Na Dk. Felician Kilahama

Kwanza nianze makala hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kwa mapenzi yake ametujalia zawadi ya uhai mpaka tukaweza kuufikia mwaka 2018.

Ni mwaka wa matumaini, lakini pia umeanza kwa baadhi ya maeneo nchini mwetu kugubikwa na sintofahamu ya usalama wa chakula kwa watu na mifugo.

Wasiwasi huo unatokana na hali mbaya ya mazingira hususani kukosekana kuwepo misitu ya asili na uoto mwingine hivyo kuambatana na kuongezeka ukame kama nilivyoshuhudia katika baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Musoma Vijijini hasa katika kata za eneo la “Bukwaya”.

Desemba 16-24, 2017 nilizuru kata nne za Halmashauri ya Musoma Vijijini na kata moja katika Halmashauri ya Butiama. Kata husika ni: Bisumwa (Butiama); EtaroIfulifuNyakatende na Nyegina (Musoma Vijijini).

Nashukuru na kupongeza jitihada zinazofanywa kupitia Umoja wa Maendeleo Bukwaya (UMABU) kujaribu kuamsha ari ya wakazi wanaoishi kwenye kata hizo ili waweze kupanda miti ya kutosha kwa lengo la kuinusuru hali ya mazingira isiendelee kuwa mbaya kwenye maeneo mengi katika Halmashauri ya Musoma Vijijini.

Kusema kweli hali ilivyo eneo la Bukwaya ni mbaya mno kiasi cha kutishia uhai wa wakazi wa eneo hilo pamoja na mifugo yao. Mvua za vuli zimekuwa kidogo.

Nguvu nyingi za wakulima zimeishia kuyaona mahindi yanakauka na wasijue nini cha kufanya isipokuwa kuomba neema za Mwenyezi Mungu na misaada ya chakula kutoka kwa Serikali na wasamaria wema.

Pamoja na hali hiyo ya ukame mkubwa kulikumba eneo la Bukwaya, nimshukuru Mratibu wa UMABU, Padre Leo Kazeli, Paroko wa Parokia ya Nyegina, ambaye aliweza kuwasiliana nami na hatimaye, kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu, nikajaliwa kutembelea maeneo husika.

Haikuwa kazi rahisi kwa kuzingatia kuwa mimi nimestaafu utumishi wa umma takribani miaka mitano iliyopita, lakini kama usemi ulivyo; ‘penye nia pana njia’ na kwa uweza wake Mwenyezi Mungu hakuna linaloshindikana; nikajikuta nimefika mkoani Mara na kuyafanya ambayo Mungu amenijalia kuyatekeleza pasipo shaka yoyote. Jina la Bwana Lihimidiwe.

Pamoja na kujionea hali ya mazingira ilivyo na hali mbaya ya ukame iliyoashiria mashamba mengi ya mahindi kukauka; niliweza kukaa na kuzungumza na watendaji kata wakiwamo madiwani.

Wengine niliokutana nao ni viongozi wa Serikali za vijiji na vitongoji; viongozi wa vikundi mbalimbali vya kujiletea maendeleo endelevu, wakuu wa shule, walimu, na wafanyakazi kutoka Idara ya Afya na Polisi. Mazungumzo yalifanyika kwa njia ya warsha ili kupata michango ya pamoja juu ya nini kifanyike ili kunusuru hali ya mazingira inayoendelea kuwa mbaya kila kukicha katika eneo la Bukwaya.

Warsha ya kwanza ilifanyika Kata ya Nyegina na kufunguliwa na Justin Mamko ambaye ni Afisa Tawala Wilaya (DAS) ya Musoma, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ambaye alikuwa awe mgeni rasmi, lakini akawa na majukumu mengine ya kitaifa. Vilevile, wakati wa ufunguzi alihudhuria Afisa Maliasili kutoka Halmashauri ya Butiama.

Kabla ya mgeni rasmi kutoa nasaha zake, Mratibu wa UMABU ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Nyegina, alieleza madhumuni ya kufanya warsha hiyo ikiwa ni pamoja na kutaka kujifunza mengi kutoka kwangu, Dk. Felician Kilahama; akikariri kuwa ni “Nabii wa Uamsho wa Mazingira” katika taifa letu la Tanzania.

Vilevile alieleza kuwa kupitia UMABU, Dk. Kilahama ameweza kufika mkoani Mara ili kwa pamoja, tuweze kutafakari kwa kina nini kifanyike katika eneo zima la Bukwaya ili kasi ya uharibifu wa mazingira ipunguzwe.

Mratibu wa UMABU aliongeza kuwa yeye kama mtumishi wa kiroho amekuwa akipambana na kuwasaidia watu waimarike kiroho, lakini pia kupitia taasisi za kidini wamekuwa wakitilia mkazo umuhimu wa kuwasaidia binadamu waweze kupata mahitaji yao ya kimwili kwa kuzingatia umuhimu na kupitia huduma za elimu, afya na upatikanaji na usambazaji maji safi na salama.

Alisema ni vigumu kuimarisha watu wa Mungu kiroho wakati kimwili, kiakili na kiafya wako dhaifu. Alimaliza utangulizi wake kwa kusema kuwa sasa wakati umewadia wa kutambua ukweli kwamba kuendelea kuhubiri habari za kiroho na ufalme wa Mungu hakutaeleweka vizuri kwa walengwa wakati “nchi inakufa”.

Hii ina maana kwamba watu wa Mungu wahubiriwe habari za kiroho (wokovu na ufalme wa Mungu), lakini pia mkazo uwekwe kwenye masuala ya kimwili ikiwa ni pamoja na utunzaji mazingira na matumizi ya rasilimali kama ardhi na misitu ya asili kwa njia zilizoendelevu.

Nawashukuru wananchi wa kata nilizozuru kwa wema na ukarimu wao mkubwa kwangu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwema atawakirimia zaidi kwa wema wao huo.

Pamoja na hayo yote inabidi jamii ya Watanzania tuwasaidie wakazi wa Bukwaya ili waweze kupata chakula hasa wakati huu kutokana na ukame maana mvua ilinyesha, lakini kwa sababu nje ya uwezo wao ikaacha kunyesha wakati mahindi yanaanza kutoa mbelewere na mengine kuweka mahindi hivyo kusababisha eneo zima la Bukwaya kugubikwa na hatari ya baa la njaa.

Inabidi pia wataalamu tujiulize na kutafakari kwa kina nini kifanyike ili kurejesha hali ya mazingira katika eneo la Bukwaya na mengineyo nchini katika uhalisia wake, hususani kama ilivyokuwa zamani takribani miaka kama arobaini iliyopita.

Misitu na uoto asilia katika mkoa mzima wa Mara kwa sasa ni historia kiasi kwamba misitu ya asili imetoweka; na hali ya mazingira ni mbaya sana kiasi cha kuashiria hali ngumu ya maisha kwa wenyeji na wakazi wengine mkoani Mara.

Vilevile, hali ya ukame imeyakumba maeneo mengi nchini kama iliyo kwenye eneo la Bukwaya hivyo kukabiliwa na hatari ya kukosa chakula cha kutosheleza mahitaji ya familia nyingi.

Isitoshe, usalama wa chakula kwa mtazamo kwamba wakazi wa maeneo mengi nchini hawana chanzo cha kuaminika (cha uhakika) kuweza kupata nishati ya kupikia chalula. Kukosekana kwa nishati rafiki ya kupikia kunaongeza hali ya usalama ya chakula kuwa tete zaidi.

Maana haiingii akilini kwamba familia inayo unga wa mahindi, lakini hakuna nishati ya kuutayarisha unga kuwa katika hali ya kuliwa na binadamu.

Ili unga uweze kuliwa sharti utayarishwe na kugeuzwa kuwa ugali au uji ndipo uweze kuwa wa manufaa kwa binadamu. Kinyume chake mwenye unga akiwa hana kuni wala mkaa, ataishia kufanana na mwananchi ambaye anazo kuni au mkaa, lakini hana unga au kitu kingine cha kupika.

Hivyo, eneo ambalo halina misitu ya asili ya kutosha au halikupandwa miti mingi kwa ajili ya matumizi ya binadamu na uhifadhi wa mazingira; eneo kama hilo litakuwa linakabiriwa na changamoto nyingi ikiwemo hali mbaya ya usalama wa chakula mara kwa mara.

Naomba wataalamu wote wa sekta za ardhi, kilimo, maliasili, mifugo, mazingira, maji, maendeleo ya jamii, nishati, madini, uvuvi, ufugaji nyuki, wanyamapori, matumizi bora ya ardhi, elimu na afya tuungane ili tuweze kuisaidia jamii ya Tanzania kuondokana na changamoto za uharibifu wa mazingira kwa kujua au kutokujua.

Kwa kusema hilo namaanisha kwamba tukiwa wataalamu katika fani tulizosomea na ni taaluma ambazo moja kwa majo zinaguza maisha ya Watanzania wenzetu walio wengi vijijini; tunawajibika kuhakikisha kwa kupitia taaluma zetu, Watanzania wanaishi maisha yaliyo rafiki kwa mazingira ikiwa ni pamoja na kutokata miti au kufyeka misitu ya asili hovyo.

Vilevile, tuhakikishe kwamba sehemu zilizo wazi zinapandwa au kuoteshwa miti hasa kwa kutumia aina za miti iliyokuwa ikistawi mahali pale miaka iliyopita (indigenous tree species).

Maeneo mengi mkoani Mara ni mfano mzuri kwa wataalamu kuweza kuonesha makali ya taaluma zetu kwa kuhakikisha wananchi wanaelimishwa ipasavyo na hatimaye waweze kuchukua hatua stahiki.

Tukitoa ushauri wetu wa kitaaluma, na siasa zikawekwa kando, kwa miaka michache ijayo hali ya Mkoa wa Mara inaweza kubadilika kwa kuhakikisha uoto wa asili unarejeshwa haraka iwezekanavyo.

Milima na vilima vyote vitunzwe na uoto wa asili urejeshwe na kuhakikisha unalindwa kwa kutumia sheria zilizopo au jamii husika kuweka sheria ndogo na kusimamia utekelezaji wake.

Shughuli zote za kibinadamu kwenye maeneo ya vilima na milima zipigwe vita kwa nguvu zote. Tusiachie uharibifu wa mazingira ukawa mbaya kiasi cha uangamiza maisha yetu na viumbe wengine.

Nawashauri viongozi wa vijiji na vitongoji wahakikishe wanasimamia matumizi bora ya ardhi ndani ya mipaka yao. Kusema kweli bado sehemu nyingi nchi rasilimali ardhi inatumiwa hovyo na ardhi haichukuliwi kama ni nyenzo muhimu sana kwa maisha yetu sasa na kwa vizazi vitakavyofuata.

Badala yake wengi wetu tunatumia rasilimali ardhi na misitu ya asili hovyo kiasi cha kutoweka na rasilimali ardhi kupoteza uwezo wake wa kutuzalishia chakula cha kutosha hivyo kugeuka jangwa (barren arable lands) na mahali pengine aina za miti ya asili kutoweka (disappear) kwenye uso wa dunia.

Nimekuwa nikizungumza na viongozi mbalimbali katika vijiji ninavyobahatika kuvitembelea, lakini cha kushanganza sijawahi kubahatika kukutana na viongozi wa vijiji wenye upeo mzuri na uelewa wa kutosha juu ya thamani na umuhimu wa rasilimali ardhi kwenye vijiji vyao.

Itaendelea…

Mwandishi wa makala hii, Dk. Feliciani Kilahama, ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Anapatikana kwa simu: 0756 007 400.

By Jamhuri