‘Naelekea bungeni’

Ben Saanane

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ndugu marafiki zangu wa karibu na wa mbali, baada ya kupitia taarifa ya kamati za kiutafiti iliyokamilisha kazi yake jana kutoka jimboni mniwie radhi kwa kukawia dakika kadhaa kuitimiza ahadi hii niliyoidokeza takribani saa 72 zilizopita kutokana na dharura iliyojitokeza ya kiutendaji katika majukumu yangu ndani ya chama ngazi ya Taifa; majukumu yaliyokuwa na maslahi mapana zaidi kwa chama chetu na Taifa kwa ujumla.


Naam, naelekea bungeni. Nimeamua kwa uhakika kabisa kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu 2015 kupitia chama changu – Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Tangazo langu hili limezingatia mambo yafuatayo:
Kwanza, nimesukumwa na maono, uwezo na umahiri wa kiuongozi, pamoja na dhamira ya dhati ya kuwa kiongozi wa watu, niliye tayari kutumia kila fursa, mikakati na mbinu zote za kiuongozi kuboresha maendeleo ya wananchi. Nawiwa kuwa mwakilishi tofauti wa wananchi, nitakayetengeneza tofauti yenye tija kwenye maisha yao, nikitumia weledi na karama zangu za kiuongozi kama ifuatavyo:


Malezi yangu kisiasa ndani ya CHADEMA ndiyo yaliyochochea kiu na dhamira yangu ya muda mrefu katika kuwatumikia wananchi wenzangu bila kutetereka, nikiakisi misingi ya kifalsafa, kiitikadi na kisera ya chama chetu. Ni katika malezi hayo hadi sasa chama chama chetu kimeniamini kuwa ninatosha na kunikabidhi majukumu mbalimbali likiwamo jukumu jipya la kuongoza Idara ya Sera na Utafiti chini ya Kurugenzi husika katika Makao Makuu ya Chama. Nimeutumikia wadhifa huu na ninaendelea kuutumikia kwa uaminifu mkubwa na kwa dhamira na moyo wa kizalendo kwa chama chetu na Taifa kwa ujumla.


Mathalan, kwa kipindi kifupi sana tumeweza kuzindua sera tano mpya za chama ambazo ni Sera ya Elimu (ambayo zaidi ya 75% Serikali ya CCM imeinakiri na kuifanya sera yake ya elimu), Sera ya Maendeleo ya Vijana, Sera ya Afya, Sera ya Uchumi na Sera ya Nishati na Madini. Sera hizi mpya zimetoa mwelekeo bora kabisa wa serikali ijayo itakayoundwa na chama chetu kama sehemu ya Serikali ya Umoja wa UKAWA, serikali inayosubiri kuapishwa miezi saba ijayo.


Naamini, ninao uzoefu wa kutosha kitaaluma na kiutendaji pamoja na ukomavu unaostahili kisiasa katika kubeba wajibu huu wa kuwatumikia wananchi jimboni na pia kubeba ajenda za kitaifa na kutekeleza wajibu wa ziada mbali na wajibu wa mbunge kama ilivyo kikatiba.
Nimekulia na kusoma katika mazingira ya kawaida kabisa ya vijijini ambako wanaishi zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania. Nimesoma Shule ya Msingi Hiti iliyopo Kijiji cha Mrere wilayani Rombo na kujiunga na Shule ya Sekondari Lyamungo kabla ya kujiunga na masomo ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Galanos mkoani Tanga.


Mwaka 2005 kwa udhamini wa Serikali ya Tanzania nilijiunga na Chuo Kikuu cha Allahabad nchini India na kusomea Shahada ya Biashara nikibobea katika masuala ya fedha. Mwaka 2008 nilijiunga na Shahada ya Uzamili katika Masuala ya Uchumi (M.A Economics).
Kutokana na mapenzi yangu katika fani ya diplomasia na siasa za kimataifa, nilijiunga na Chuo Kikuu cha Annamalai na kuhitimu Shahada ya Uzamili katika Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa. Kwa sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Sera na Uongozi (Ph.D in Governance and Policy Analysis) kwenye Chuo cha Maastricht nchini Uholanzi.


Ninaelewa adha wanayopata watoto kutoka familia za masikini kwa kuwa nimesoma na kukulia katika mazingira hayo. Na nina uhakika kuwa adha na dhiki zote zinazowasibu Watanzania wenzangu hazitokani na mapenzi ya Mungu, nuksi wala kurogana, bali zinatokana na udhaifu wa kisera na kiuwajibikaji katika mfumo wa utawala wa nchi yetu; mfumo uliolea mataifa mawili ndani ya nchi moja katika sekta za Elimu, Afya, Ajira na nyinginezo – Taifa la mafukara na Taifa lenye nacho; Taifa la wale wanaoweza kusomesha watoto wao kwenye shule bora hasa English Mediums na kutibiwa kwenye hospitali za ughaibuni, na Taifa la akina siye tunaosomesha kwenye shule za kata na kutibiwa kwenye zahanati chache zilizo mbali na zisizo na dawa.


Nitaongeza idadi ya wabunge makini bungeni katika kuvunja matabaka haya mawili na kubakisha Taifa moja lenye kusimamia fursa na mgawanyo wa rasilimali kwa usawa katika kuwawezesha wananchi kujiendeleza!
Katika kupanga na kutekeleza mikakati na vipaumbele vyangu kwa jimbo nitazingatia zaidi maoni na matakwa ya wananchi na ushauri wa kitaalamu.


Ninaamini ninao uwezo wa kubuni, kupanga, kuchanganua, kusimamia na kuandika ripoti za miradi ya maendeleo kutokana na uzoefu wangu wa kiutendaji katika taasisi za fedha, asasi za kiraia na sekta binafsi. Mathalan, hadi sasa nimeshavuka hatua ya awali ya kushirikiana na taasisi ya “Yunus Social Business-Global Initiatives (YSB)’’ yenye makao yake mjini Frankfurt, Ujerumani iliyoanzishwa na Profesa Muhammad Yunus na kubadili hali ya uchumi na maisha ya mamilioni ya watu nchini Bangladesh kwa kutoa mikopo ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana katika sekta mbalimbali.
Nitashirikiana na asasi kama hizi za ndani na nje ya nchi yetu katika kuhakikisha mikakati nitakayoipanga kwa ajili ya wananchi inatekelezeka huku tukiendelea kuibana halmashauri katika matumizi sahihi ya fedha za umma.


Nitajenga hoja na kubainisha mikakati kukishawishi chama changu kwanini tunaweza kufanya vizuri zaidi. Tutawashawishi wananchi kwanini tunaweza kufanya vyema zaidi kuliko miaka mingine yote iliyopita katika uwakilishi wa nafasi ya ubunge.
Nikipewa ridhaa na chama changu, sitapeleka bungeni ajenda ya kuongezewa posho kwa kisingizio chochote kile, bali nitaainisha vipaumbele, nitashauri na hata kuishinikiza Serikali kwa hatua za kibunge na kiharakati nje ya Bunge kuhakikisha wananchi nitakaowawakilisha wanapata haki wanayostahili.

Sitajisikia fahari kuhudhuria misiba mingi ya wananchi, bali nitajivunia rekodi ya kuhakikisha huduma za afya zinapatikana na kuokoa vifo visivyo vya lazima. Hiki ndicho nitakachojivunia baada ya miaka mitano.
Ninasikitika sana kuona kwamba nchi maskini kama Tanzania inachezea fedha za umma kwa kutoa fedha majimboni, ukaguzi na udhibiti mzuri wa fedha hizo zinazotolewa kwa jina zuri la Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF) ambao unakua chini ya mbunge na DED.


Je, wabunge watakapotumia fedha hizo kwa manufaa yao na hasa kipindi hiki cha uchaguzi ambacho wabunge wengi wanazitumia fedha za umma majimboni kuwaghilibu wananchi kwa misaada ya mifuko ya bati na saruji na kuwahadaa kuwa zimetoka mifukoni mwao sio ufisadi? Ni lazima tupiganie misingi ya uwajibikaji kuanzia ngazi za chini ili pia tuweze kujenga hoja za kuiwajibisha Serikali katika masuala ya maadili hasa dhidi ya tatizo sugu la ufisadi, uzembe na kuacha tabia ya kulindana.


Sheria kandamizi zisizokuwa za haki na zilizopitwa na wakati zitakuwa adui yangu mkubwa ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria nchini. Ni lazima nihakikishe kwa nafasi yangu Bunge letu linasimama na kutetea haki ya Watanzania na kurejesha heshima ya kibunge na kitaifa miongoni mwa mabunge mengine duniani. Sitatetea sheria hata kama ina maslahi binafsi kwangu.


Kwa mfano sheria na kanuni zinazoruhusu wabunge kulipwa mafao yao baada tu ya kumaliza muda wao wa kibunge ni sheria chochezi katika ufisadi na rushwa kwenye uchaguzi. Ni kwanini wabunge wasilipwe baada ya uchaguzi ili kuhakikisha kuwa hakuna mianya ya rushwa katika uchaguzi wetu? Watumishi wa umma hasa walimu na madaktari wanalipwa mafao yao miezi sita baada ya kustaafu na wanavumilia; je, kwanini wabunge wasivumilie?


Katika Bunge linalomaliza muda wake, miongoni mwa wabunge waliotekeleza kwa weledi wajibu wao wa kibunge ni wabunge vijana. Ninapotangaza uamuzi wangu huu, ninasimama juu ya mabega ya baadhi ya kaka na dada zangu waliotuwakilisha vyema ndani ya Bunge la 10 linaloelekea ukingoni.
Wengi wao nimefanya nao kazi kwa karibu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge kulingana na nafasi yangu. Ni muda wangu sasa kuomba ridhaa ya chama changu ili niweze kupata ridhaa ya wananchi katika safari hii mpya tunayoianza, safari ya utumishi wa kweli kwa wananchi wa jimbo langu na Watanzania kwa ujumla.


Pili, ninazo sifa za jumla na vigezo vyote vilivyotajwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 67(1).
Tatu, tangazo langu hili la “Naelekea Bungeni” linazingatia ukweli kuwa mpaka sasa nimeshafanya kazi kubwa iliyozaa matunda ya kuimarika kwa mtandao wa chama changu katika jimbo ninalokusudia kugombea na kuchangia kwa kiasi kikubwa chama changu kufanya vizuri kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita kama kilivyofanya vizuri pia maeneo mengi nchini. Naomba tuendelee kuidumisha nguvu hii kubwa ya uungwaji mkono kuelekea kura za maoni na hatimaye nitaunda timu ya kampeni kabambe kuelekea bungeni Oktoba 2015.

 

Ben Sanaane ni miongoni mwa viongozi vijana ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwa na dhamira ya kushika nafasi ya Mbunge wa sasa wa Rombo, Joseph Selasini ambaye pia anatokana na CHADEMA.