Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula

Na Charles Ndagulla, Moshi
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, amesema Serikali
imepata Sh bilioni nne zitakazotumika kurekebisha mipaka iliyopo kwa nchi za Tanzania na
Kenya inayoharibika na mingine kuwa na umbali mrefu.
Mabula ameyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kutembelea eneo la mpaka wa
nchi hizo katika tarafa ya Tarakea mkoani Kilimanjaro. Mpaka huo ni miongoni mwa
itakayorekebishwa.
Kwa mujibu wa Mabula, mipaka itakayorekebishwa ni iliyopo kwenye mikoa ya Mara, Arusha,
Kilimanjaro na Tanga na kwamba marekebisho hayo yanatokana na maafikiano kati ya nchi
hizo.
Mabula amesema maofisa wa Serikali ya Kenya na Tanzania wanaohusika na utambuzi wa
mipaka, wameshakutana katika vikao vya awali na kukubaliana kazi hiyo kuanza rasmi Machi
22, mwaka huu.
Amesema utambuzi wa mipaka hiyo utaanza kwa kuondoa alama za mipaka zilizovunjika na
kuweka mpya.
“Tunakusudia umbali wa alama moja ya mpaka hadi nyingine iwe karibu, kwani za awali
zilikuwa mbali na hivyo kusababisha wananchi hususan upande wa Tanzania, kuvamia eneo la
hifadhi na kujenga makazi ya kudumu,” amesema.
Kutokana na hatua hiyo, Mabula ametoa siku 20 kwa wananchi wa mikoa ya Mara, Arusha,
Kilimanjaro na Tanga waliovamia na kujenga makazi ya kudumu kwenye eneo la hifadhi ya
mpaka kati ya Tanzania na Kenya kuondoa makazi yao.
Mabula alishuhudia makazi ya kudumu zikiwamo nyumba za kifahari kwenye eneo la hifadhi.
Amesema muda huo utakapopita bila utekelezaji wa hiari wa agizo hilo, Serikali itabomoa
nyumba hizo kwa kushirikiana na mamlaka za utawala za Kenya.
Hivi karibuni, Serikali iliweka alama za X kwa wananchi walioingia na kujenga makazi ya
kudumu kwenye hifadhi ya mipaka katika mikoa inayopakana na Kenya.
Katika hatua nyingine, Mabula amezitaka halmashauri za wilaya nchini kutenda haki katika
bajeti zao na kwa idara zilizopo ikiwamo ya ardhi ambayo alidai imekuwa haipewi bajeti stahiki.
Amesema kila wilaya aliyopita, changamoto kubwa aliyokutana nayo ni bajeti ndogo
isiyozingatia mahitaji kwa idara ya ardhi, hali inayosababisha zitegemee msaada zaidi kutoka
wizarani.
“Niwaombe halmashauri zote, tendeni haki kwenye idara zote katika bajeti zenu, idara hii
imeachwa kama mtoto yatima, haipewi bajeti stahiki na hata ukiwauliza kama wana gari,
watasema hawana, hata kompyuta ni shida,” amesema.
Pia, Mabula ameelezea kutoridhishwa na makusanyo kwenye kodi ya ardhi na kwamba
ikisimamiwa vyema, inaweza kuongeza pato la halmashauri husika.
Aliagiza wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi kupewa hati ya siku 90 ya kusudio la kufikishwa
mahakamani, kama watashindwa kulipa malimbiko ya kodi zao.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edward Ntakilikho, amesema ukosefu wa
vitendea kazi zikiwamo kompyuta, na kukosekana kwa umeme wa uhakika ni miongoni mwa
changamoto zinazoathiri ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agnes Hokororo, amesema uvamizi uliofanyika umeathiri shughuli
za kijamii kwenye mpaka huo.
caption:

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula (kushoto),
akiangalia alama za mpaka wa Tanzania na Kenya, eneo la Tarakea Wilaya ya Rombo,
mkoani Kilimanjaro.

2116 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!