Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama imeunda kamati ndogo inayoandaa Mpango Kazi wa kuzuia na kudhibiti ujangili.

Utekelezaji wa mpango kazi huo utatumia teknolojia ya kisasa, ikiwamo ya unmanned air vehicles (UAV) inayobaini uwepo wa majangili katika maeneo yenye wanyamapori na kuchukua hatua zinazostahili kwa wakati.

 

Hatua hiyo imetangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, bungeni, jana.

 

Kuhusu kuimarisha ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori, alisema doria -siku 59,338 zimefanyika ndani na nje ya Mapori ya Akiba. Watuhumiwa 1,215 walikamatwa kwa makosa mbalimbali na bunduki 85 na risasi 215 zilikamatwa.

 

“Kesi 670 zimefunguliwa katika Mahakama mbalimbali nchini. Kati ya hizo, kesi 272 zimekwisha kwa washitakiwa 247 kulipa faini ya Sh 175,002,420 na washitakiwa 71 kupewa adhabu ya vifungo vya jumla ya miaka 99. Aidha, kesi 398 zenye washitakiwa 897 bado zinaendelea katika Mahakama mbalimbali nchini.

 

“Wizara ilifanya operesheni za kiintelijensia katika Wilaya za Liwale na Tunduru ambazo ziliwezesha watuhumiwa 354 kukamatwa na kufunguliwa jumla ya kesi 283 ambazo zinaendelea katika Mahakama za Liwale na Tunduru. Bunduki 435 za aina mbalimbali, risasi 1,129, maganda 514 ya risasi, mbao 10,332 na nyara mbalimbali zenye thamani ya Shilingi 855,013,701.20 zilikamatwa.

 

“Vilevile, Wizara inaendelea na mikakati ya kuzuia, kudhibiti, na kukabili wimbi la ujangili nchini awamu kwa awamu katika maeneo mbalimbali kwa kufanya operesheni kama hizo. Wizara inatambua mchango mkubwa wa wananchi katika mapambano dhidi ya ujangili. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wanaosaidiana na Serikali kuwafichua wahalifu  na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kizalendo. Natoa rai kwa wananchi wengine wote washiriki mapambano hayo ya kulinda maliasili zetu.

 

“Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wote kwa ujumla katika juhudi za kuhifadhi wanyamapori kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.  Baadhi ya watu kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakifanya ujangili ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuchukuliwa hatua stahiki pale wanapokamatwa.

 

“Katika kutekeleza majukumu yao, baadhi ya Wahifadhi na Maafisa Wanyamapori wamekuwa wakiuawa au kujeruhiwa na majangili. Kati ya mwaka 1997 na 2012, Wizara imepoteza watumishi 17 kutokana na kuuawa na majangili. Aidha, kumekuwepo na matukio mengi ya wananchi kujaribu kuwazuia wahifadhi wanyamapori kutenda kazi zao,” alisema Kagasheki.

 

 

 

 

987 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!