Rekodi ya utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan ilianza kujionyesha wazi tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo.

Watanzania na walimwengu kwa ujumla wao mara moja walianza kuonja pepo ya haki miongoni mwa wananchi. 

Kwa muda mfupi, mamia ya watu waliokuwa wamebambikiwa kesi na kuwekwa katika mahabusu nchini kote walianza kuachiwa huru na wengine wakiachiwa kwa masharti.

Unyanyasaji wa wafanyabiashara kupitia vikosi kazi vya ukusanyaji kodi ulikoma, nao wakaanza kuona mwanga mpya katika Tanzania mpya. Kwa ufupi Rais Samia amefanya mengi mazuri ya faraja kwa Watanzania katika muda mfupi.

Pamoja na mazuri yote hayo, kumeanza kujitokeza madoa katika serikali anayoiongoza ambayo tuna kila aina ya sababu ya kuamini kuwa hayatokani na utashi wake, bali ni watendaji ambao, ama wamekusudia kumuundia taswira mbaya kwa wananchi na walimwegu, au ni wale waliozoea kuishi katika maovu na uonezi.

Tunasema hivyo tukirejea baadhi ya matukio ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa baadhi ya wanasiasa. 

Jeshi la Polisi limetoa sababu kadhaa za kukamatwa kwao, lakini kubwa ikiwa ni ya madai ya kuzuia mikusanyiko inayoweza kuchochea maradhi ya UVIKO-19.

Hatupingi polisi kutekeleza wajibu wao, hasa linapokuja suala la kutekeleza amri za wakubwa wao wa kazi. Hata hivyo tunahoji, iweje uzuiaji wa mikusanyiko hiyo uwahusu wanasiasa wa upinzani tu, usiwaguse wale wa chama tawala?

Pamoja na kuunga mkono juhudi zote za mapambano dhidi ya ugonjwa huu, bado tunaamini kuwa polisi wanao wajibu wa kuhakikisha amri hizi zinasimamiwa kwa pande zote badala ya kuegemea upande mmoja. Kwa kufanya hivyo wananchi wataona na wataheshimu uamuzi wowote.

Tunatoa mwito kwa Jeshi la Polisi, vyombo vya usalama na watendaji wa serikali wakiwamo wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kujiepusha na matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kutia doa taswira ya Rais wetu kwa wananchi wake na katika jumuiya ya kimataifa.

Wasifanye mambo kwa kudhani wanamfurahisha Rais ilhali ukweli ni kuwa wanamweka katika mazingira magumu, maana kwa wananchi, kila linalotendwa hata na polisi wa kata wanajua ni maagizo ya Rais.

Tunatoa mwito kwa watu wote wenye mamlaka kusimama katika sheria, kanuni na miiko ya kazi zao. Wasifanye mambo ya kumjengea chuki Rais ambaye kwa muda mfupi amekonga nyoyo za wengi.

By Jamhuri