Kwa siku kadhaa sasa mamlaka katika Jiji la Dar es Salaam zimekuwa zikiwahamisha wachuuzi waliovamia hifadhi za barabara na kuendesha biashara. Vurugu zimeripotiwa kutokea katika baadhi ya maeneo ya Ubungo na mengine jijini humo.

Kuondolewa kwa wachuuzi hao kunatokana na agizo la Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli. Waziri huyo anayesifika kwa uchapaji kazi aliwaagiza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuwaondoa ili maeneo hayo yabaki kwa matumizi yaliyokusudiwa kisheria. Agizo hilo lilikuwa halali.

Baada ya kuanza kuwaondoa, baadhi ya wachuuzi wameibua vurugu na kuandamana hadi kwa wakuu wa wilaya kulalamikia uamuzi huo. Sasa wanataka waonyeshwe mahali pa kwenda kuendesha uchuuzi wao.

Tunavyoona ni kwamba nchi hii hata ikiwa na Katiba mpya na nzuri kwa sifa zote, utii wa sheria bila shuruti hautakuwapo. Tunayasema haya kwa sababu tuna viongozi wazembe na mizigo.

Viongozi wa Serikali za Mitaa ni wazembe na wamepoteza sifa ya kuitwa viongozi. Tunasema hivyo kwa sababu hatari wanayoliandalia taifa hili ni kubwa sana.

Wamekuwa wakilea uvamizi huu kwa miaka mingi. Wavamizi wamekaa maeneo hayo. Wameendesha shughuli zao kinyume cha sheria kwa muda mrefu. Wamefikia hatua ya kujiona kuwa hapo walipo, wapo kihalali. Haya yamefanyika huku viongozi ‘mamangi meza’ wakiwa kimya kana kwamba hakuna uvunjifu wa sheria uliofanywa.

Baada ya wachuuzi hao kujiona hapo walipo ni stahiki yao, sasa wanagoma kuhama. Katika hali ya kawaida ya kibinadamu, wanajiona kuwa wanaonewa. Kuwaondoa sasa kunaweza kusababisha uvunjifu mkubwa wa amani na utulivu si kwa Dar es Salaam pekee, bali katika mikoa yote nchini.

Ndiyo maana tunasema kwamba kama kweli tunataka tuendelee kuishi kwa amani na utulivu, viongozi hawana budi kusimamia sheria. Wakijitokeza wachuuzi wakavamia eneo lisiloruhusiwa kisheria, waondolewe mara moja kabla hawajajenga vibanda au kabla hawajajiona kuwa na uhalali wa kuwapo mahali fulani.

Ikitokea mtu kajenga nyumba ya kuishi au ya kibiashara ndani ya eneo lisiloruhusiwa kisheria, aondolewe haraka kabla ya kumaliza msingi. Kama viongozi wa Serikali za Mitaa na Serikali Kuu watakuwa makini, wataliepusha taifa letu na manung’uniko haya yasiyo ya msingi, ambayo mwisho wake unaweza kuwa ni kuleta machafuko katika jamii yetu.

Madiwani lazima wasimamie sheria walizoapa kuzisimamia. Mameya lazima wapite katika maeneo yao. Wajiridhishe kuwa sheria na kanuni vinafuatwa. Kama wapo watendaji wanaozembea kusimamia sheria na kanuni wawajibishwe mara moja. Waulizwe, inakuwaje watu wavamie hifadhi ya barabara ilhali wao wakiwa mashuhuda tu bila kuwachukulia hatua za kisheria.

Lazima nchi hii tufike mahali watu waheshimu sheria. Lakini hilo halitawezekana endapo viongozi watabaki kuwa kama masanamu yasiyokuwa na utashi wala akili ya kutofautisha baya na zuri.

Tunasema kwamba bila kusimamia sheria na kudhibiti matatizo yakiwa bado mabichi, kuna siku taifa hili litaingia kwenye mapambano na wachuuzi ambayo hakuna vyombo vya dola vitakavyokuwa na uwezo wa kuyadhibiti.

14249 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!