Leo ni Mwaka Mpya. Ni mwaka 2013. Tunafahamu Januari hii ni kichomi kwa familia nyingi. Iwe kwa matajiri au masikini, waajiri au waajiriwa ni mwezi wa tabu. Kodi za nyumba zinadai, ada za shule zinadai, wenye magari mengi yanaisha bima na hati za njia na hata wenye kununua viatu na nguo kwa msimu zimekwisha, wanahitaji vipya.

Katika mazingira hayo kila mtu analia ukata. Waajiriwa wengi huu ni wakati wa kuomba ‘salary advance’. Hii inatukumba si kwa sababu nyingine, ni kwa sababu tu hatukujipanga. Tuliyaacha maisha yaende yenyewe. Hatukujipa muda wa kukaa chini tukapanga masuala haya yasiyonyesha kama mvua. Mwaka huu tunashauri uwe tofauti.

 

Ndugu msomaji, wewe ndiyo uwe wa mfano mwaka huu. Mahangaiko unayopata mwezi huu kutokana na malipo mbalimbali jiambie hapana. Hutaki kuyapata tena mwakani. Panga maisha yako. Ada za shule kwa watoto au kodi za nyumba hazinyeshi kama mvua. Jiandae kuweka akiba. Anza tangu siku ya leo. Punguza matumizi yasiyo ya lazima.

 

Kama ulizoea kwenda baa kugida bia nane hadi 10, sasa punguza. Kunywa mbili hadi tatu. Kiasi kinachosalia kihifadhi kwenye simu yako; M-Pesa au tigo-Pesa. Ukiweza zaidi zipeleke benki. Ukiweka fedha kwenye akaunti ya benki ni vigumu kwenda kuchukua Sh 10,000 ya kulipia pombe baa. Hebu tuanzishe vibubu katika kila familia.

 

Vibubu ni makasha ya kuhifadhi fedha. Tujiwekee utaratibu kwa wanaoweza kila siku tuhifadhi Sh 3,000 hadi 5,000 kila siku. Bila kukisumbua kibubu hicho, ukiweza kutunza kiasi hicho cha fedha bila kukosa, kwa mwezi utakuwa na wastani wa Sh 150,000 na kama utafanikiwa kufanya utaratibu huu kwa miezi 12 basi utajikuta una akiba ya Sh 1,800,000 kila mwaka. Kiasi hiki si kidogo. Kinaweza kumaliza matatizo ya msingi.

 

Ukiacha hilo tunapenda kuwahimiza Watanzania. Mwaka huu ni mwaka mmoja kabla ya ahadi ya Katiba mpya kutekelezeka mwakani. Pia ni mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kufanyika mwakani, na ni miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Kisiasa hii ni miaka ya kuchemka. Tunatarajia kusikia watu wengi wakijinadi na kujinasibu na vyama mbalimbali vya siasa.

 

Itakuwapo mikutano mingi ya hadhara na baadhi ya vyama vitaitisha maandamano bila kuchoka. Katika hili tunasema huu ndiyo wakati wa Watanzania kutathmini faida za harakati mbalimbali. Badala ya kutumia muda mwingi kushiriki shughuli zisizo na tija ya moja kwa moja kwa familia yako, tuelekeze nguvu kubwa katika kufanya kazi.

 

Kama ni maneno tumezungumza ya kutosha. Tukifika mahala hatupimi tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi kama familia, tutakuwa katika hatari kubwa ya kusambaratika. Pato letu halisubiri maandamano. Tufanye kazi. Watoto wetu wanataraji sisi kama wazazi tutimize wajibu wetu. Hebu kila Mtanzania aamue kufanya kazi mwaka huu kwa nafasi yoyote aliyopo kisha tupitie mapato yetu baada ya mwaka huu.

 

Tuache maneno, tuchape kazi kwa maendeleo ya taifa letu. Mungu ibariki Tanzania.

 

 

 

 

By Jamhuri