tatu (3) za shule zilijulikana sana kama “African Schools,” “Indian School” na “European Schools”. Kila aina ya shule ilikuwa na mfumo wake tofauti na mfumo wa aina nyingine ya shule. Ndiyo kusema elimu katika nchi yetu ilitolewa kwa matabaka.
  Mwalimu Nyerere alilalamikia hilo kule kwenye Umoja wa Mataifa mwaka 1956. Alisema hivi, namnukuu, “Now I turn on to education: In Tanganyika education is racial. There are separate schools for the children of the different racial groups. All European children and all Asian children receive primary education. Only 40% of the African children go to school”. (Hotuba ya Mwalimu Nyerere – Umoja wa Mataifa kikao cha 579 tarehe 20 Desemba, 1856). Hapo Baba wa Taifa alionesha namna watoto wengi wa wananchi (sisi waafrika) wanavyokosa elimu wakati watoto wote wa wageni wanapata elimu ya msingi. Elimu yote kwa ujumla wake ilikuwa inatolewa kwa matabaka ya rangi.


  Wizara ya Elimu enzi za ukoloni iliongozwa na Mkurugenzi wa Elimu aliyesaidiwa na Naibu Mkurugenzi wa Elimu. Baada ya hao wawili waliteuliwa maafisa walioitwa wakurugenzi wasaidizi wa elimu kwa kushughulikia matabaka ya watoto katika nchi hii. Alikuwapo Mkurugenzi Msaidizi kwa Elimu ya Waafrika (Assistant Director African Education) na alikuwapo Mkurugenzi Msaidizi kwa Elimu ya wageni – (Assistant Director for Non-Native Education). Huyu ndiye hasa aliratibu elimu kimatabaka na hata Wizara ikaunda Mabaraza manne (4) ya Elimu kulingana na matabaka ya makundi ya wakazi wan chi hii.
Wizara iliunda mabaraza namna hii:-


    1.    Lilikuwapo Baraza la Ushauri kwa Elimu ya Waafrika (The Advisory Committee for African Education).
    2.    Kuliundwa Mamlaka ya Elimu kwa Wazungu (The European Authority for Education).
    3.    Kuliundwa Mamlaka ya Elimu kwa Wahindi (The Indian Authority for Education) na;
     1.    Kuliundwa Baraza la ushauri kwa elimu ya wale wageni wengine (The Advisory Committee for other Non-Native (Including Goan) Education).


Kama mnavyoona muundo wa mabaraza hayo; yapo mawili yalikuwa ni ya kushauri tu, lile la Waafrika na la Magoa na wageni wengineo. Lakini kwa Wazungu na Wahindi kuliundwa mamlaka kamili yenye uwezo wa kuendesha ile elimu ya Wazungu na ya Wahindi. Kwa mfumo namna hiyo wa elimu ni dhahiri wananchi wasingeweza kuwa na mchango mkubwa hapo Wizarani.


  Sisi wazee tuliohitimu ualimu zamani zile tunajua adha ya ubaguzi ule katika elimu kwa wananchi. Mimi mwenyewe nimehitimu Chuo cha Ualimu daraja 1A mwaka 1953 nikaanza kufundisha katika shule ya Sekondari tangu Januari 1954. Ninaelewa sana elimu aliyokipata mtoto Mwafrika kuanzia shule za msingi, za kati mpaka za sekondari.


 Sheria nzima ya elimu katika nchi hii ilikuwa ovyo. Sheria mama ya Elimu ilitungwa mwaka 1927 na inajulikana kama Sheria ya Elimu kwa Waafrika ya 1927. (The Education (AFRICAN) Ordinance of 1927). Kulingana na mazingira ya wananchi sheria hii ilifanyiwa marekebisha mara kwa mara. Hapo mwaka 1933 sheria hii ilirekebishwa kusawazisha elimu itolewayo katika shule za Serikali kuwa sawa na ile itolewayo katika shule tulizokiziita “Native Authority” (L.A Schools) za wanachi wenyewe.


 Mwaka 1950 sheria ilirekebishwa na kutaka kila darasa lisizidi watoto 45 wala lisipungua watoto 30. Sheria iliweka utaratibu wa kuwa na mabaraza ya shule (Native Authority Education Committees) na pia sheria ilimpa Mkurugenzi madaraka ya kufuta shule kama haikidhi matakwa ya kisheria.
 Mwaka 1954, sheria iliweka utaratibu wa kusajili walimu na shule zile za awali za misheni zilizojulikana kama “BUSH SCHOOL”. Wakati tunaelekea kwenye Uhuru na huo Uhuru unanukia nukia, Serikali ya TANU ilikusudia kusawazisha utaratibu wote wa elimu uendane na hadhi ya taifa huru. Basi uliandaliwa mpango wa kufumua mfumo wote wa elimu ya kikoloni na kuunda mfumo mpya kwa taifa zima.


 Mwaka 1958, baada tu ya ule uchaguzi wa mseto, Serikali ya TANU ilifikiria kubadilisha kabisa ule mfumo wa elimu. Basi iliundwa kamati maalum iliyojulikana kama KAMATI YA KUREKEBISHA ELIMU NCHINI-(THE INTEGRATION COMMITTEE). Kamati ile iliagizwa kuandaa mapendekezo ya kuoanisha mifumo yote ya elimu katika nchi na hatimaye kuwepo na mfumo mmoja wa elimu kwa Taifa la Tanganyika.


 Mapendekezo ya Kamati ile yalitolewa mwaka 1960 na mara tu baada ya kupokewa mapendekezo yale Serikali ya wananchi iliandaa tamko maalum lililotolewa kama “White Paper” No. 1 ya 1960”. White Paper ile ilitoa yafuatayo:-
     1.    Kusitishwa kwa matumizi ya lugha za Kihindi katika mashule ya Wahindi (The Asian Vernacular medium was dropped).
    2.    Kufutwa kwa shule za mataifa na za dini (titles reffering to race and religion were abolished).
     3.    Shule zote za wageni ziliamriwa mara moja kufundisha somo la Kiswahili kuwaandaa watoto watakaomaliza elimu ya msingi kuandika mtihani wao kwa lugha ya KISWAHILI au Kiingereza (English-Medium Schools were required to introduce Kiswahili as a subject in the schools).


 Kwa kumbukumbu zangu mimi Serikali mwaka 1967 ilianza kuwaondoa walimu wakuu wa shule wasiokuwa raia wa Taifa hili na hivyo kukabidhi uendeshwaji wa shule zote hapa nchini mikononi mwa wananchi wenyewe wanaojua lugha yetu ya Kiswahili. Hii ilikuwa kuandaa wananchi kwa ujio wa shule za Taifa huru.
 Pili, Serikali ilisitisha shule za Wazungu, ilibakiza shule 11 tu zenye kuitwa shule za kimataifa katika nchi ndizo ziendeshe masomo yote kwa Kiingereza. Hizi zilijulikana kama shule za kimataifa au English Medium. Shule hizi ni kwa kuelimisha watoto wa wageni katika nchi hii. Wageni wenyewe ni maafisa wa Balozi mbalimbali, na wataalamu waliohitajika kwa maendeleo katika nchi yetu.


 Serikali ilidhamiria kutoa elimu safi na bora iliyo sawa kwa watoto wote na hivyo kufuta na kukomesha ubaguzi wowote katika elimu kwa wakazi wote wa nchi hii. Lakini sasa zinaporuhusiwa shule za Wahindi, Waarabu na Serikali inavyozidi kuruhusu shule tunazoita “English Medium” katika nchi, wazee tunapelekwa mbali sana kimawazo. Ndipo tunajiuliza ubaguzi katika mashule unarudi kule kule kwa miaka ya ukoloni? Mbona mwaka 1970 Serikali ilitaifisha shule zote?


 Wakati utaifishaji wa shule mwaka ule wa 1970 ulibakiza shule 11 tu za English Medium kwa wageni, leo hii 2015 zipo shule 651 hizo zinazoitwa English Medium (za Serikali zipo 8 tu lakini za binafsi ziko 414 na za dini 229) zinazotambulika na Wizara. Wageni wengi wa kujaza shule hizo wako wapi? Shule hizo sasa ni za watoto wa vigogo na wenye kujiweza na wala si kwa watoto wa wageni tena kama ilivyokusudiwa miaka ile ya nyuma. Na hizi za mataifa ya Wahindi na Waarabu zimepataje usajili wa Wizara? Nchi hii iliamua watoto wote wasome pamoja, elimu moja ili kuwajengea uzalendo katika makuzi yao. Sasa unaporuhusu ziwepo shule za Wahindi na shule za wenye uwezo si ndiyo chanzo cha kujenga matabaka katika taifa? Tunakwenda wapi? Ni “about turn” hiyo kielimu.


 Hapa nchini Tanganyika walikuja kuishi Wahindi wa aina mbalimbali kutoka Bara Hindi. Walifika makundi makubwa matatu ya hao Wahindi. Sijui kama Watanzania wa leo (vijana) wanajua makundi ya hao wa Bara Hindi. Sisi wazee tunakumbuka wapo wale wanaotoka maeneo ya Gujarati kule India.
Hawa kwa ujumla ni Wahindi, miongoni mwao wapo tunaowaita Wahindu, wapo wa Shia na wapo wale wa Ithna-Asheri na wa Aga Khan. Kundi la pili ni wale wa kutoka maeneo ya Punjab. Hapo tunao Wahindu, na Makalasinga. Na kundi la tatu ndiyo wale wa kutoka sehemu za kusini magharibi mwa Bara Hindi na wengi wao tuliwajua kama Magoa na wafuasi ya dini ya Kikristo. Kila kundi kati ya hao walikuwa na shule zao hapa nchini.


  Baadhi ya shule zilizokuwa za Wahindi siku za ukoloni hapa Dar es Salaam ni hizi Shaaban Robert, Tambaza, Jangwani, Kisutu, Azania, Forodhani (St. Josephs Convent sasa Millennium), Mzizima na Zanaki hizo zote zilijukana kama Indian Schools. Zote zilitaifishwa mwaka ule wa 1970 na kupata majina hayo ya sasa badala ya majina yao ya Kihindi/Kigoa.


  Leo hii ninapoona basi limeandikwa Indian School Bus au Yemen School Bus mimi najiuliza, Wizara ya Elimu inaturudisha kule miaka ya 1950? Au mtazamo wangu huo ni potofu? Hapa nahitaji kuelimishwa.
 Kama kweli Wizara imeamua kurudisha matabaka katika mashule, mitaala gani inatumika katika shule hizo? Kwa vile watu binafsi na taasisi zenye fedha zina uwezo wa kuendesha shule na wanaona fahari kuwa na shule za English Medium, je, nchi ya wajamaa, raia walio sawa, inaweza kuwaelimisha watoto wao kimatabaka namna hii?


 Hapo walionacho watapata elimu tofauti na katika mazingira tofauti na wasionacho ndiyo hao wa shule za kata. Ni sawa malezi namna hiyo? Mbona tunarudia kwenye ule utaratibu wa mkoloni? Tunawaandaa watoto wa Taifa lipi hapa Tanzania? Sijui kama mtoto anayetoka kule Indian School anaweza kushirikiana vizuri na mtoto wa kutoka kule Pembamnazi au Chanika?


 Moja ya shabaha za elimu ya taifa ni kuwalea na kuwakuza watoto wa Taifa hili katika maadili ya Kitanzania na kizalendo. Hii shule ya Yemen, sijui wenyewe ni watu gani! Lakini sote tunajua kuwa nchi ya Yemen haijatengemaa kisiasa. Je, walimu wanaofundisha shule hiyo tunawajua vilivyo? Isije tukawa tunalea wanaharakati wa huko Yemen? Tuna uhakika gani na uzalendo wa wanaosoma humo? Wakaguzi kutoka Wizara ya Elimu wameridhika vilivyo na mafunzo katika shule hizo?


 Mimi nafikiria makuzi ya watoto wetu katika mashule yetu yanakuza na kulenga UZALENDO. Shule zote za gharama kubwa kwa mtazamo wangu huwa na mawazo ya unafsi, ubepari na sioni namna wanavyoweza kufikiria ujamaa huku mazingira waliyokulia yana muono wa ubepari. Jina la shule linatia wasiwasi na uzalendo wake. Sipendi kufikiria dhana ya mamluki katika malezi ya watoto kwenye mazingira ya utajiri unaoelekea kuwapo katika aina hii ya shule?


  Nimechimbua historia ya mfumo wa elimu enzi za ukoloni, pale wakurugenzi wa elimu walipoweza kupanga na kuratibu elimu ya watoto wa Tanganyika. Hizo shule za Wahindi na Waarabu za sasa zinaratibiwaje? Je, zipo shule nyingine kama hizi mahali pengine katika Jamhuri yetu hii?
 Kuna methali inayosema KINGA NI BORA KULIKO TIBA. Taifa linafaa kuwa na tahadhari katika uanzishaji wa shule hizi za mataifa tusije tukatengeneza vituo vya kufunza magaidi hapa nchini. Utaifishwaji wa shule za mataifa na za madhehebu za dini ulikuwa kukinga kukua kwa matabaka miongoni mwa wakazi wa Tanganyika. Sasa kuongeza shule za English Medium ni kueneza sera ya matabaka. Taifa hili litaweza kuhimili matabaka miongoni mwa Watanzania?


 Mimi nimetoa dukuduku langu la moyoni juu ya kile nilichokiona. Nitashukuru sana kupata maelezo sahihi juu ya shule zenye mabasi haya. Aidha, nitafurahi kuthibitishiwa kuwa elimu itolewayo katika shule hizi siyo hatarishi. Watoto wale siyo wakuja bali ni raia safi wa nchi hii. Wala siyo watoto wa uraia wa nchi mbilii (dual citizenship). Kumbe wazalendo ni wale wote wenye kuifia nchi yao na wana uraia wa nchi moja tu. Siyo vibaya kukumbusha wenzangu kuwa TANZANIA ITAJENGWA NA WENYE MOYO NA WAZALENDO.


 Naomba tena nikumbushie maneno ya Mwalimu Nyerere kule kwenye Umoja wa Mataifa kikao cha 579 cha Kamati ya Nne, tarehe 20 Desemba 1950. Narudia lalamiko lake ….in Tanganyika education in racial “in terms of separate school systems for Europeans, Asians and Africans, with different financial, teaching and other resources….. so this apparent injustice to the African, like so many others, is done for the good of the African!


  Kwa maneno haya sisi Watanzania wa leo bado tunakubali kuwapo kwa shule za wenye kipato eti wawe na majengo mazuri, walimu bora, mazingira tofauti kabisa na yale ya shule za watoto wa wakulima, kwenye shule za Kata ya Mlingoti au Nalasi kule Tunduru halafu wote wafanye mtihani ule ule kuingia kidato cha kwanza. Je, ni ulinganisho halali namna hii? Mwalimu alisema tofauti hizo siyo sahihi. Mtoto asiyepitia English Medium na yule wa English Medium tukubali jamani kimazingira hawapo sawa!


  Kama hivyo basi kwa nini Serikali iendeleze kusajili shule hizi za binafsi za English Medium? Kabla ya Uhuru zilikuwa 11 tu, leo hii zipo 651! “So, this apparent injustice to peasants' children in our country should be discouraged”. Nionavyo mimi.
 Naomba matabaka katika elimu ya nchi hii yasiruhusiwe kwa kisingizo chochote kile. Wizara isikubali kusajili shule za elimu ya matabaka Tanzania. Tujenge UZALENDO miongoni mwa watoto wetu hawa, taifa la kesho.

3128 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!