Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameeleza kuridhishwa kwake na kasi ya utandazaji na uunganishwaji wa mabomba ya kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Gesi hiyo itatumika kuzalisha umeme katika mitambo ya kufulia nishati hiyo itakayojegwa eneo la Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.

Profesa Muhongo amewataka Watanzania kuwapuuza watu wanaobeza mradi huo wa gesi akisema hakuna haja ya kuwasikiliza kwani hawajui umuhimu wa mradi huo katika kukuza uchumi wa Watanzania.

 

Muhongo ameyasema hayo hivi karibuni wilayani Mkuranga, wakati wa ziara ya kukagua uunganishwaji wa mabomba hayo yanayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2014.

 

Amesema kwamba ujenzi huo wa mabomba ya gesi unaendelea vizuri na kwamba kuna vikosi vitano ambapo baadhi vinajenga kuanzia Mtwara kuelekea Dar es Salaam na vingine vinaanzia Dar es Salaam kwenda Mtwara ili kukamilisha kilomita 542 za mradi huo.

 

Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Lu Youqing, ameuhakikishia umma wa Watanzania kwamba ujenzi wa bomba unajegwa kwa technolojia ya hali ya juu na kwa umakini mkubwa na viwango vyake ni vya kimataifa.

 

Youqing amesisitiza uwepo wa uhuru, urafiki na demokrasia katika kutimiza azma ya kukamilisha ujenzi huo ambapo ametamka wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mradi kuisha kabla ya wakati uliopangwa kutokana na kasi waliyonayo wafanyakazi katika ujenzi huo.

 

Muhongo amefafanua kuwa mabomba yaliyolazwa na yanayofanyiwa kazi yanakamilisha kilomita 104 ambapo tayari kilomita 34 zimeshaunganishwa kwa kuchomelewa, ikiwa ni hatua ya awali ambapo kilomita sita zimesilibwa kuzuia nafasi ya gesi kupenya na kupotea.

 

Mhandisi wa bomba la gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Mafuta nchini (TPDC), Injinia Baltazari Thomas, amethibitisha hayo. Akielezea changamoto zinazowakabili katika ujenzi wa bomba la gesi, Peter Erasmus, Manager wa mradi (QA/QG), amesema hali ya kunyesha mvua inakwamisha ujenzi wa mradi huo kwani ni vigumu na ni gharama kubwa kujenga kipindi hicho pia ni hatari kwa afya za wafanyakazi.

 

Hii ni mara ya pili kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Balozi wa China, Lu Youqing, kufanya ziara maeneo ambayo ujenzi wa mabomba unaendelea na kwamba wamekubaliana kutembelea maeneo hayo kila mwezi ili kuwapa hamasa wajenzi kuwa na kasi inayotakiwa na hivyo kuwezesha mradi kukamilika kwa wakati.

 

 

By Jamhuri